28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Mganga Mkuu Dar aeleza mikakati kukabili ebola

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Yudas Ndugire, ametoa tahadhari kwa wakazi wa mkoa huo kuwa makini pindi wanapompokea mgeni anayetoka katika nchi zinazotajwa kuwa na ugonjwa wa ebola.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Agosti 30 kuitaja Dar es Salaam kuwa mmoja wa mikoa iliyopo hatarini kwa ugonjwa huo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Dk. Ndugire alisema iwapo mkazi ataona dalili zozote, ni vema akatoa taarifa haraka katika mamlaka husika.

“Ni kweli mkoa huu umetajwa kuwa kati ya mikoa nane iliyo hatarini na ebola, hii ni kutokana na Dar es Salaam kuwa mji mkuu wa kibiashara na una mwingiliano na watu kutoka katika nchi mbalimbali.

“Hivyo lazima kila mtu awe makini, hasa pale anapompokea mgeni kutoka katika nchi zinazotajwa kuwa na ebola kama Uganda, Wilaya ya Kasese na Congo, unapoona ana dalili za kutoka damu sehemu mbalimbali, homa kali, kutapika, usimpime kwa mikono wala kumgusa, nenda katoe taarifa katika mamlaka husika,” alisema Dk. Ndugire.

Alisema mkoa umeshaanza kuchukua tahadhari kwa kuunda timu ya uratibu ili ugonjwa usiingie pamoja na timu ya matibabu na vifaa.

“Dar es Salaam haipo mpakani, lakini kuna uwanja wa ndege na pia stendi kubwa ya mabasi yanayotoka nje ya nchi, tumeunda timu ya uratibu ambayo kazi yao ni kuratibu timu nzima katika mapambano ya kuzuia ebola kuingia.

“Sehemu kama airport wapo maofisa afya ambao wanafuatilia mienendo ya watu wanaotoka nje ya nchi, na hapo kuna vifaa maalumu vimefungwa vinavyohisi mgonjwa mwenye joto kali.

 “Pia timu za matibabu zimeundwa kwa ngazi za manispaa na tayari wanapewa mafunzo, vilevile kuna jengo limeandaliwa katika Hospitali ya Temeke, kwa wagonjwa watakaohisiwa watapelekwa pale,” alieleza Dk. Ndugire.

Alisema tayari wameshaanza kutoa elimu kwa wanachi kuhusu dalili za ugonjwa huo na namna ya kuuepuka.

 “Elimu imeanza kutolewa kwa njia ya vipeperushi vyenye kuonyesha picha, hatua gani mwananchi anachukua akihisi kuna ugonjwa wa ebola, pia hata kwa njia ya vyombo vya habari tunatoa elimu,” alisisitiza Dk. Ndugire.

Agosti 30, mwaka huu, Wizara ya Afya ilitaja mikoa ya Kigoma, Mwanza na Kagera kuwa katika hatari zaidi huku mikoa ya Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Dodoma na Dar es Salaam ikitakiwa kuchukua tahadhari zaidi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) Julai 17, mwaka huu lilitangaza kuwa mlipuko wa ebola ni janga linaloathiri afya ya jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles