27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Mfupa uliomshinda Mapalala atauweza Lipumba?

Profesa Ibrahim Lipumba akihutubia wananchi.
Profesa Ibrahim Lipumba akihutubia wananchi.

Na ELIZABETH HOMBO,

KWA takribani miaka 22 sasa historia ya mapinduzi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) inajirudia, tangu waasisi wake, Maalim Seif Shariff Hamad na James Mapalala walipohitilafiana mwaka 1994.

Awali wawili hao waliunganisha vyama vyao kuunda CUF mwaka 1992, lakini miaka miwili baadaye uhusiano wao ukaingia shubiri na kuishia Mapalala kufukuzwa.

Wanasiasa hao wakongwe kabla ya kuhitilafiana kisiasa, walifanikiwa kutengeneza chama kilichopata umaarufu mkubwa na kuhesabiwa kama mbadala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Historia hiyo safari hii inamhusisha Maalim Seif na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mwanazuoni msomi, ndiye aliyepewa heshima kubwa ndani ya chama hicho kwa kugombea urais mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010.

Tofauti zilizojitokeza baina ya wanasiasa hao kuanzia Mapalala, Maalim Seif na Lipumba kwa mtazamo wa ndani unaonyesha kuw apo na dhana ya ‘mkono wa mtu’.

Dhana hiyo imezungumziwa enzi za Mapalala na leo inazidi kunadiwa kuwa chanzo cha kutoelewana kwa wanasiasa hawa ni mashinikizo yanayotoka nje ya chama.

Wakati wa Mapalala, vurugu zilianza kuiandama CUF kiasi cha kuwapo habari kuwa miongoni mwao yupo aliyerubuniwa na chama tawala ili kukipunguza kasi chama hicho.

Hatimaye Mkutano Mkuu wa CUF ulimvua uanachama Mapalala mwaka 1994, ambaye alikuwa akimshutumu Maalim Seif kwamba alikuwa ni kiongozi anayetamani kurejesha Utawala wa Kisultan Visiwani Zanzibar.

Maalim naye alielekeza lawama kwa Mapalala kuwa amekuwa kibaraka ndani ya chama hicho aliyetumwa kukipunguza nguvu ili CCM ikose mpinzani wa kweli.

Kutokana na kusambaratika huko, baadaye ikawa faida kwa Chama cha NCCR-Mageuzi kuwa chama cha pili baada ya CCM.

Baadaye chama hicho cha CUF kikapoteza nguvu Tanzania Bara na kikabaki na uhai Visiwani Zanzibar.

VURUGU ZA LIPUMBA

Profesa Lipumba alijiuzulu nafasi yake ya uenyekiti Agosti mwaka jana, huku matarajio ya wengi wakati huo wakiamini kuwa mbobezi huyo wa uchumi angetumia taaluma yake kulisaidia Taifa kupitia ushauri.

Lakini kinyume na matarajio ya wengi, msomi huyo aliibuka na kumwandikia Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif akitengua barua yake ya kujiuzulu.

Itakumbukwa Profesa Lipumba alichukua uamuzi wa kujiuzulu wakati ambao ulikuwa ni wa kipindi kigumu cha kisiasa kwa sababu tayari mbio za kuelekea katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana, zilikuwa zimeshaanza.

Pamoja na mambo mengine, wakati akitetea uamuzi wake wa kujiuzulu, msomi huyo alisema anakerwa na hatua ya Ukawa ambao CUF ni chama shiriki kushindwa kusimamia makubaliano yaliyosababisha kuundwa kwake.

Kwamba umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kulinda masilahi ya wananchi yaliyoainishwa katika Katiba iliyowasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba na kwamba nafsi yake inamsuta kuendelea na uongozi, huku waliokuwa wanaipinga au kuisigina iliyokuwa Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba wakikaribishwa kuwania uongozi wa nchi kupitia umoja huo.

Maelezo yake hayo yalilenga kupinga uteuzi wa mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa, ambaye alijiengua kutoka CCM baada ya jina lake kukatwa katika vikao vya uteuzi wa mgombea urais kupitia chama hicho.

Ni kutokana na barua hiyo ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu ndiyo ambayo sasa inakipitisha chama hicho katika kipindi kigumu.

Ukimya uliokuwapo baada ya barua hiyo kutojibiwa na uongozi wa chama hicho ndio ambao sasa umempa faida Profesa Lipumba kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye Jumamosi iliyopita alitoa msimamo wake juu ya mgogoro uliopo ndani ya chama hicho, kwamba anamtambua Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF.

Siku hiyo hiyo ya Jumamosi baada ya msajili kutoa kile alichokiita ushauri, mbobezi huyo wa uchumi alirudi kwenye ofisi na cheo chake cha zamani kwa msaada wa polisi ambapo aliongozana na wafuasi wake huku wakivunja geti na mlango wa ofisi ili aingie.

Mbali ya milango kuvunjwa, kingine ambacho kimesikitisha ni kitendo cha walinzi waliokuwa getini kupigwa na wafuasi hao wa Lipumba.

Ni jambo la kushangaza kwamba msomi huyo pamoja na heshima aliyojijengea katika jamii, kwanini atumie nguvu kiasi hicho?

Na imekuwaje apewe sapoti kubwa na polisi? Licha ya vurugu zilizofanywa na wafuasi wake huku wakipiga walinzi, polisi hao hawakuchukua hatua zozote.

Lakini pamoja na hilo, je, msajili alikuwa chombo sahihi cha kutafsiri hicho kilichotokea au mahakama?

Je, msajili anateua wenyeviti siku hizi? Na katika hali kama hiyo Lipumba atafanya kazi na nani huko CUF?

Licha ya kwamba Msajili amesema hakumrudisha bali alitoa ushauri kwa kutumia Katiba ya CUF, lakini alitakiwa kutumia busara zaidi ili kutozua kile kinachoonekana sasa.

CUF WALIKUWA SAHIHI?

Lakini kwa upande mwingine ni kwanini CUF walichukua muda mrefu kuitisha vikao vya uamuzi hata kwa dharura, kujadili tukio kubwa na zito kama la kujiuzulu kwa mwenyekiti wao?

Kwanini Katibu Mkuu Maalim Seif alikaa na barua zote hizo mbili pasipo kuitisha vikao vya maamuzi kujadili tukio zito, je, kigugumizi hiki kilisababishwa na nini?

Kwanini kikao cha Mkutano Mkuu Maalumu kilijikita kujadili barua ya kujiuzulu ambayo imepitwa na wakati na kuacha kujadili barua ambayo ndio ilikuwa mpya ya kufuta barua yake ya kujiuzulu?

Kwanini busara haikutumika kumpa muda kujieleza au wajumbe kupiga kura za siri kuamua hatua za kumchukulia, badala yake kutumia zile za wazi?

Kutokana na uzembe huo uliofanywa na CUF pamoja na kwamba walipokea barua ya Lipumba, lakini haikufanyiwa kazi, ndiyo iliyosababisha yote hayo.

Kwamba kwa sababu CUF hawakuweza kumwandikia msajili barua ya ukomo wa mwenyekiti, ndiyo maana bado anamtambua Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Kwa haya yanayoendelea sasa ndani ya CUF ni sinema mpya kuliko baadhi yetu tunavyofikiri, unaweza kuwa mwanzo wa kuparanganyika kwa CUF.

Mbaya zaidi mgogoro huo umekuja wakati kuna hali mbaya ya kisiasa katika ngome yake Visiwani Zanzibar.

Nasema hivyo kwa sababu itakumbukwa kuwa Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alifuta uchaguzi wa Zanzibar, uamuzi uliopingwa na aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF, Maalim Seif huku mara kadhaa akisisitiza kuwa tume hiyo imtangaze kuwa mshindi.

Pamoja na hilo, baadaye ulifanyika uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu huku CUF wakisusa na Dk. Ali Mohamed Shein akaibuka kuwa Rais wa Zanzibar.

Kutokana na hilo, inadaiwa kuwa hali si shwari visiwani humo na kwamba wafuasi na mashabiki wa vyama hivyo hawashirikiani katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Kama hali ndiyo hiyo, ni wazi kwamba itakuwa ni hatari kwa mustakabali wa Wazanzibari.

Lakini wakati huu ambapo CUF wanatumia muda mwingi kwenye mgogoro wa madaraka, wanaweza wakasahau hali hiyo ya Zanzibar na CCM wakatumia mwanya huo.

Kwa sababu hata haya yanayoendelea ndani ya CUF yawezekana kuna mkono wa CCM kuwa pengine ni mbinu za kuiua CUF, japo hakuna uthibitisho.

Hii ni safari mpya ya CUF katika medani za siasa. Lakini kwa upande mwingine inaweza kuwa na madhara hata kwa wasio wanaCUF huko tuendako.

MSAJILI YUKO SAHIHI?

Pia tukimtazama Jaji Mutungi kwa upande mwingine anazidi kudhihirisha malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na upinzani kwamba anakibeba chama tawala.

Kwamba pamoja na yote hayo, kitendo chake cha kutoa msimamo huo haoni kama amezidi kuchochea mgogoro ndani ya chama hicho badala ya kusaidia?

Msajili wa Vyama vya Siasa ndiye mlezi wa vyama vya siasa na vyama ni kama watoto wake, hivyo pale anapoona mambo hayaendi sawa anapaswa kuwasikiliza pande zote au hata wakati mwingine kutumia busara badala ya kuchochea mgogoro.

LIPUMBA ATAFANIKIWA?

Hivi sasa ukipita mitaani, mitandaoni mjadala ni Lipumba na kundi kubwa linamtuhumu kwamba ametumwa na chama tawala kusambaratisha upinzani.

Kwamba lengo lake ni kuhakikisha kuwa CUF kinagawanyika kati ya Tanzania Bara na Visiwani.

Pia kitendo cha Jeshi la Polisi kumsindikiza kurejea ofisini na kuvunja milango kinatafsiriwa kuwa msomi huyo anatumiwa na chama tawala.

Wengi wanahoji kwamba ni kwanini aje wakati huu kuvuruga CUF ambayo imetulia baada ya Uchaguzi Mkuu?

Pia kwanini Lipumba anakuja kupindua maamuzi ya chama wakati kimeshafanya taratibu zote kuhusu umeya wa Kinondoni na Ubungo?

Kwa muktadha huo, ni dhahiri kwamba historia inajirudia kama ilivyokuwa kwa Mapalala, kwamba alitumiwa na CCM kusambaratisha chama hicho, ndivyo inavyotajwa hivi sasa kwa upande wa Lipumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles