Na MWANDISHI WETU-KAGERA
MFUNGWA aliyepata msamaha wa Rais Dk. John Magufuli Disemba 9 mwaka huu kutoka Gereza la Kyakailamo, Bukoba Mkoani Kagera ameua mtu mmoja na kujeruhi watano na yeye kuuwawa.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la kituo kikuu cha mabasi Bukoba mjini juzi usiku.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi alisema mfungwa huyo aliyepata msamaha juzi (hajatambulika jina ) amefariki dunia baada ya kupigwa na watu wenye hasira kali kutokana kufanya unyama huo.
Akieleza tukio hilo ambalo limehusisha mauaji ya watu wawili akiwemo mtu huyo aliyekuwa mfungwa, Kamanda huyo alisema lilitokea juzi saa tatu usiku katika eneo la kituo kikuu cha mabasi cha Manispaa ya Bukoba mjini.
“Mtu huyo alivamia ghafla eneo hilo la stendi na kuanza kuwavamia watu na kuwajeruhi kwa kisu, mtu kwa kwanza kuvamiwa ambaye ni marehemu kwa sasa, maana alifariki pale pale alitambulika kwa jina la Geoffrey Obad ambaye ni dereva bajaji anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30 na 35.
“Marehemu Obadi alipata maafa hayo stendi akiwa katika eneo lake na kazi, alikuwa ameegesha bajaji yake ndipo ghafla huyu mtu akatokea akamvamia na kumjeruhi katika sehemu ya tumboni, jeraha kubwa ambalo lilisambabisha madhara makubwa,
“Lilisababisha sehemu ya utumbo ikatoka na akamjeruhi sehemu ya kwenye paji la uso na kutokana ukubwa wa jeraha marehemu hakuweza kuendelea kuishi hivyo alifariki hapo hapo,” alisema Kamanda Malimi.
Alisema hakuishia hapo mtu huyo aliendelea kuwavamia watu wengine na kuleta taaruki kubwa na hofu katika eneo la kituo cha mabasi.
Alisema katika vurugu zake hizo aliweza kujeruhi watu wengine watano ambao wametambulika kwa majina ya Michael Bukelebe (24), Salumu Athumani na Nasri Abdala (19) (wote ni mafundi magari), Jalia Abdi (40) ambaye ni wakala wa kukatisha tiketi na Jimmy Mishael ( 45) kondakta wa mabasi.
Alisema waliwasiliana na Jeshi la Magereza ambao walithibitisha kuwa alikuwa ni mfungwa katika gereza hilo.
Kamanda Malimi alisema bado wanaendelea kufatilia utambuzi wa mtuhumiwa huyo ingawa naye ni marehemu kwani aliuawa baada ya kushambuliwa na wananchi kwa silaha za jadi.
“Huyu mtuhumiwa (ambaye naye ni marehemu) alikuwa anatumikia kifungo chake katika Gereza za Bukoba alikuwa ni mfungwa wa kufungo kifupi.
“Kilichotufanya tumtambue kuwa ni mfugwa ni kwa kuwa alikuwa anatembe na karatasi yake ya kutoka kifungoni ambayo wanaiita Discharge 4,” alisema Kamanda Malimi.
Tangu Rais Magufuli atangaze kutoa msamaha kwa wafungwa wakati wa sherehe ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu, kumekuwa na wimbi la matukio ya kihalifu yaliyotekelezwa na wafungwa hao waliopatiwa msamaha.