MFUNDISHE MTOTO KUWEKA AKIBA YA FEDHA

0
1065

 

 

NA AZIZA MASOUD,

MZAZI ana nafasi kubwa ya kumfundisha mtoto mambo mbalimbali ambayo yatakuwa  yakimuonyesha njia katika maisha yake.

Yapo mambo ambayo yatambadilisha kitabia na kumjenga kwa wakati huo, pia yapo ambayo yatamsaidia kuwa sawa katika maisha yake ya baadaye.

Taratibu mbalimbali, zikiwamo za mtu kujua kutunza fedha ama kujiwekea akiba hutokana na mazoea na tabia aliyofunzwa ama kuoneshwa akiwa mtoto.

Mazoea hutokana na mafunzo anayoyapata kutoka kwa mzazi akiwa mdogo, mtoto kuanzia miaka saba mpaka 11 anakuwa katika nafasi nzuri kumfundisha jinsi ya kuhifadhi fedha.

Ili uweze kumsaidia mtoto kuwa na utaratibu mzuri wa kuhifadhi fedha mbali na kumfungulia akaunti ya benki ambayo atakuwa anaifahamu, pia unaweza kumwelekeza utaratibu mbadala ambao utamfanya ahifadhi fedha zake ndogondogo.

Hakikisha mtoto anakuwa na chombo maalumu ambacho atatumia kuhifadhi fedha ambazo unampa kwa ajili ya matumizi yake ya kila siku, huku ukimsisitiza zitakuja kumsaidia wakati ujao.

Anza kwakumfanyia majaribio  wa kumpa fedha mfululizo,mfano pamoja na kwamba umemuwekea utaratibu wa kumpa fedha za shule  siku moja jaribu kumnyima  huku ukimsisitiza  kuwa atumie fedha ya akiba aliyonayo.

Kufanya hivyo kutamfanya kuwa makini katika kuhifadhi fedha, kwakuwa atafahamu kuwa ipo siku atahitaji kuitumia.

Mwelekeze jinsi ya kuficha katika sehemu salama ambayo hataisahau wala hakuna mtu yeyote ambayo ataiona.

Ili kumpa hamasa ya kuendelea kuzihifadhi fedha inapofika muda fulani zitakapokuwa nyingi mshauri akanunue kitu kikubwa ambacho anakipenda na kupitia fedha ndogo anazopewa kwa siku hawezi kukinunua.

Lengo la kumfundisha vitu hivyo siyo kwamba unamwelekeza mtoto awe mchoyo, isipokuwa unamfundisha kujua thamani ya fedha.

Pia inaelezwa kuwa, mtoto yeyote anayefundishwa kutunza fedha anakuwa na matumizi mazuri ukubwani.

Mbali na hilo, mtoto pia unamfundisha mtoto kuishi kwa malengo, kwakuwa endapo atazoea utaratibu huo atakuwa na uwezo wa kujipangia kununua vitu ambavyo havina gharama kubwa  kama mpira wa kuchezea na vingine.

Kumfundisha kuishi katika maisha hayo kutamfanya mtoto awe na heshima na fedha, pia atakuwa makini katika matumizi yake ya kila siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here