23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mfumo wa kudhibiti ajali za mabasi waja

Mohamed Mpinga
Mohamed Mpinga

Na PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM

SERIKALI inatarajia kufunga mfumo wa vidhibiti mwendo (Car Trucking System) kwenye mabasi yote yanayokwenda mikoani   kupunguza ajali za mara kwa mara.

Uamuzi huo umefikiwa na Serikali baada ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa awali kupunguza ajali za barabarani kushindikana huku watu wakiendelea kupoteza maisha kila siku.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri Barabarani wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), Johannsen Kahatano, alisema mfumo huo mpya ni mzuri na utakuwa unasimamiwa na polisi na Sumatra.

Alisema mfumo huo ambao ni wa kwanza nchini, utawezesha kuiona gari popote ilipo kupitia chumba maalumu kitakachokuwa kinaratibu mienendo ya mabasi yote yanayokwenda na kutoka mikoani (Control room).

Alisema kwa sasa mkandarasi yupo kwenye maandalizi ya awali ya kutengeneza mfumo huo ambao  unatarajiwa kuanza kazi kabla ya Januari mwakani.

Kahatano alisema katika kipindi hiki ambacho Baraza la Taifa la Usalama Barabarani linatekeleza mpango wa kupunguza ajali nchini, miongoni mwa mambo yanayokusudiwa kufanywa ni kuhakikisha mabasi yote yanafungwa mfumo mmoja ambao utasaidia kuyadhibiti.

“Tunaamini kabla ya Desemba mkandarasi atakuwa amemaliza hatua zote za kufunga mfumo wa kudhibiti mwendo katika mabasi yote yanayokwenda mikoani  jambo ambalo linaweza kupunguza ajali,”alisema Kahatano.

Alisema  mkandarasi huyo amepewa miezi mitatu kuhakikisha anakamilisha kutengeneza mfumo huo ili ifikapo Desemba waanze kufunga mabasi hayo.

Mabasi yote yatakaguliwa na Sumatra kwa kushirikiana na polisi wa usalama barabarani mara kwa mara   kuhakikisha mfumo huo hauharibiwi wala kuchezewa na mtu yeyote, alisema.

Alisema  mabasi yatakayobainika yameharibu mfumo baada ya kufungiwa, madereva na wamiliki wa mabasi hayo watachukuliwa hatua za sheria  iwe fundisho kwa wengine.

Mpaka sasa idadi kubwa ya ajali zinazotokea zinasababishwa kwa kiasi kikubwa na uzembe wa madereva wakiwa barabarani, jambo ambalo limechangia kuongezeka vifo vya watu wasio na hatia.

“Ajali nyingi zinazotokea nchini zinatokana na uzembe wa madereva, hatuwezi kuvumilia, lazima tuangalie mfumo maalumu ambao utadhibiti madereva kwenda mwendo kasi,”alisema.

Katibu wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Tanznaia (Taboa), Enea Mrutu alisema chama hicho kitashirikiana na Sumatra kuhakikisha madereva wazembe wanachukuliwa hatua kali.

Alisema chama hicho kimeunga mkono mkakati wa kudhibiti mwendo jambo ambalo linaweza kusaidia kupunguza ajali zinazojitokeza mara kwa mara.

“Taboa iko mstari wa mbele kushirikiana na serikali kupunguza ajali ikiwa ni pamoja na kufunga vidhibiti mwendo katika magari yote   na ukaguzi wa mabasi na madereva walevi,” alisema Mrutu.

Mbinu za polisi zimegonga mwamba?

Licha ya Jeshi la Polisi kutumia tochi ili kukagua mabasi yaendayo kasi katika maeneo mbalimbali nchini hususani barabara kuu idadi ya ajali za barabarani zinazotokea inaongezeka siku hadi siku.

Hivi karibuni Serikali ilizifungia kampuni 12 na mabasi 60 kutokana na kusababisha ajali za barabarani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles