KUMEKUWAPO na malalamiko ya muda mrefu kuhusu baadhi ya vyuo vinavyotoa masomo ya afya kuwa na sifa ambazo hazikidhi viwango.
Pamoja na kutokidhi viwango, vingi vilikuwa na kasoro kubwa ya kutokuwa na usajili kutoka serikalini na kusababisha wanafunzi wengi kushindwa kutimiza ndoto zao.
Hali hiyo ilikuwa ikisababisha wanafunzi kuandamana kutokana na kuzuiliwa na mamlaka za Serikali kufanya mitihani ya mwisho, licha ya kulipa gharama zote. Jambo hili lilikuwa linatia uchungu kutokana na wazazi au walezi kujitolea kwa hali na mali kuhakikisha watoto wao wanasoma.
Lakini baada ya hali hiyo kuendelea, Serikali imeamua kufanya mapinduzi makubwa ambayo tunaamini yataleta mafanikio na kufungua ukurasa mpya.
Jana tumeshuhudia Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainab Chaula akitangaza mabadiliko makubwa vyuo vya afya kwa kuviunganisha vyote vilivyo karibu.
Uamuzi huu umepunguza idadi ya vyuo kutoka 37 hadi kufikia tisa. Hili si jambo dogo, linapaswa kupongezwa kwani kubaki na vyuo vichache kutasaidia matumizi mazuri ya rasilimali chache zilizopo katika kuzalisha rasilimali watu.
Tunaamini wizara imeona ili kuboresha utoaji taaluma katika vyuo vyake, ni vema ikabadilisha mfumo uliopo wa kuendesha vyuo vidogovidogo na kutengeneza mazingira ya kuwa na vyuo vikubwa vichache vyenye mfumo mzuri wa kiuongozi ili kuzalisha wataalamu sahihi. Haya ni mapinduzi makubwa katika sekta ya afya.
Tunategema sasa kuona wataalamu wa afya wanavyojipanga kuboresha taaluma ndani ya vyuo vya vyao ili kutoa watumishi bora zaidi jambo litakalosaidia kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima kwa Watanzania.
Siku zote kunapotokea mfumo mpya, utaleta taswira bora ya utawala vyuoni na mhimili mkubwa.
Lakini kikubwa kuhakikisha mafunzo bora yanatolewa katika vyuo vyetu na wahitimu wanaozalishwa wanakuwa na umahiri unaokusudiwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Hakuna ubishi kwa kipindi chote hicho, Serikali ilikuwa ikipokea changamoto za uendeshaji wa mafunzo vyuoni, ikiwamo uchache wa watumishi vyuoni, vifaa vya kufundishia, viwango vya ubora wa wahitimu kushuka na ikawa inatafuta njia sahihi ya kupata ufumbuzi.
Jambo kubwa ambalo sasa, tunaliona ni viongozi wa vyuo tisa ambao wamekabidhiwa jukumu hili kuhakikisha wanasimama kidete kushughulikia changamoto ya malalamiko kutoka kwa wazazi na wanafunzi wanaosoma vyuoni, ikiwemo kukosa baadhi ya haki zao.
Sisi MTANZANIA, tunasema mabadiliko haya yamekuja wakati mzuri ambao sasa taifa linaweza kuwa na vyuo vichache ambavyo vitazalisha wataalamu bora.
Tunasema hivyo kwa sababu taifa linahitaji wataalamu wengi wa afya hasa maeneo ya vijijini ambako mamilioni ya Watanzania wanaishi, lakini wanapata tiba kwa shida, licha Serikali kuchukua hatua kuboresha sekta ya afya.
Tunatoa wito kwa wakuu wapya wa vyuo kufanya kazi kwa ushirikiano ili kusaidia na kuleta mageuzi mazuri ya rasilimali chache zilizopo kuzalisha rasilimali watu.
Tunaishauri wizara isirudie makosa yaliyopita ya kuruhusu vyuo vinachipuka kama uyoga na kuacha maumivu kwa wanafunzi ambao wanasoma wakiwa na matarajio makubwa baada ya kuhitimu masomo wakalitumikie taifa.
Tunaamini wapo watakaosikitika katika mabadiliko haya, lakini wanapaswa kukubaliana na ukweli wa mazingira tuliyonayo sasa kwani zama za ujanja ujanja zimepitwa na wakati.