Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania umejipanga kuboresha huduma kwa wasanii na wabunifu katika mwaka wa fedha 2025/26, kwa kuzidisha ubora na ufanisi wa utoaji wa huduma pamoja na kushirikiana na wadau kutatua changamoto zinazowakabili.
Hayo yameelezwa leo Februari 28, 2025, na Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Nyakaho Mahemba, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya utamaduni na sanaa.
Mahemba amesema kuwa mfuko huo unatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha sekta ya sanaa na utamaduni.
“Tumejipanga kuwezesha wasanii wadogo na wachanga kupitia utoaji wa ruzuku ili kuwasaidia kukuza vipaji vyao, hasa kwa wale wasio na uwezo wa kifedha kufanikisha miradi yao,” amesema Mahemba.
Mfuko huo utaendelea kuhakikisha mazingira bora kwa wasanii, wakitilia mkazo ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuimarisha mchango wa sekta ya sanaa katika maendeleo ya taifa.