Mfichua siri wa pili aibuka sakata la Trump,Ukraine

0
538

WASHINGTON, MAREKANI

MFICHUA siri wa pili amejitokeza katika sakata linalomkabili Rais wa Marekani, Donald Trump.

Taarifa hizo zimefichuliwa na wanasheria wanaomuwakilisha ofisa wa kwanza aliyemlipua Trump kuhusiana na mawasiliano ya siri aliyofanya na Rais wa Ukraine yenye nia ya kumwangamiza kisiasa mpinzani wake kuelekea uchaguzi wa 2020, Joe Biden.

Mwanasheria ambaye amebobea katika masuala ya kitaifa ya usalama, Mark Zaid  alikiambia kituo cha ABC News kuwa mtu huyo wa pili naye ni jasusi na kwamba walikuwa wamezungumza na Inspekta mkuu.

Ofisa huyo wa usalama ambaye ni wa pili kuibuka katika sakata hilo amesema ana taarifa zinazounga mkono madai ya mfichua siri wa kwanza kuhusu mazungumzo ya simu ya Rais Trump na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy.

Mark Zaid ambaye ni wakili wa mfichua siri wa kwanza, amesema mfichua siri huyo wa pili ana taarifa za kuaminika zinazomuunga mkono mfichua siri wa kwanza, kwamba Trump alimshinikiza Zelenskiy kumchunguza aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden pamoja na mwanawe wa kiume.

Haijajulikana bado iwapo ofisa huyo wa pili naye anawakilishwa na Zaid.

Hata hivyo, Trump na wafuasi wake wameyakanusha madai hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema ofisi yake itafuata sheria kwa kutekeleza ombi la bunge la Marekani la kuwasilisha nyaraka kama sehemu ya uchunguzi dhidi ya Trump.

Wiki iliyopita Kamati za Bunge la Marekani zinazoendesha uchunguzi dhidi ya Rais Donald Trump ziliiamuru Ikulu ya White House kuwasilisha nyaraka zote za mawasiliano kati ya Trump na Ukraine.

Amri hiyo ilitolewa baada ya Ikulu ya Marekani kushindwa kuchapisha kwa hiyari nyaraka hizo kabla ya kumalizika kwa muda wa mwisho juzi  Ijumaa.

Mmoja wa viongozi wa kamati za Bunge la Marekani alisema ni wazi Rais Trump amechagua njia ya kuficha ukweli baada ya kushindwa kwa mwezi mzima kuweka wazi nyaraka za mawasiliano yake na Ukraine.

Wiki hiyo hiyo Rais Trump alikaririwa akisema huenda asitoe ushirikiano kwenye uchunguzi dhidi yake ambao unahusu madai kwamba alimshinikiza rais wa Ukraine kumchunguza makamu wa rais wa zamani Joe Biden na mwanawe kwa tuhuma rushwa.

Trump ambaye tayari anakabiliwa na shutuma hiyo inayoweza kumwondoa madarakani, katika hali ya kushtua aliibuka na kauli mpya akiitaka China  nayo imchunguze mpinzani wake huyo, Biden

Hatua yake hiyo ilijiri siku chache baada ya mazungumzo ya siri ya simu ya Trump na Rais wa Ukraine kunaswa.

Mazungumzo ya simu kati ya rais Trump na kiongozi wa Ukraine Rais Volodymyr Zelensky,Julai 25 yalisababisha wapelelezi kupeleka taarifa zinazoweza kumuondoa Trump madarakani.

Ingawa Alhamisi wiki iliyopita Rais Trump alidai kuwa madai hayo ni upuuzi.

Katika ujumbe wake wa usiku wa manane kupitia kurasa yake ya Tweeter, Trump aliongeza kuwa yeye ana jukumu la kuchunguza kashfa za rushwa, jambo ambalo linajumuisha kuuliza na kutoa mapendekezo kwa nchi jirani kutoa msaada.

Trump anamshutumu Biden na mtoto wake Hunter kwa kashfa za rushwa katika mikataba yao ya kibiashara na kisiasa nchini Ukraine na China,

Wakati ambao Hunter Biden alipoingia katika mkataba wa gesi asilia katika katika kampuni ya Burisma mwaka 2014, maswali mengi yaliibuka kuwa anaweza kumletea mgogoro kisiasa baba yake.

Ukraine ilikuwa inakabiliana na mgogoro wa kisiasa baada ya kiongozi wake kulazimishwa kuondoka madarakani, wakati huo Biden alikuwa Makamu wa Rais katika utawala wa Barack Obama.

Mwaka 2016, Biden aliishinikiza Serikali ya Ukraine kumfukuza mwendesha mashitaka Viktor Shokin, ambaye ofisi yake ilikuwa inaichunguza kwa karibu mmiliki wa kampuni ya Burisma.

Katika hotuba yake mwaka jana Biden alijisifia kwa kumfukuza Shokin na kutishia kutotoa mkopo wa mamilioni ya fedha kwa Ukraine.

Trump na washirika wake wanamshutumu Biden kwa kumlinda mwanae.

Kama maofisa wengine wa Serikali ya Ukraine pia walitaka Shokin aondoke madarakani kwa sababu ya jitihada zake za kukabiliana na rushwa.

Wiki mbili zilizopita mwendesha mashtaka nchini Ukraine ambaye alichukua wadhifa wa Shokin aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kuwa hakuna ushaidi wa uovu alioufanya Biden au Hunter Biden.

Trump alipohojiwa kuhusu mazungumzo yake ya simu na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky alijibu kuwa; jibu ni rahisi kuwa ;

“Nilidhani kuwa wameanza kufanya uchunguzi tayari kama kweli walikuwa na nia njema basi wangeanza kumchunguza Biden,”

“Vilevile, China pia inapaswa kuanza kumchunguza Biden kwa sababu kile kilichotokea China ni sawa na kile kilichotokea Ukraine”, Trump aliongeza.

Msemaji wa Biden wa kampeni za mwaka 2020 amemshutumu Trump kwa kutumia vibaya televisheni ya taifa kwa kutoa taarifa za kusadikika.

Naye msemaji wa Hunter Biden ameviambia vyombo vya habari vya Marekani kuwa kiwango cha dola bilioni 1.5 ni hesabu ya uongo, hawajahi kupokea fidia yoyote ya malipo ya kiwango hicho cha fedha katika kiwanda chochote China.

Mwaka 2013,  Biden alipokuwa makamu wa rais alipofanya ziara ya kikazi nchini China na kukutana na rais wa nchi hiyo, Xi Jinping, Hunter Biden na binti yake waliongozana naye.

Biden alikuwa makamu wa rais wa kwanza kuongozana na familia yake katika shughuli za kikazi.

Katika ziara hiyo ya siku mbili , Hunter alikutana mfanyakazi wa benki wa nchini humo, Jonathan Li, ambaye baadae akawa mshirika wake katika biashara.

Li alipata ufadhili binafsi muda mfupi tu baada ya ziara hiyo ingawa msemaji wa Hunter alikiambia chombo cha habari cha NBC News kuwa hawakujadili masuala yoyote ya kibiashara katika ziara ile na ufadhili ulikuja miezi michache baadae.

Hunter amekanusha kuwa na mkutano wowote kuhusu biashara na ofisa wa China.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here