Mfanyakazi ubalozi kortini makosa 16, ikiwamo utakatishaji

0
601

ERICK MUGISHA-DAR ES SALAAM

MFANYAKAZI wa Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Athanas Madebe amepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na makosa 16 likiwamo la utakatishaji.

Wakili Mkuu wa Serikali, Wakyo Saimon akisaidizana na Wakili Elia Athanas kwa nyakati tofauti jana walimsomea hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Rashid Chaungu.

Walidai katika shtaka la kwanza hadi la saba kosa la kughushi Oktoba 1, 2014 na Desemba 31, 2016 katika Ubalozi wa Tanzania ofisi za Addis Ababa, nchini Ethiopia akiwa kama Muambata Fedha na Ushirikiano wa Kimataifa alitengeneza nyaraka ya benki.

Anadaiwa kupitia nyaraka hiyo, alidai kuwa Akaunti namba 1000001080017 inayoendeshwa na ubalozi wa Tanzania katika benki ya biashara ya Ethiopia ina akiba ya Dola za Marekani 472,787.91.

Katika shtaka la nane na tisa kati ya tarehe Februari 25, 2017 katika Ubalozi wa Tanzania ofisi za Addis Ababa, nchini Ethiopia akiwa kama Muambata wa Fedha na Ushirikiano wa Kimataifa anadaiwa kughushi nyaraka za Benki ya Commercial.

Kwamba Akaunti 1000001080017 inayoendeshwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia ina dola za Marekani 80,829.35 huku ikionyesha iliwekewa dola 80,000 ambazo ziliamishwa kwenda akaunti maalumu ya Benki ya Tanzania (BoT).

Katika shtaka la 10 kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri wake kati ya Februari 28, 2017 katika ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia anadaiwa alitumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya muajiri wake kwa kuonyesha dola za Marekani 236,000 nje ya dola 472,684.09 zimetoka Shirika la Umoja la Amani Afrika na kuingia kwenye Akaunti ya Tanzania (BoT).

Katika shtaka la 11 la kughushi, Machi 3, 2017 katika ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia anadaiwa alighushi nyaraka  ikionyesha Akaunti 1000001080017 inayoendeshwa na Ubalozi wa Tanzania  Addis Ababa, Ethiopia katika benki ya bishara Ethiopia aliweka dola 76,789.15 na dola 76,000 ilihamishwa kutoka Benki ya Tanzania (BoT).

Katika shtaka la 12 kati ya Mei 2, 2019 na Juni 3, 2019 katika ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia akiwa kama mfanyakazi wa Muambata anadaiwa kuiba fedha kiasi cha dola za Marekani 14,422.20 mali ya Jamhuri.

Katika shtaka la 13  ambalo ni la wizi inadaiwa Julai 1, 2019 katika ubalozi wa Tanzania Addis Ababa, Ethiopia akiwa kama Muambata wa Fedha aliiba dola za Marekani 1,330 na ETD 289,900 ikiwa ni thamani ya Sh milioni 25 mali ya Jamhuri.

Katika shtaka la 15  la utakatishaji fedha ambapo kati ya Mei 3, 2019 na Agosti 31, 2019 katika ubalozi wa Tanzania Addis Ababa, Ethiopia anadaiwa  alijipatia fedha dola za Marekani 15,752.20 na ETD 289,900 huku akijua ni mapato ya Serikali.

Katika shtaka la 16 anadaiwa kati ya Aprili 5, 2013 na Juni 30, 2015 katika ubalozi wa Tanzania Addis Ababa, Ethiopia alisababishia hasara Jamhuri dola za Marekani 472,684.09.

Wakili Mkuu wa Serikali Wakyo alidai upelelezi wa shauri hilo unaendelea na kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa kuja kutajwa tena.

Hakimu Chaungu alisema mshtakiwa hataruhusiwa kujibu kitu chochote na atakuwa akitokea rumande kwa kutokuwa na dhamana katika mashtaka yake na atarudi tena mahakamani kwa kutajwa Januari 14.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here