23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Mfanyabiashara Dar mbaroni kwa tuhuma dawa za kulevya

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA mkubwa Dar es Salaam aliyetambuliwa kwa jina la Abuu Kimboko, ambaye pia ni mmiliki wa magari yaliyoandikwa Mashallah, anashikiliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa tuhuma za kujihusisha na kusafirisha dawa hizo.

Kimboko, inadaiwa kuwa amekuwa akitafutwa na vyombo vya usalama nchi mbalimbali kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo na hatimaye amenaswa na sasa anashikiliwa wakati taratibu zikiendelea ili aweze kufikishwa mahamani.

Akizungumza juzi Dar es Salaam, Kaimu Kamishna Jenerali wa DCEA, James Kaji, alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamtwa Desemba 29, mwaka jana maeneo ya Mbagala Zakiem, akiwa na dawa za kulevya aina ya Heroin gramu 400 pamoja na bastola moja na risasi za moto 15 na vyote amekutwa navyo akiwa kwenye gari namba T 568 DKC aina ya Toyota Spacio.

“Huyu jamaa alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu sana, na si Tanzania tu bali hata nchi nyingine nako walikuwa wanamtafuta kutokana na kujihusisha na biashara hii haramu. 

“Kwa namna ambavyo mamlaka na vyombo vya ulinzi na usalama tumejipanga vema katika mapambano ya dawa za kulevya, tumemnasa na sasa tunamshikilia.

“Kwa wanaomfahamu huyu Abuu kwa jina lingine la mjini tunaita Kipusa, ndiyo anamiliki magari yaliyoandikwa Mashallah,” alisema Kamishna Kaji.

Mbali ya mtuhumiwa huyo, alisema kuwa pia mamlaka hiyo inamshikilia Pascal Lufunga ambaye anatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya.

Alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa eneo la Bwilingu Kibaha akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 133.33.

Kaimu Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, alisema watuhumiwa hao wote wako ndani na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Alisema kwa mwaka 2019, mamlaka hiyo wamefanikiwa kufanya operesheni mbalimbali na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya kiasi cha kilo 325.69 za bangi zikiwahusisha watuhumiwa wawili, kilo 892.24 za mirungi zikiwahusisha watuhumiwa tisa na kilo 34 .47 za heroin zikiwahusisha watuhumiwa watano.

Kuhusu kesi za dawa za kulevya, alisema kuwa 35 zimemalizika katika Mahakama Kuu na dawa zilizohusika na kesi hizo zilishateketezwa.

Pia alisema kuwa pale ambapo Jamhuri haikuridhika na maamuzi au adhabu iliyotolewa kwa washtakiwa wa dawa za kulevya haikusita kukata rufaa.

Akitolea mfano alisema Jamhuri ilikata rufaa Mahakama Kuu kupinga faini ya Sh milioni moja aliyopewa Mustafa Juma Khamis na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin gram 40.16 ndani ya chumba chake.

Kamishna Kaji alisema kuwa msingi wa rufaa ya Jamhuri ni kwamba kiasi cha faini alichotozwa mtuhumiwa hakiendani na adhabu mbadala ya kifungo cha miaka 30 jela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles