25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Mfanyabiashara aliyehukumiwa kulipa bil 24/- atiwa hatiani tena

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA Mohammed Yusufali aliyeamriwa kulipa zaidi ya Sh bilioni 24 wiki iliyopita, ametiwa hatiani tena katika kesi nyingine na kukubali kurejesha Sh milioni 101.5 kwa kosa la kusababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya Sh bilioni 2.9.

 Mshtakiwa Yusufali alitiwa hatiani kwa mara ya pili jana Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Lilian Mashaka baada ya kukiri kosa.

Mshtakiwa huyo aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa yake. 

Baada ya kukiri, Wakili wa Serikali Mkuu, Pendo Makondo alidai mshtakiwa ni mkosaji kwa mara ya pili kwani alishatiwa hatiani na mahakama hiyo katika kesi namba 6/2019 kwa makosa ya kuisababishia hasara mamlaka hiyo.

“Pamoja na adhabu itakayotolewa na mahakama, naomba mahakama itoe amri kwa mshtakiwa kulipa fidia ya sh milioni 100,” aliomba Makondo.

Akiomba kupunguziwa adhabu, Yusufali aliomba mahakama isimpe adhabu kali kwakuwa amezingatia msamaha wa Rais na aliingia makubaliano na DPP kwa hiyari yake.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo aliondolewa mashtaka  ya kula njama, kughushi, kufanya biashara bila leseni na utakatishaji fedha na kusomewa mashtaka mawili ya kukwepa kulipa kodi na kuisababishia hasara TRA.

Mbali na Yusufali, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Alloycious Gonzaga na Isaack Kasanga ambao jana hawakukiri makosa hayo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Hashim Ngole, akisoma maelezo ya awali, alidai pamoja na mambo mambo mengine, mshtakiwa akiwa na wenzake Gonzaga na Kasanga, walishirikiana kutenda makosa hayo.

Ilidaiwa mwaka 2010, Yusufali na wenzake hao waliunda mpango wa kufanya biashara isiyo halali ya kukopesha fedha kwa umma na Machi 4 mwaka 2011 walianzisha kampuni iliyoitwa Superial Finacing Solution (SFS) na kuisajili Brella wao wakiwa kama wanahisa na wakurugenzi.

Machi 11, 2011 kampuni hiyo ilipata leseni ya biashara Manispaa ya Kinondoni iliyowapa mamlaka ya kufanya biashara ya kutoa ushahuri wa kifedha kwa manispaa hiyo tu na kwamba ukopeshaji fedha kwa lengo la kupata faida haikuwa miongoni mwa mamlaka waliyopewa.

Ilidaiwa mshtakiwa huyo na wenzake walipata namba ya usajili ya mlipakodi (TIN) kutoka TRA Ilala na kuanza biashara ya ukopeshaji fedha kwa riba Kinondoni tofauti na Tin waliyopewa.

Ilidaiwa mwaka 2016 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilipata taarifa na uchunguzi ulibaini biashara hiyo iliendeshwa bila leseni na kulipiwa kodi stahiki.

Ilibainika kuwa kwa vitendo hivyo, Yusufali na wenzake waliisababishia TRA hasara ya Sh 2,983,310,039.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, mahakama iliamuru mshtakiwa  kwa kosa la kwanza alipe faini shilingi milioni moja au jela miaka miwili, shtaka la pili faini Sh 500,000 au jela miaka mitatu, pia alipe fidia ya Sh milioni 100 TRA na tayari ameshailipa.

Yusufali wiki iliyopita aliamuriwa katika kesi nyingine kulipa zaidi ya Sh bilioni 24 na tayari amelipa Sh bilioni moja, zilizobakia atalipa kwa makubaliano waliyofikia na DPP.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles