25.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Mfahamu Jamal April ‘Professor’ wa The Story Book anayeikubali singeli

KARIBU kwenye safu hii inayokupa nafasi ya kuwafahamu mastaa mbalimbali kwa kuwauliza maswali. Leo tupo na Jamal April maarufu kama Professor, bosi wa Wasafi Tv na mtangazaji wa kipindi maarufu cha The Story Book.

SWALI: Aidani Michosa wa Mbande Dar anataka kufahamu historia yako mpaka ulivyoingia kwenye tasnia ya habari?

Jamal April: Kila binadamu ana kipaji chake ila nashukuru mimi nilikitambua kipaji changu mapema ambacho ni muelimishaji, kama ninavyopenda kujitambulisha kwa watu kama muelimishaji, mwandishi wa habari na mwanahistoria.

Sikuwa navutiwa kuelimisha watu nikiwa kama mwalimu wa darasani nilikuwa nataka nisiwe na mipaka ndio maana unaona sasa hivi nafundisha watu kwenye The Story Book, nafundisha mambo ya kisayansi, kihistoria, kiusalama na vingine vingi, napenda nikifungua mdomo wangu niwe nanena kitu kinachoacha alama kwa watu.

Pili mama yangu alikuwa mwandishi wa habari alikuwa anafanya kazi TVT sasa hivi TBC alikuwa anafanya kipindi kinaitwa Familia na pia redio Uhuru na hata nikiwa shule ya msingi nilikuwa nashiriki kwenye kazi zake na kutazama kile anachokifanya hiyo ilinisukuma sana kuingia kwenye tasnia hii.

SWALI: Elizabeth Masiye wa Dodoma anataka kufahamu unadhani kwanini The Story Book imekuwa kipindi pendwa cha TV hapa Bongo kwa sasa?

Jamal April: Nadhani kwa sababu ni kipindi tofauti na vipindi vyote vya runinga kwa Afrika nzima kwa maana ya uwasilishwaji wake. Watu wengi wanafanya simulizi lakini je unachimba mambo kwa kina kiasi gani, sifa kubwa ya The Story Book, tunaweza kuchimba mambo na kuzama ndani mno kuliko mtu yeyote aliyewahi kufika au kama kuna mtu alifika tulipochimba sisi basi sisi tunatofautiana kwenye engo ya kuchambua mambo ninayofanya kwenye The Story Book hiyo inaleta upekee sana.

Pia na kuweza kufikiri tofauti kwa namna mbadala kwahiyo watu wanasikia vitu vipya ambavyo hawajawahi kusikia kabla, watu wanafurahia hiyo. Tunafanya tafiti kubwa mno lakini uteuzi mzuri wa nini cha kuzungumza, hii dunia ina vitu vingi sana sasa kwenye The Story Book tunachagua kilicho sahihi ambacho watu wanataka kusikia.

SWALI: Edwin Mushi wa Arusha Mjini anauliza: “Umeshafanya simulizi nyingi kwenye kipindi chako, je simulizi ipi ya kutisha unayoikumbuka?”

Jamal April: Nimefanya simulizi nyingi lakini ile ya Freemasons kwa sababu wanaaminika kama jamii ya siri ya watu waovu kwahiyo chochote utaakacho zungumza kuhusu wao, watu wanakuwa na hofu kwamba wenyewe watakufanya nini wakikusikia kwa sababu inaaminika wanatoa kafara na wanaua watu kwahiyo hiyo ilinitia hofu.

Pia hivi karibuni nimefanya simulizi ya Samatha Lwethwaite ‘The White Widow’ yaani Mjane Mweupe, ambaye ni kiungo muhimu katika kundi la kigaidi la Al-Shabaab kwa mujibu wa mashirika ya Kimataifa ya kijasusi kwahiyo historia kama hiyo inanitia hofu.

Pia nimefanya simulizi ya kuhusiana na shambulio la Septemba 11, na nikasema nikaenda na mtazamo kwamba lile shambulio lilipangwa na serikali ya Marekani wenyewe na sio Osama sasa unaposema mambo kama hayo kuhusu watu wenye nguvu duniani inatia hofu kidogo ila sisi huwa tunazungumza katika hali ambayo haihitimishi ila tunamuacha mtu ambaye anasikiliza afanye hitimisho mwenyewe.

SWALI: Sharif Hamis wa Zanzibar anauliza: “Unapata changamoto gani unapoandaa The Story Book.”

Jamal April: Changamoto ya kwanza ninayoipata ni unahitaji kusoma sana, inahitaji kutulia na kwa bahati mbaya mimi ni Mkurugenzi wa Wasafi Tv na majukumu ya kazi ni mengi sana kiasi kwamba napata muda mchache wa kupumzika, hiyo ni changamoto chanya pia watu wanategemea kusikia na kutegemea vitu vikubwa kutoka kwangu na mimi sitaki kuwaangusha, kwahiyo kila siku natafuta namna mpya ya kufikiria vitu ila ninafurahia.

SWALI: Leonard Simwiche wa Mbeya anauliza: “Mbali na kusikiliza muziki wa Diamond, unapenda kusikiliza nyimbo za wasanii gani nje ya WCB?”

Jamal April: Mimi napenda sana muziki nje ya wasanii wa WCB, napenda kusikiliza muziki wowote mzuri sina ile ya kujifunga kwamba mimi ni shabiki wa msanii fulani na fulani lakini napenda sana wasanii wenye uwezo wa kuimba na utundu kwenye uandishi.

Wanaotoa nyimbo ambazo mtu ukisikiliza mashahiri yake na jambo la kushangaza huwa napenda sana singeli zile stori zao, kama kisimu changu laini mbili kinanisevu bwana (Mzee wa Bwax -Kisimu) au utatoa hutoi (Dulla Makabila- Ujaulamba) au mchumba mbona hutokei (Balaa Mc-Nakuja), nikisikiliza nyimbo kama hizo kwa kuwa huwa nafanya kazi nyingi za kuumiza kichwa basi nafurahia sana.

SWALI: Joseph Pascal wa Mtwara anauliza : “Uhusiano wako na Mtiga Abdallah upo vipi kwa sasa maana inasemekana mpo kwenye bifu zito.”

Jamal April: Mimi ndio nimemtengeneza Mtiga Abdallah, vile unavyomsikia midondoko yake na Mungu amemjalia ana sauti nzuri sana lakini zile njia za usimuliaji nilimmezesha mimi kwahiyo huwezi kuwa baba ukamchukia mtoto wako kwahiyo sina tofauti naye na kubwa zaidi mimi sio mtangazaji tu ni kiongozi kwenye chombo cha habari, nafasi ambayo haifananii kuwa na ugomvi wa mtu.

SWALI: Catherine wa Ilala, Dar es Salaam anauliza : “Starehe gani unapenda kufanya nje ya kazi zako na mtu akitaka kukuona anakupata vipi?”

Jamal April: Mimi starehe yangu ni tofauti kidogo, mimi sipendi kutembea ni mtu wa kukaa ndani hasa hali ya hewa ya Dar es Salaam ya jua kali ndio kabisa. Wikiendi mara nyingi nakuwa nimejifungia tu ndani natazama Tv, naangalia filamu au tahmthilia ya kizamani zinazozungumzia historia kama vile Spartacus hapo naweza kuelewa maisha ya Roma yalivyokuwa pia makala za watu mashuhuri huwa nafurahi starehe yangu ni kuijaza akili yangu vitu vipya ila ninapokuwa na marafiki napenda sana kucheza Play Station, napenda sana kucheka na hii huwa napenda nikiwa kazini na wafanyakazi wenzangu.

Kuhusu kunipata naandaa utaratibu wa kuifikia jamii kwa makundi yao kama wanafunzi wa sekondari na vyuo, watu wenye mahitaji maalum kama wagonjwa, kina mama wajasiliamali, watoto yatima wanaoishi kwenye mazingira magumu na vijana wenye ndoto kubwa za mafanikio nikishirikiana na taasisi zingine na Wasafi Media.

SWALI: Rosemary Jacob wa Buzurugwa Mwanza anauliza: “Umeoa kama ni ndio unaweza vipi kubalansi kazi na kuhudumia familia?”

Jamal April: Mimi bado sijaona, unajua kwenye umri nilionao sasa hivi nina miaka 29 ni umri wa kutengeneza maisha kwahiyo hata familia yangu inajua kwamba natengeneza kesho yangu, naweza nikavumilia nisikutanae na familia yangu kwa muda hata wiki mpaka miezi huko ila tunazungumza kwenye simu na wao wananipa nafasi ya kutengeneza ‘future’ yangu mpaka pale nitakapokuwa nimeoa nataka saa 11 jioni nipo na familia mpaka kesho yake tena kazini ila sasa natengeneza ‘future’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,454FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles