OSCAR ASSENGA, TANGA.
KUFUTIA wimbi la vibaka katika Jiji la Tanga, Mstahiki Meya wa jiji hilo, Alhaji Mustapha Selebosi amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa kumpatia ulinzi ili asidhuriwe na vibaka ambao wamekuwa tishio kwenye maeneo ya jiji hilo.
Vibaka hao ambao wamekuwa adha kubwa kwenye jiji hilo tarai wamesharipotiwa kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Relini Kata ya Central Jijini Tanga, Abdallah Mtige na kuzua hofu kwa wananchi.
Meya huyo alitoa ombi hilo juzi wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani ambapo alisema wapo baadhi ya viongozi wanafanya mazoezi mazoezi ya kukimbia asubuhi sana kuanzia saa 10 na saa 11 alfajiri hivyo huenda wanaweza kudhurika kwa kutekwa kutokana na kutokuwa na ulinzi.
Alisema kutokana na uwepo wa mazingira ya wimbi la vibaka anaweza kuwa anafanya mazoezi na akapata tatizo kutokana na uwepo wakati huo baki giza linakuwa halijatoka hivyo anaomba kama anaweza kupewa ulinzi.
“Mimi nafanya mazoezi usiku saa kumi na moja, nafanya mazoezi ya kukimbia hivyo ninaomba ulinzi wakati wa kukimbia vinginevyo ninaweza kutekwa kwani vibaka hawa hawachagui nani wa kumvamia. Kila wanayokutana naye wanakula naye sahani moja…DC najipenda nami hivyo naombeni ulinzi,” alisema.
Alisema anaomba ulinzi wa askari awe nao ndani ya gari kama ilivyokuwa kwa mameya wengine kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini ili kumuepusha kuondokana na kadhia ya kukumbana na vitendo vya uhalifu.
Akionyesha kuunga mkono hoja hiyo, Mbunge wa Jimbo la Tanga (CUF) Alhaji Mussa Mbaruku alisema kwamba hali ya jiji hilo sio shwari kwa kuwa kumekuwa na vimbi la vijana ambao wanajiita ‘Ibilisi’ wamekuwa wakifanya matukio ya kutisha kwa wananchi.
Alisema vijana hao ambao mpaka sasa wamekwisha kujeruhi zaidi ya watu 10 wanatembea kwa vikundi zaidi ya watu 50 wakiwa na silaha mbalimbali yakiwemo Mapanga, Marungu, Misumeno, Mikuki na Nyundo.
Hata hivyo alisema kwamba ni muhimu wananchi kushirikiana kuwafichua wahalifu waliopo kwenye maeneo yao ili kuweza kukomesha vitendo vya namna hiyo ambavyo visipozibitiwa zinaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii.