Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Anthony Komu, (Moshi Vijijini) na Saed Kubenea (Ubungo), wameingia kwenye vita ya maneno baada ya Meya huyo kudai wabunge hao wanataka kumpoteza.
Sakata hilo limechagizwa baada ya kusambaa kwa ujumbe wa sauti (voice note) zinazodaiwa kuwa za wabunge hao kuanzia jana Jumamosi Oktoba 13, iliyoambatana na ujumbe wa Jacob, akidai wabunge hao wanapanga kumpoteza hadi kuomba msaada wa serikali ili kumuumiza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye wabunge hao wanataka aangushwe lakini Bony amekuwa mwiba katika mpango wao huo.
Katika sauti hizo, wabunge hao wanasikika wakizungumza namna Meya huyo alivyo na nguvu na msaada mkubwa kwa Mbowe, kiasi kwamba ukimuondoa yeye utakuwa umemuumiza Mbowe. Hata hivyo, wabunge hao kwa nyakati wamekana sauti hizo si zao, ambapo Kubenea akidai ni mpango wa watu ambao inaonekana wako kazini kuendeleza mchezo wao kuchafua watu na anaamini imekuja wakati huu kwa sababu ya uchaguzi.
“Ni kwa sababu kuna uchaguzi ndani ya chama na watu wanajipanga kwa ajili ya 2020 na kuna makundi, kwa hiyo watu wanahitaji ubunge, urais, uongozi kwenye chama, sisi tunaamini ni makundi tu ndani ya chama,” amesema Kubenea.
Kwa upande wake Komu, amesema sauti inayosikika si yake, ni sauti zilizochezewa na watu ambao hajui nini malengo yao lakini amepuuza na hatajibu kwenye mitandao kwani si tabia yake.
“Bony mimi natoka naye wapi? Yaani Bony ni kijana mdogo sana, yeye ni Meya wa Ubungo na mimi Mbunge wa Moshi Vijijini, nakutana naye wapi? Yaani tuna maslahi gani tunayopigania mimi na Bony, sina nia na jimbo lake sijui udiwani wake au umeya wake.
Akizungumzia suala hilo, Meya Jacob amesema amesikia sauti hizo na tayari amechukua hatua kwa kukitaarifu chama na mamlaka nyingine husika.