25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MEYA ARUSHA AIBUA MAPYA FEDHA ZA RAMBIRAMBI

MEYA wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro (Chadema), amesema Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent waliofariki dunia kwa ajali, wakubali sehemu ya rambirambi zao zikarabati Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

 

 

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

MEYA wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro (Chadema), amesema Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent waliofariki dunia kwa ajali, wakubali sehemu ya rambirambi zao zikarabati Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika ofisi za Chadema Kanda ya Kaskazini alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiwa kwa dhamana yeye na viongozi wengine 12, wakiwamo wa Shirikisho la Wenye Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco) walioshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa siku mbili baada ya kukamatwa walipokwenda kutoa rambirambi kwa wazazi na walezi hao.

Wengine waliokamatwa ni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Ephraim Jackson, Diwani wa Olasiti, Alex Martin, Katibu wa Mbunge wa Arusha Mjini, Innocent Kisanyaga, Katibu wa wa Tamongsco Kanda ya Kaskazini, Leonard Mao na viongozi wengine wa dini.

Lazaro alidai kuwa Gambo aliwaita wazazi na walezi hao wiki iliyopita katika Hoteli ya Mount Meru kwa chakula cha mchana na kuwaeleza kuwa kiasi cha Sh milioni 56 zilizotolewa na wadau mbalimbali kwa familia hizo zitumike kukarabati hospitali hiyo.

“Cha kunisikitisha zaidi ameita wafiwa Mount Meru Hotel, amewapeleka ‘lunch’, ananikamata mimi kukutana na wafiwa kwenye shule ya wanafunzi waliopata ajali kwa ajili ya kuwapa mkono wa pole, yeye amewaita Mount Meru Hotel, amewasumbua wafiwa kutoka kwenye kata zetu, kwanini yeye asikamatwe?

“Halafu anawaambia eti fedha zilizobaki, shilingi milioni 56, zikakarabati Hospitali ya Mount Meru, ni lini rambirambi zinaenda kutekeleza Ilani ya CCM? Nataka nihoji Rais Dk. John Magufuli, mimi ni Meya wa Jiji, natekeleza shughuli za jamii hapa, Serikali imesema inaleta fedha kwenye miradi, ni kwa nini Mkuu wa Mkoa anashinikiza fedha za rambirambi zilizobaki zikakarabati hospitali?

 “Eti fedha hizo zikatekeleze ilani ya CCM, ilani ya CCM inatekelezwa kwa fedha za rambirambi? Haya tusipofiwa, kusipokuwa na maafa hiyo ilani itatekelezwaje? Hiyo hospitali tutakarabati kwa namna gani kama hakutatokea maafa?” alihoji.

Pia alidai kuwa Gambo amepeleka kiasi kingine kwa familia ya watu walioangukiwa na mti hivi karibuni huku fedha hizo zikiwa hazijatolewa kwa shughuli hiyo.

Alidai kuwa Gambo amepeleka Sh milioni 1.5 katika Kata ya Sambasha kwa familia tatu ambazo maharusi wake walifariki Februari, mwaka huu baada ya kusombwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha na kuhoji rambirambi hiyo isingekuwapo angepeleka fedha kutoka wapi.

“Hizo fedha alipeleka kwenye familia tatu wakati walifiwa familia tano, hiyo fedha alimpa mkuu wa wilaya na alitangaza, ndiyo maana hizi taasisi wakaona kwa vile mkuu wa mkoa hana utaratibu unaoeleweka ambao uko wazi, wakaona waende moja kwa moja kwa wahusika, namna ya kuwapata wahusika ni sisi viongozi wa maeneo husika.

“Kwa hiyo niseme mkuu wa mkoa akitaka kuongoza vizuri, awe na utaratibu unaoeleweka. Huu uongozi wa ubinafsi kwenye mkoa na Jiji la Arusha sisi hatutakubali, wenyeviti wa halmashauri za mkoa huu na ma- DC wetu na wakurugenzi hatutakubaliana na mkuu wa mkoa anayefanya biashara binafsi, shughuli za umma anafanya binafsi, hatuwezi kuwa na ‘one man show leadership or business’,” alisema.

Pia alisema kuwa Gambo ameletwa kuongoza mkoa huo, hivyo anapaswa kumshirikisha yeye, wabunge, wenyeviti wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wakurugenzi katika shughuli za kijamii.

 “Maafa haya yametokea, Gambo anasimamia msiba mwenyewe, wakati tukio lilipotokea hakuwepo ila viongozi wengine wa ngazi za wilaya na mkoa walilishughulikia, haiwezekani anataka fedha za jiji zitumike kwenye gharama za mazishi, lakini kwenye shughuli hiyo hataki viongozi tushiriki.

“Hatuwezi kuwa na uongozi wa aina hii na nimweleze tu Magufuli, tuna nia njema na nchi hii, sisi ni viongozi tuliochaguliwa na wananchi, lakini ajue kwamba kuna tatizo, kiongozi wake aliyemleta kwenye mkoa huu ni mbinafsi na mimi siwezi kufanya kazi na kiongozi ambaye ni mbinafsi, kazi za wananchi zinatakiwa zifanyike kwa uwazi,” alisema.

Alisema Gambo atakuwa kiongozi wa kuonyesha mfano, uwazi kwenye uongozi wake na jamii kwa ujumla, iwapo kuna mtu au taasisi inataka kutoa rambirambi ataielekeza kwenye familia husika kwa sababu tangu mwanzo hakuwa wazi.

Alidai kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro, hajui kinachoendelea katika suala la rambirambi.

“Hajui namna zinavyogawanywa, angekuwa kiongozi anayeelewa ushirikishwaji kwa wenzake, jambo hili angeshirikisha wakuu wa mikoa ya Manyara na Kilimanjaro.

 “Angesema meya ni mpinzani, mbunge ni mpinzani sawa tungekaa mbali, awashirikishe basi hawa CCM wenzake, Joel Bendera sio Chadema, kwa nini anawatenga wenzake na wamechaguliwa na rais? Huyu ni kiongozi msiri, hili ameshughulika nalo mwenyewe.

 “Na nasema atalibeba mwenyewe na nitaendelea kufuatilia fedha zilizopelekwa kwa wafiwa ili wapate kwa usahihi bila udanganyifu na kwenye hili najua Magufuli ataniunga mkono na Gambo atabaki peke yake kwa sababu namjua rais hataki longolongo, kificho wala ubinafsi,” alisema.

Alimwomba Magufuli kutambua kuwa Arusha kuna tatizo linalosababishwa na Gambo aliyedai ni mbinafsi, hivyo hawezi kufanya kazi naye kwa sababu kazi za wananchi zinatakiwa zifanyike kwa uwazi.

“Niseme kwa mara ya kwanza rais ajue Arusha kuna shida, hatuwezi kuwa na kiongozi ambaye hajielewi, mimi ni meya, natimiza wajibu wangu kama kiongozi wa jamii, nakamatwaje kwa amri yake?

 “Kwenye tukio hili niseme nawasifu Jeshi la Polisi wameliweka wazi, nimetoka leo (jana), nimeangalia magazeti na taarifa za polisi, wamesema wao wamepewa agizo na RC, kwa hiyo tulikuwa ndani kwa agizo lake akitaka tumpelekee yeye rambirambi ili yeye azipeleke.

 “Sasa msimamo wangu kama meya nasema rambirambi zitakazopitia ofisini kwangu zitaelekezwa kwangu sitazipokea nitawaelekeza wahusika kwa waliofiwa moja kwa moja sitampelekea yeye (Gambo), kwa sababu yeye hakufiwa na huu sio msiba wa ofisi yake,” alisema.

Alisema suala jingine linalomfanya asipeleke rambirambi kwa Gambo ni kuwa ni tofauti na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka jana mkoani Kagera, ambapo kamati ya kushughulikia maafa hayo iliwekwa wazi na akahoji iweje yeye hakuweka wazi kamati wala akaunti maalumu ya kupelekwa michango hiyo.

 “Hakuna utaratibu wa michango, hata ofisi yangu haina maelekezo yoyote kutoka ofisi ya Serikali inayosema fedha za rambirambi zinapelekwa wapi, hatuwezi kupokea maelekezo kwa mtu mmoja tu, yeye amekuwa nani apokee hela za watu agawe?” alihoji.

Akizungumzia kauli ya Gambo ya kuwataka viongozi kuacha kuingiza siasa katika msiba huo, alidai kuwa hakuna kiongozi aliyeingiza siasa katika msiba huo kama Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu na yeye hajawahi kufanya siasa kupitia msiba huo.

 “Mimi sifanyi siasa, nashukuru kwamba anajiweka wazi, kama kuna mtu amechukulia hili jambo kisiasa ni Gambo na Nyalandu na mliona kuanzia siku miili inaagwa uwanjani alishindwa kunitambua, alikuwa anafanya siasa, hata shughuli hii anavyoiendesha aliiendesha peke yake, kama angekuwa hafanyi siasa angetushirikisha, alizichukua familia na magari ya Serikali kuwapeleka Hoteli ya Mount Meru,” alisema.

Pia alisema leo kutakuwa na ibada maalumu ya kuwaombea majeruhi na waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea Mei 6, mwaka huu katika eneo la Marera, Rotia, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha na wafiwa kutoa shukrani katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Olasiti na itaongozwa na Askofu Dk. Solomon Masangwa.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Gambo kupitia simu yake ya mkononi ili kutoa ufafanuzi wa madai yaliyotolewa na Lazaro lakini hakupatikana hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno.

SABABU YA KUKAMATWA

Kuhusu kukamatwa, meya huyo alisema hadi wanaachiwa hajui kosa lililosababisha wakamatwe na kuwekwa ndani kwa siku hizo mbili.

Alisema suala la rambirambi ni kwenda kutoa mkono wa pole na kuwafariji wafiwa na si kugawa fedha, bali ni ibada ndiyo maana kulikuwa na viongozi wa dini.

“Hadi sasa ninavyoongea sijui kosa na itakuwa ni mara ya kwanza Tanzania inaenda kuweka rekodi ya kutoa rambirambi, tumekuwa tukitoa rambirambi kwenye kata zetu na misiba mingine kwa nini hii iwe nongwa, sijui kesi yangu ni ipi labda nitakaporudi Jumatatu nitaambiwa ila mimi ni Mkristo najua maana ya rambirambi, siwezi kuwaambia watu watume rambirambi kwa njia ya simu, lini rambirambi inatumwa kwa simu.

“Nilichojiuliza ni maswali tuliyokuwa tunahojiwa, kwamba kwa nini fedha hizo hazijapitishwa kwa Gambo, kwangu mimi ni jambo ambalo limenisikitisha na Watanzania wajue hakuna kiongozi wa Serikali aliyefariki, walifiwa wananchi wa kata zetu, nimefiwa na wananchi wangu, rambirambi za wananchi zinatakiwa zipelekwe kwa waliofiwa na ndiyo maana siku nne zilizopita nilimtaka Gambo aje hadharani awape rambirambi waliofiwa na alitekeleza.

“Sasa kama yeye alikusanya rambirambi akapeleka kwa nini anazuia mimi kupeleka? Tena siyo mimi napeleka, wanapeleka wadau, mimi kazi yangu ni kuratibu  kuhakikisha waliofiwa wanapatikana,” alisema.

KAULI YA POLISI

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo, ameliambia MTANZANIA Jumapili kuwa viongozi hao wameachiwa kwa dhamana na kesho wanatakiwa kuripoti polisi.

 “Tuhuma ni zilezile za juzi, huwezi kuzuia watu kufikiri wanavyotaka, hao wameambiwa tuhuma zao na wameachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti Jumatatu,” alisema.

Juzi alisema walipata maelekezo kutoka kwa Gambo kuwa kuna mkusanyiko, hivyo wao kama polisi wakaenda kuwakamata na kuwahoji na kuhusu kukamatwa kwa waandishi wa habari 10 waliokuwa wakifuatilia tukio hilo, alisema walichukuliwa kimakosa ndiyo maana waliachiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles