MEYA AITAKA JAMII KUSAIDIA WENYE MAHITAJI

0
669

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam,  Isaya Mwita ameishauri jamii kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia watoto wenye ulemavu kupata elimu ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Akizungumza kwenye mahafali ya 45 ya darasa la saba ya Shule ya Walemavu ya Jeshi la Wokovu, iliyopo jijini Dar es Salaam juzi, Mwita alisema kwa sasa watu wenye ulemavu wanaonekana hawafai na hawapati nafasi katika jamii.

“Ninashauri jitihada mahususi zitumike kuwatambua watu hao na kuhakikisha wanapata elimu na kutambuliwa na jamii,” alisema Mwita.

Alisema katika sekta ya elimu, taasisi mbalimbali na mashirikia ya dini  yako mstari wa mbele kutoa nafasi za elimu kwa makundi hayo lakini jamii imekuwa kama haiwaoni.

“Nitoa wito kwa jamii nyingine kujitoa kwa hali na mali kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu ili waweze kujisikia ni sehemu ya jamii,” alisema Mwita.

Alisema kazi inayofanywa na Jeshi la Wokovu kuwapatia elimu kundi hilo ilitakiwa ifanywe na serikali lakini kwa nafasi yao wameweza.

“Niwapongeze Jeshi la Wokovu kwa kuifanya kazi hii kwa niaba ya serikali na nitumie nafasi hii kuwaalika viongozi wa serikali, mashirika mbalimbali kujitoa ili kusaidia shule hii ambayo imeonyesha nia dhabiti ya kusaidia watoto hawa,” alisema Meya Mwita.

Meya Mwita aliwataka wazazi waliokuwa na watoto wao shuleni hapo kuwa mabalozi kwa wazazi wengine na kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu kama wengine.

“Niwapongeze wazazi wenye watoto wenu hapa, mmeonyesha uthubutu mkubwa, hizi siyo dhama za kuficha watoto, waambieni na wengine wasiwafiche waleteni wapate elimu ili iwasaidie baadaye, hawa ndiyo watakuja kuwa viongozi wa baadaye,” alisema Meya Mwita.

Awali akisoma risala, mkurugenzi wa shule hiyo, Luteni Thomas Sinana alisema ina jumla ya wanafunzi 210 wenye ulemavu na ikikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni upungufu wa vitabu, huku wanafunzi wengine wakishindwa kufika shuleni baada ya likizo kwa kukosa fedha za kuwasafirisha.

Alisema shule hiyo inachukua wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini hivyo wakati mwingine huwawia vigumu wanafunzi hao kurudi shuleni kutokana na ukosefu wa fedha na aliiomba serikali kusaidia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here