MERRY CHRISTMAS SIMBA

0
826

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

SIMBA imetoa zawadi ‘bab kubwa’ ya Sikukuu ya Krismasi kwa wanachama na mashabiki wake kwa kuifunga Lipuli ya Iringa mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini hapa jana.

Ushindi huo, umeiwezesha Simba kuziki kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 28 baada ya kushuka dimbani mara 11, huku Lipuli wakibaki katika nafasi ya nane wakiwa na pointi zao 18 walizovuna ndani ya michezo 13.

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Francis Kahata ndiye aliyeanza kuifungia timu hiyo bao, kabla ya Meddie Kagere kuongeza lingine na Hassan Dilunga ‘HD’ kupiga mawili safii.

Ushindi wa jana wa Simba ni salamu tosha kwa Yanga walioambulia suluhu dhidi ya Mbeya City Jumanne ya wiki hii kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuelekea pambano lao na watani wao wa jadi, Simba linalotarajiwa kupigwa Januari 4, mwakani.

Simba ndio waliouanza mchezo huo kwa kasi na iliwachukua dakika tisa tu kulitikisa lango la Lipuli kwa shambulizi matata lililoishia kwa Kagere kushindwa kucheka na nyavu, akiwa ndani ya 18, ikiwa ni kutokana na pasi ya Clatous Chama.

Dakika moja baadaye, Kahata aliiandikia Simba bao la kwanza kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 akipokea pasi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe.

Chama alikaribia kuifungia Simba bao la pili dakika ya 19, akiwa ndani ya 18, akibaki yeye na kipa na kupiga shuti lililookolewa na mabeki wa Lipuli.

Lipuli ilijibu mapigo dakika ya 23 pale mshambuliaji wao, Mwinyi Ahmed alipopiga shuti la mbali, lakini mpira ukatua mikononi mwa kipa wa Simba, Beno Kakolanya.

Dakika ya 35, mchezaji wa Lipuli, Steven Mgau, alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Dilunga.

Mshambuliaji wa Lipuli, Paul Nonga alimtia majaribuni Kakolanya kwa kupiga shuti kali ambalo kipa huyo aliliona. 

Simba walikianza kipindi cha pili kwa kasi, wakifanya mashambulizi ya nguvu yaliyozaa bao la pili dakika ya 49 kupitia kwa Kagere aliyetikisa nyavu baada ya kuwatoka mabeki wa Lipuli na kuachia shuti lililojaa nyavuni, hiyo ikiwa ni pasi ya Chama.

Dilunga aliifungia Simba bao la tatu dakika ya 54 kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya beki wa Lipuli, Norvat Lufunga kumvuta Chama ndani ya 18 na mwamuzi, Martin Sanya kumwonyesha kadi ya njano.

Dakika ya 64, Dilunga aliiandikia Simba bao la nne baada ya kuambaa na mpira kutoka katikati ya uwanja na kuwapita mabeki wa Lipul hadi eneo hatari na kuachia shuti kali lililojaa nyavuni, akiwa amepokea pasi ya Shiboub.

Kenneth Masumbuko wa Lipuli nusura afunge bao dakika ya 77 baada ya kupiga kiufundi mpira wa adhabu lakini ulitoka nje kidogo ya goli la Simba.

SIMBA: Beno Kalolanya, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Tairone Santos, Pascal Wawa/Kennedy Juma (dk73), Jonas Mkude/mzamiru Yassin (dk58), Hassan Dilunga, Sharaf Shiboub, Medie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata/Deo Kanda (dk58).

LIPULI: Agathony Mkwando, David Kameta, Emmanuel Kichiba, David Majige, Norvat Lufunga, Fredy Tangalo, Mwinyi Ahmed/Shaaban Ada (dk65), Steven Mgayu, Paul Nonga, Daruesh Saliboko/Issa Ngoah (dk83) na Kenneth Masumbuko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here