BRIGHITER MASAKI, DAR ES SALAAM.
MSANII wa muziki na filamu nchini, Menina Abdulkarim, juzi aliitikia wito alioitwa tangu Oktoba 11 katika Ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam na kutoa maelezo juu ya kusambaa kwa video na picha zake za utupu kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumza na MTANZANIA, jana Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Godfrey Mngereza amesema Menina amelipoti ofisini hapo na watatoa taarifa rasmi hatua iliyochukuliwa.
“Mara kadhaa BASATA kupitia utaratibu wake wa kutoa Elimu kwa wasanii imekuwa ikiwaelekeza wasanii wote nchini kufanya kazi zao za Sanaa kwa kuzingatia maadili mema kwa jamii pamoja na kufuata taratibu za kujisajili, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya wasanii wamekuwa hawazingatii maelekezo hayo na hivyo kujikuta wanavunja sheria za nchi.
“Kupitia mahojiano kati ya msanii na BASATA kwa pamoja wamesikiliza maelezo ya Menina Abdulkarim na nini kilichojitokeza katika sakata zima la kusambaa kwa video na picha zake za utupu kupitia mitandao ya kijamii, hivyo taarifa itatolewa juu ya hatua iliyochukuliwa,” alisema Mngereza.