25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mengine yaibuka kuondolewa Meya Ubungo

Mwandishi Wetu -Dar es salaam

IMEBAINIKA kuwa suala la kuondolewa madarakani  Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (Chadema), lilikuwa limepangwa muda mrefu na baadhi ya wanachama wenzake baada ya kile kilichodaiwa kuvuruga kikao cha Kamati ya Utendaji ya Jimbo la Ubungo  kilichofanyika Mabibo jijini Dar es Salaam Aprili 3, mwaka huu.

Pamoja na hali hiyo pia inadaiwa kuwa Jacob alikuwa kwenye harakati za kuanza kukusanya fedha kwa wafanyabiashara kwa ajili ya kujiandaa katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge katika Jimbo la Ubungo, jambo ambalo amesema kuwa si kweli na wala si dhambi kuomba michango.

Chanzo  kutoka ndani ya Chadema, kilieleza kwamba kutokana na hali hiyo hatua ya kuvurugwa kwa kikao hicho iliibua mkakati wa kuanza kushughulikiwa kwa Jacob hadi kufikia kuvuliwa uanachama jambo ambalo yeye pamoja na uongozi wa chama hicho cha upinzani wanapinga hatua hiyo.

 “Huyu jamaa alikuwa ana mambo mengi, mojawapo ni hili la kukusanya fedha kwa wafanyabiashara kwa faida zake binafsi, kwa ajili ya kuzitumia katika uchaguzi mkuu ujao. Lakini jambo la kusikitisha Jacob wakati wote akiwa meya alikuwa anasema kwamba Ubungo hakuna matatizo lakini leo imekuaje baada ya kuondoka ndiyo anaibuka na madai ya ubadhirifu,” kilisema chanzo hicho.

Kutokana na madai hayo MTANZANIA ilimtafuta Jacob, ambapo alisema kuwa taarifa hizo hazina ukweli lakini hata kama ikiwa hivyo, atakuwa hajafanya kosa lolote kisheria.

“Hawa jamaa ni kama wanatapatapa, japokuwa si kweli lakini ni kwamba hata kama ningefanya hivyo ningekuwa nimekiuka sheria? Mbona suala la watu kuchangisha fedha kwa ajili ya uchaguzi ni la kawaida sana na wote hata hao viongozi wengine wanafanya?

“Kimsingi ni kwamba walikuwa wanatakiwa angalau watafute sababu zenye mashiko siyo hizo sababu nyepesi nyepesi ambazo kabisa unaona hazina uzito,” alisema.

Jacob ambaye amekuwa meya wa Ubungo kwa kipindi kimoja na diwani wa Kata ya Ubungo kwa vipindi viwili, hivi karibuni alitangaza nia yake ya kutowania tena udiwani na kwamba anatarajia kuwania ubunge katika Jimbo la Ubungo kwa kile alichoeleza kuwa ni kutokana na maoni ya wananchi ambao waliandamana kumpelekea ombi hilo.

Kuhusu suala la kuvuruga kikao cha Kamati ya Utendaji Jimbo la Ubungo kilichoketi Aprili 3, mwaka huu katika Kata ya Mabibo kwa kutumia mabaunsa, Jacob alisema kuwa si kweli kwani huenda watu wanafanya jitihada za kuendelea kumchafua.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika alisema chama hicho hakijamfukuza uanachama Diwani wa Ubungo ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob na wala hakijawahi kujadili suala lolote kuhusu yeye. 

Mnyika alitoa kauli siku moja baada ya kusambaa barua iliyodaiwa kuandikwa na mtu aliyejitambulisha kama Katibu Kata ya Ubungo, Asheri Mlagwa ambaye hata hivyo amekanusha kuhusiana na barua hiyo. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema alishamwandikia barua Mkurugenzi wa Maniapaa ya Ubungo, kumtaka afute barua yake aliyoandika na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii, ambayo inaonesha uongozi wa Chadema pia umepewa nakala japokuwa bado hawajakabidhiwa nakala hiyo. 

“Chama kinamtambua Jacob kama mwanachama, diwani na Meya wa Manispaa ya Ubungo. Pamoja na barua hii tumemtaka afute barua yake kwani utaratibu wa hatua za kinidhamu upo wazi kwa mujibu wa Katiba. 

Wiki iliyopita akizungumza na waandishi wa habari, Jacob alisema kuwa kwa sasa ameshaandika barua kwenda kwa Waziri wa Tamisemi akisubiri maamuzi yake ambapo kama hatakuwa ajaridhika ataeleza hatua zaidi atakazo chukua.

BARUA YA MKURUGENZI 

Katika barua iliyoonesha kuandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Aprili 2, 2020 yenye kumbukumbu KUMB:NA. CAB./74/216/01/07 kwenda kwa Mstahiki Meya, Boniface Jacob, ilimweleza kuhusu kupokea nakala ya barua hiyo ya kufukuzwa kwake uanachama. 

“Kutokana na barua hiyo kunitaarifu kuwa “Umefukuzwa Uanachama” kuanzia tarehe 28/04/2020, nachukua nafasi hii kukutaarifu rasmi kuwa umekoma kuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa mujibu wa kitungu cha 

39(2)(f) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa sura ya 292 toleo la Mwaka 2015 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 73(1)(e) na (f) ya kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo za Mwaka 2019. Sheria na kanuni hizo zinazofafanua kwamba “Mjumbe atapoteza sifa kuwa Mjumbe wa Halmashauri endapo atakoma kuwa mwanachama wa chama cha Siasa kilichompendekeza kuwa mgombea wa kiti cha udiwani. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles