24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Meneja Tanesco asiyetimiza lengo kuchukuliwa hatua

Mwandishi Wetu -Geita

WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema Mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) watakaoshindwa kutimiza malengo ya kuunganisha umeme vijijini na kuwawashia wananchi umeme watachukuliwa hatua kwa mujibu wa mikakati iliyowekwa katika kupima utendaji kazi wao.

Dk. Kalemani alisema hayo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea baadhi ya vijiji ambavyo vimepitiwa na vilivyojirani na miundombinu ya umeme ambavyo bado havijafikiwa na mradi wa usambazaji wa umeme vijijini REA katika Wilaya ya Nyang’hwale, Geita na Chato mkoani Geita.

Baada ya kukagua vijiji hivyo aliwaagiza mameneja wa Tanesco nchini kuunganisha umeme katika vijiji hivyo pamoja na kuwawashia wananchi umeme kwa gharama ya Sh 27,000 tu.

Dk. Kalemani aliweka wazi kuwa katika kutimiza azma na malengo ya serikali ya kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinapata umeme, mameneja wa Tanesco kote nchini waliwekewa vigezo vitatu vya kuwapima na kufanya tathmini ya utendaji kazi wao katika kutekeleza malengo hayo, zoezi hilo lilianza Julai, 2019, ambapo sasa utekelezaji wake unaanza kwa kuwachukulia hatua mameneja hao.

Vilevile mameneja walitakiwa kuunganisha umeme katika vijiji ambavyo vimepitiwa na njia ya kusafirisha umeme mkubwa ambavyo bado havijafikiwa na REA pamoja na vile vilivyo umbali mfupi kutoka katika maeneo yaliyopitiwa na njia za umeme.

“Tathmini zinazotumika kuwapima mameneja katika utendaji kazi wao, kuwa ni kuongeza idadi ya wateja katika maeneo yao na kuunganisha wateja hao kwa wakati mara tu baada ya mteja kulipia gharama za uunganishaji, tathmini hiyo inachukuwa asilimia 45ya utendaji kazi wake.

 “Kama unakataa wateja katika eneo lako, umeme unakatika mara kumi kwa mwezi, huwasikilizi wateja wala kutatua kero zao,hupokei simu za wateja wewe hutoshi na hufai kuwa maneja andika barua ujitoe mwenyewe, pia tunakutoa, mameneja wa kanda simamieni hili na muanze kuchukuwa hatua, na kama hamtachukuwa hatua tutaanza kuwatoa kuanzia chini mpaka juu,” alisema Dk. Kalemani

Aidha alifanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi Ndogo ya Tanesco Katoro na kumtaka meneja wa kituo hicho kuandika barua ya kujieleza, kutokana na baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo kutokuwepo kazini bila taarifa yoyote, na wengine kukutwa wakipiga soga bila kuwepo katika maeneo yao ya kazi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles