NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Meneja Ukaguzi shughuli za maabara Wizara ya Madini Donald Njonjo(30) na Mfanyabiashara wa Tandika Gamba Muyemba (51) kulipa fidia Sh milioni 300, baada kukiri kosa la kuuza madini bila kibali.
Washtakiwa hao, walitiwa hatiani na kuhukumiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina.
Mahakama iliamuru walipe Sh milioni 50 na zingine watamalizia ndani ya miezi 12 kuanzia Oktoba 23, mwaka huu.
Mahakama hiyo, iliamuru mali za mshtakiwa Donald ambazo ni Viwanja viwili ploti namba 51/1/bloc C kilichopo Njedengwa high Density Dodoma na kingine kilichopo eneo la Nzuguni B Dodoma pamoja na gari aina ya Nissan Hard Body lenye namba za usajili T 563 BUK vitaifishwe na kuwa mali za Serikali.
Mbali na adhabu hizo, mahakama ilitaifisha dhahabu feki yenye uzito wa kilogramu 2,794.5 na kukabidhiwa kwa Tume ya Madini
Mahakama hiyo, pia iliamuru kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh milioni 5 na iwapo watashindwa watatumikia kifungo cha miaka 3 jela.
Hakimu Mhina, alisema alitoa adhabu hizo baada ya kuzingatia hoja zilizotolewa na upande wa mashtaka na utetezi na kwamba kosa hilo halikufanyika kwa bahati mbaya kwa sababu waliiba na kuuza.
Pia aliangalia uhalisia wa ushauri hilo washtakiwa walikiri kosa na kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Jacqline Nyantori aliieleza mahakama kuwa hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma za washtakiwa hao hivyo ni wakosaji wa Mara ya kwanza.
Nyantori alidai kwa kuwa washtakiwa hao walikiri makosa yao na walikubali kuingia makubaliano na DPP, aliiomba mahakama wakati ikitoa adhabu yake izingatie makubaliano hayo.
Nyantori aliiomba mahakama iwaadhibu washtakiwa hao kwa sababu makosa yao yanadidimiza moja kwa moja uchumi wa nchi na wangefanya shughuli hiyo kihalali nchi ingepata mapato ambayo yangetumika katika shughuli muhimu za kijamii.
Kwa upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Jonas Nkya kwa nyakati tofauti, waliiomba mahakama itoe adhabu nafuu kwa Wateja wao kwa sababu walikiri kosa, wameomba msamaha na kujutia makosa yao.
Nkya alidai washtakiwa wakosaji wa Mara ya kwanza na wanafamilia zinazowategemea wakiwamo mke na Watoto.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, washtakiwa wanadaiwa kati ya Julai mosi na Novemba 30,mwaka jana ndani ya Jiji la Dar es Salaam, waliuza madini ya dhahabu kilogramu 6.244 yenye thamani ya Sh 507.3 milioni bila ya kuwa na kibali.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali Nyantori, alidai kilogramu 6.244 zilikamatwa eneo la feli ya Azam zikisafirishwa. Ambapo ilifunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi namba 67/2017 ambao washtakiwa kwenye kesi walikiri kosa na kuhukumiwa ambao mahakama ilizitaifisha na kuwa mali ya serikali.
Baada ya kutaifishwa dhahabu hizo zilikabidhiwa kwa Donald ambaye alikuwa mwajiliwa wa Wizara ya Madini ambaye alizihifadhi katika kasiki ambao mwaka 2018 aliwasiliana na Gamba wakaingia makubaliano ya kuiba hizo dhahabu kwa lengo la kujipatia faida, wakiiba na kuuza.
Baada ya kuiuza walitafuta mtu wakatengeneza dhahabu feki yenye umbo na uzito kama ule wa 6.244 ili waweze kuzirudisha zionekane kama zile halali, lakini hawakufanikiwa kwa sababu zilihitajika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mwisho