23.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Meneja maabara ya madini mbaroni kwa wizi dhahabu ya Sh milioni 507

Na Leonard Mang’oha-Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Meneja wa Maabara wa Tume ya Madini, Donald Njonjo (30), kwa tuhuma za kuiba dhahabu  kilo 6.244 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 507 iliyokuwa imehifadhiwa ofisi za Wakala wa Madini Masaki, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar  es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema Juni 29, mwaka huu walipata taarifa kutoka kwa Ofisa Madini Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Sadick baada ya kugundua kuibwa madini hayo.

Kamanda Mambosasa alisema baada ya kupata taarifa hizo, jeshi hilo lilianza uchunguzi mara moja na kubaini kuwa madini hayo yaliibwa na Njonjo na kuwa alianza kuyaiba tangu Desemba mwaka jana.

Alisema baada ya mtuhumiwa kuhojiwa, alikiri kuiba madini hayo kidogo kidogo kutoka katika ofisi za Tume ya Madini.

“Mtuhumiwa alieleza kuwa madini hayo aliyauza katika duka la kuuzia vito vya dhahabu na kisha kuhifadhi madini bandia yenye uzito wa kilo 6.001 nyuma ya jengo la Tume ya Madini ili kuyapeleka katika chumba walichoiba madini hayo halisi kuyabadilisha.

“Madini hayo halisi ya dhahabu yalikamatwa mwaka 2017 huko maeneo ya bandarini Zanzibar yakiwa yanasafirishwa kinyume cha sheria kisha kutaifishwa na Serikali na kuhifadhiwa katika ofisi za Tume ya Madini.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linakamilisha utaratibu wa kupeleka jalada kwa mwendesha mashtaka wa Serikali ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani,” alisema Kamanda Mambosasa.

Wakati huohuo, jeshi hilo linawashikilia watu saba kwa tuhuma za wizi wa bajaji maeneo ya Ukonga.

Kamanda Mambosasa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Salum (27), Amo Kefas (30), Said Ahmad (38), Mohamed Musa (31), Mboke Samwel (26), Abdallah Kipaneli (25) na Mfaume Mussa (25).

Alisema Julai 9 mwaka huu saa 8:00 usiku huko maeneo ya Kibeberu na Magole  Ukonga, watuhumiwa hao wanadaiwa walivunja maduka matatu na kuiba fedha pamoja na bidhaa mbalimbali zikiwamo bajaji mbili zenye namba za usajili MC 312 CFB na MC 540 CED zote aina ya TVS zikiwa na rangi ya bluu.

“Baada ya wizi huo, taarifa zilipokewa katika Kituo cha Polisi Stakishari na upelelezi ulianza mara moja ambapo Julai 9, 2019 saa tano asubuhi watuhumiwa walikamatwa huko maeneo ya Hondogo Gogoni Kiluvya, Wilaya ya Ubungo.

“Aidha watuhumiwa hawa wamekuwa wakifanya matukio ya uhalifu kwa kutumia gari aina ya Toyota Harrier nyeusi yenye namba T 666 DJG ambayo inashikiliwa na Jeshi la Polisi ili kubaini mmiliki wake,” alisema Kamanda Mambosasa.

Alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles