25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Membe pasua kichwa

Ramadhan Hassan – Dodoma

WAZIRI wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe jana alifika mbele ya Kamati ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma na kuhojiwa kwa saa tano.

Membe aliyepata kugombea urais ndani ya chama hicho na kuingia tano bora katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alifika ofisi ya makao makuu ya CCM jana saa 3:10 asubuhi na kutoka saa 8:43 mchana.

Desemba 13 mwaka jana, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliketi na kuagiza makada watatu wa chama hicho waitwe na kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho baada ya kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali.

Makada hao mbali na Membe, ni makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho tawala, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba ambao nao watahojiwa.

Jana, akiwa ndani ya gari lake aina ya Range Rover Vogue baada ya kuhojiwa, Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa safari yake ya kuhojiwa na kamati hiyo ya maadili ilikuwa na manufaa makubwa kwake, kwa CCM na kwa taifa.

Mbunge huyo wa zamani wa Mtama, alisema amekuwa mtu mwenye furaha mara baada ya kuhojiwa, na anakwenda kula chakula kizuri yeye na mke wake hoteli ambayo haijulikani na kwamba mengine yatakuwa yakipatikana kidogo kidogo mara baada ya kushiba.

“Lakini niwaambie safari hii ya kuja Dodoma ilikuwa ni ya manufaa makubwa sana sana sana kwangu, kwa chama na kwa taifa letu, mengine yatakuwa yanapatikana kidogo kidogo nikishiba.

“Kwa hiyo sasa hivi mimi na mke wangu tunaenda kula chakula kitamu sana kwenye hoteli moja ambayo haijulikani, ‘and then’ baada ya hapo nitaanza safari ya kwenda Dar es Salaam,” alisema Membe.

Vilevile alisema amekuwa ni mtu mwenye furaha kwa sababu amepata nafasi ya kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa na pia amepata nafasi ya kufafanua mambo pamoja na kutoa mawazo yake.

“Nasema hivi, tulikuwa na mkutano wa masaa matano ya mijadala mizuri mikubwa ya kitaifa inayohusu chama chetu CCM, inayohusu nchi yetu na nimekuwa mtu wa furaha kubwa ajabu, kwa sababu nimepata nafasi nzuri ya kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa.

“Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu walitaka kuyajua, nimepata nafasi nzuri ya kutoa mawazo ya yale mambo ambayo niliombwa kutoa mawazo,” alisema Membe.

ALIVYOWASILI

Membe aliwasili Makao Makuu ya CCM maarufu White House majira ya saa 3.10 asubuhi akiwa kwenye gari aina ya Range Rover Vogue lenye namba za usajili T 748 CNV, akiwa amevaa shati la kijani lenye mchanganyiko na rangi nyeusi pamoja na suruali nyeusi huku akiwa ameongozana na mke wake.

Mara baada ya kuingia getini, alipokewa na watumishi watano wa CCM katika lango kuu la kuingia kwenye ukumbi wa White House zilipo ofisi za viongozi wa CCM na ukumbi wa mikutano ndani ya jengo hilo.

HALI YA ULINZI

MTANZANIA iliyoweka kambi Ofisi za Makao Makuu ya CCM jijini hapa, licha ya kwamba kulikuwa kuna mvua, ilishuhudia ulinzi wa hali ya juu, huku askari wawili wa Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT pamoja na wa vyombo vya dola walikuwa na jukumu la kuratibu hali ya usalama eneo hilo.

Walinzi wa Suma JKT wao walikuwa na kibarua cha kufungua na kufunga geti la lango kuu sambamba na kuhoji kila aliyesogea eneo hilo na kumkagua.

Kwa siku ya jana hali hiyo kwenye lango kuu la ofisi hizo za chama tawala ilikuwa tofauti na siku nyingine.

Kila aliyeenda aliulizwa anataka nini huku waandishi wa habari walizuiwa na askari hao kuingia ndani kwa madai hawajapewa maelekezo kwamba wanahitajika katika eneo hilo.

Pamoja na kukatazwa huko mwandishi wa gazeti hili alikaa jirani na eneo hilo kushuhudia jinsi ambavyo anaingia na kutoka waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje.

Pia katika geti la kuingilia kuliwekwa kibao cha ‘No Parking’ kikiashiria kwamba magari hayatakiwi pia kuegeshwa jirani na makao makuu hayo ya CCM.  

KAULI YA MEMBE KABLA KIKAO

Juzi jioni akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam, Membe alisema anaamini kikao hicho kitakuwa kizuri na angetamani waandishi wa habari wawepo ili kuwe na uwazi.

Alipoulizwa na mtangazaji wa kituo hicho aliyekuwa akimhoji kama atakuwa tayari kwa uamuzi wowote, Membe alijibu kwa ufupi; “Itategemea.”

Kuhusu jopo litakalomfanyia mahojiano, alisema kikao hicho kitaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na kwamba mahojiano hayo yatakuwa mazuri yenye uwazi.

“Ninawaambia Watanzania, kesho (jana) ni siku muhimu sana kwangu, nilikuwa ninaisubiri sana kukutana na hii kamati na ninamwomba Mungu anijaalie niwepo katika kamati kwa sababu nitapata nafasi ya kuzungumza na wanakamati mambo wasiyoyajua na wanayoyajua.

“Kwa hiyo kesho (jana) saa tatu asubuhi nisikosekane kwenda, niko sasa safarini kwenda Dodoma ili kesho (jana) tukazungumze.

“Kamati itasikiliza hoja na watatoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo itaamua kutoa uamuzi wowote, nadhani uamuzi utatoka mwishoni mwa mwezi huu Februari au Machi,” alisema Membe.

Mapema wiki hii, Membe aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter: “Hatimaye, nimepokea barua ya kuitwa kwenye kikao cha Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu jijini Dodoma.

“Kikao kitafanyika Februari 6, 2020 saa 3 asubuhi kwenye jengo la White House. Nitahudhuria bila kukosa na bila kuchelewa! Stay tuned!”

KAULI YA MANGULA

Jana, gazeti moja la kila siku, lilimnukuu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Mangula akisema wanaanza kuwahoji makada hao mmoja baada ya mwingine na baada ya kuhitimisha hilo, vikao vya chama vitapitia maelezo na kutoa uamuzi.

Mangula alisema wamepanga kukamilisha kazi ya kuwahoji viongozi hao wiki hii na atakayeanza kuhojiwa ni Membe.

“Tumepanga kuwahoji kwa siku moja kila mmoja, lakini utaratibu unaweza kubadilika kulingana na maelezo atakayotoa mhusika. Kama tutaona siku moja haitoshi, atarejea tena siku itakayofuata,” alisema Mangula.

Mangula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili ya chama hicho, alisema wahusika wote wameshapewa taarifa ya kufika makao makuu ya CCM jijini Dodoma kuhojiwa.

Alisema vikao hivyo vya kuwahoji vitaongozwa na Katiba ya CCM na Kanuni za Maadili ya Viongozi.

Makada hao wanatuhumiwa kukiuka maadili ya viongozi wa CCM kwa kushiriki kuandaa waraka wa siri dhidi ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Waliibua mjadala baada ya sauti zao kusikika mitandaoni wakizungumzia mpasuko ndani ya CCM.

Wakati vigogo hao wakitakiwa kuhojiwa, Halmashauri Kuu ya CCM iliwasamehe na kuwaonya wabunge wake watatu, January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama) ambao kwa nyakati tofauti walimwomba msamaha Rais Magufuli.

Kinana na Makamba walikuwa wamewasilisha malalamiko yao CCM, Julai 14 mwaka jana wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu ambaye amekuwa akiwadhalilisha na ambaye walimwelezea kuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Makamba na Kinana waliokuwa watendaji wakuu wa chama hicho tawala katika awamu ya nne, walitumia Katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122 kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalizua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Sauti za makada hao zilianza kusambaa mitandaoni baada ya waraka huo wa Makamba na Kinana walioupeleka kwa Katibu wa Baraza la Ushauri wa Viongozi wa CCM, Pius Msekwa kuwa umesambazwa kwenye vyombo vya habari.

KANUNI ZA UONGOZI

Kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la 2017, zimebainisha adhabu tatu kwa wanachama wanaofika mbele ya kamati hiyo na kutiwa hatiani.

Katika kanuni hizo kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika Katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha wataondolewa katika chama au uongozi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,530FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles