30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Membe azindua kampeni Lindi kwa ahadi ya neema

 FARAJA MASINDE NA HADIJA OMAR -DAR/LINDI

CHAMA cha ACT Wazalendo kimezindua rasmi kampeni zake mjini Lindi huku kikianisha vipaumbele vyake vinne.

Kampeni hizo zilizinduliwa jana katika Uwanja wa Mpilipili na Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya urais upande wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akitaja vipaumbele hivyo, mgombea urais kupitia chama hicho, Bernard Membe alisema atahakikisha kuwa anaziba mapengo yaliyomfanya aamue kuwania nafasi hiyo, ikiwemo miundombinu ambapo kitaimarisha barabara hususani za mikoa ya Kusini. 

“Jambo la kwaza ni barabara mbovu tena barabara moja, wenzetu wana barabara nyingi, hapa inapita tu kutoka Dar es Salaam.

“Hivyo ACT Wazalendo ikiingia madarakani itajenga barabara hizi, tumechoka kutembea na mavumbi kana kwamba tunatoka shambani kila kukicha. 

“Pia tunataka wakulima wetu wauze mazao yao kokote kule wanakotaka, sisi tunataka mkulima auze kama ni korosho zake anapewa fedha yake.

“Uchumi duniani unakwenda na watu wa kati, limeni korosho zenu, ufuta wenu, mbaazi zenu nitazisimamia mwenyewe uza kokote, cha msingi utoe kodi,” alisema Membe.

Akizungumzia suala la afya, alisema kwenye Serikali yake atalipa bima kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanapewa matibabu bora hususan wazee, wajawazito na watoto.

“Wajawazito na akina mama wanaojifungua, wazee na watoto wataona raha sababu bima ya afya itakuwa ndogo na watatibiwa bila gharama yoyote.

“Sisi ni nchi ya wakulima na wavuvi ambao ndio tunatakiwa kuangalia maendeleo yake, lakini hatuwaonei huruma wakulima na wavuvi ambao wanapata mlo mmoja tu kwa siku na tunamwambia ana hela nyingi,” alisema Membe.

Alisema Watanzania wasingepaswa kuwa mafukara na kwamba kuna watumishi ambao wanafanya kazi bila kupandishwa mshahara na madaraja na haki ya kulipwa likizo.

Membe alisema kipaumbele kingine ni cha kusimamia bei za mazao ambapo atahakikisha kuwa wakulima wanauza mazao yao kokote kule ikiwa ni pamoja na kuangalia kila mkoa zao lililopo na namna ya kuliboresha kwa ajili ya kuleta tija kwa wakulima.

“Tutaunda wizara ambayo kazi yake ya kwanza ni kwenda nje kwa ajili ya kutafuta masoko ya mazao yetu. “Ndugu zangu wa Lindi mkitaka tushinde tuondoe tu woga kwa kuichagua ACT Wazalendo,” alisema Membe.

Membe alisema ACT itaimarisha diplomasia ya kimataifa ambapo ataunda wizara itakayoimarisha urafiki wa Tanzania na nchi nyingine. 

Kwa upande wake, mgombea mwenza katika nafasi ya urais, Profesa Omar Faki alisema dhamira ya kuja kwenye mikutano ya kampeni ni kuielezea hali halisi ya Watanzania ambayo na wao wamo.

“ACT Wazalendo tumekuja kuwahakikishia kuwa tuna ilani inayotoa haki sawa, naamini kuwa mtaunga mkono juhudi hizi,” alisema Profesa Faki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Maalim Seif aliwaomba wanakusini hao kukipigia kura chama hicho ili wachague Serikali ambayo itajali maisha yao na masilahi yao. 

“Hakuna cha kufanya isipokuwa kumchagua Membe ili kuwa rais wa Tanzania ambaye atajali masilahi yenu. 

“ACT Wazalendo ndiyo chama kipya kuliko vyote, lakini kinakua kwa kasi kubwa sana na sasa kimekuwa ni tishio kwa Chama Cha Mapinduzi ndiyo maana mkasikia wagombea wetu wengi wameenguliwa Bara na Zanzibar kwa asabu ambazo hazina msingi, lakini nawaambia CCM, mwenyekiti atatoa msimamo wa chama sasa maonevu basi, nasema ng’ombe atakavyolala tutamchinja hivyohivyo. 

“Tunahitaji Serikali itakayowajali ninyi wananchi, itakayorudisha uhuru wa wananchi,” alisema Maalim Seif.

Awali, Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe alisema anawashukuru watu wa Lindi kwa kuwapa baraka ya kuzindua kampeni zao kitaifa kwa wagombea wao wa nafasi ya urais na makamu wa rais Bara na Zanzibar. 

 “Tayari mgombea wetu wa urais upande wa Zanzibar ameshatuzindulia kampeni hizi, wajibu wangu ni kuweka njia ili mgombea urais na mgombea mwenza wazungumze na Watanzania, lakini mmeona wagombea wetu wa ubunge wako hapa huku baadhi wakiwa wametangulia Dar es Salaam ambako kuna mafunzo maalumu”, alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles