24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Membe afafanua kuhusu kauli ya Nape

Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wiki moja baada ya Mwanasiasa nguli nchini, Benard Membe kurejea rasmi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu alipofukuzwa mwaka 2020, hatimaye ameeleza kuhusu kauli tata iliyotolewa siku ya kukaribishwa kwake na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Itakumbukwa kuwa Mei 29, mwaka huu Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje ya Nchi alikaribishwa tena ndani ya CCM baada ya miaka miwili aliyoishi nje ya chama hicho, akihamia ACT-Wazalendo na baadaye kutangaza kuachana nacho na kubaki kuwa mshauri wa kisiasa.

Nape alisema nini?

Mbunge wa Jimbo la Mtama ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema baada ya Membe kuondoka CCM wananchi wengi walichukia, lakini aliwaomba wasichukie kwani kuna siku moja atarejea.

“Leo mwenyezi Mungu ameturudishia faraja la Rondo, ameturejeshea furaha Chiponda. Mtama ni wastaarabu na hatuna shida tena,tuna imani kubwa na Membe, alinikabidhi kijiti na kuvaa viatu vyake, kulikuwa na mambo yaliyokwama huku nyuma kwa sababu za kisiasa, lakini Mama Samia amekuja ameziondoa,” alisema Nape.

Aidha, Nape alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Mtama kushikamana, fitina ambazo ziliingia kati zimekwisha.

“Membe amenipigania katika mambo mengi, nilipotaka ubunge baada ya kuonekana fitina zimeingia katikati Membe aliamua kuchora ramani.

“Ndio maana safari yangu ya ubunge imekuwa nyepesi. Kaka Membe amenipigania sana na bahati nzuri amerudi CCM. Niseme tu Mungu ameamua ugomvi,” alisema Nape.

Kauli hiyo iliibua mitazamo tofauti kutoka kwa baadhi ya wananchi wakitamani kujua ugomvi uliomalizwa na Mungu ni upi, huku tafsiri za baadhi yao zikijielekeza kwenye ugomvi wa kufukuzwa kwake CCM.

Ingawa kufukuzwa kwa Membe ndani ya CCM kulitokana na kile Kamati Kuu ya CCM ilichokieleza kuwa ni mwenendo wa kujirudia makosa licha ya kupewa adhabu nyingine lakini hakujirekebisha.

“Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake (Membe) ndani ya chama zinaonyesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha lakini imeonekana sivyo,” alisema aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, Februari 28, 2020.

Ufafanuzi wa Membe ni upi?

Akifafanua kuhusu kauli ya Mungu ameumaliza ugomvi, Membe alisema ililenga kuwaeleza wananchi wa Tarafa ya Rondo aliokuwa na ugomvi nao kwamba sasa umemalizika.

Alisema kufukuzwa kwake ndani ya CCM kuliibua hasira miongoni mwa wananchi, hatua ambayo ilisababisha katika moja ya mkutano wa Nape kuhudhuriwa na watu 12 pekee.

“Kwa sababu watu walikuwa na hasira na wakabishana pale …. Mimi mwenyewe sikuwepo. Nilipata tabu sana kama mbobevu, kama mataafu, kama mtu ambaye nilimshabikia Nape Nnauye.

“Sasa tumekwenda na hiyo misuguano hadi niliporejea CCM na Nape alikuwa miongoni mwa viongozi ndani ya chama waliokuwa wanakuja kila mwezi kuniomba nirejee CCM. Nikarejea CCM,” alisema Membe.

Baada ya kurejea CCM, alisema alizungumza na wananchi na kuwaeleza kuwa “Yaliyopita si ndwele tugange yajayo” na kusisitiza kuwa mtafaruku yao na Nape umalizike.

“Nilimtaka Nape alieleze hilo, sasa Nape ni msomi na mwanasiasa, akaliweka kwa lugha aliyoliweka. Kwa hiyo wananchi wa Rondo kauli ya Nape ni ya kueleza kwamba mgogoro wa wananchi wa Rondo na mbunge ambao walikuwa nao sasa umekwisha hiyo ndiyo tafsiri tuliyoipata,” amesema Membe.

Kinyume na tafsiri hiyo, Membe amesema magazeti yalikuja na yao ambayo hata yeye hakuwahi kuzungumzia.

Miaka miwili akiwa nje ya CCM, Membe aligombea urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo alichojiunga nacho Julai 15, 2020 miezi kadhaa baada ya kufukuzwa CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles