27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MELI 19 ZAPIGWA FAINI YA BIL 19/-

NA MWANDISHI MAALUM- ZANZIBAR

SERIKALI imeziamuru meli 19 za uvuvi kulipa faini ya jumla ya Dola za Kimarekani 8,636,363 sawa na Sh bilioni 19 ndani ya siku 14 baada ya kukiuka masharti ya leseni zao na kushiriki vitendo vya uvuvi haramu na uchafuzi mkubwa wa mazingira katika ukanda wa uchumi wa bahari kuu.

Meli hizo zinazotakiwa kulipa faini hiyo ambapo kila moja itapaswa kulipa faini ya Sh bilioni 1, ni Tai Hong no.2,  Tai Hong no. 8, Tai Xiang no. 5, Tai Xiang no.5, Tai Xiang no. 8, Tai Xiang no. 9, Tai  Xiang no. 9, Tai  Xiang no. 10, Tai Xiang no.7, Tai  Xiang  no 6, Tai Hong no  6, Tai Hong no .7, Xian Shiji no. 81, Xin Shiji no. 82, Xin Shiji no. 83, Xin Shiji no. 86, Xin Shiji no.76, Xin Shiji no. 76, Jian Shen no.1

Mbali na kutakiwa kulipa faini hizo, Serikali pia imeiagiza Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), kuwaandikia notisi wahusika wa meli hizo kuwajulisha kuhusiana na maamuzi hayo na pia kuijulisha Kamisheni ya kusimamia samaki aina ya Jodari, Bahari ya Hindi (Indian Ocean Tuna Commission –IOTC) juu ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kuhusu meli hizo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema jana mjini Zanzibar kuwa uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya meli hizo kukiuka Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 1998 Kanuni ya 10 ikisomwa kwa pamoja na Kanuni ya 68 ya Kanuni za Uvuvi wa Bahari Kuu za mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa kutoripoti katika bandari za Dar es Salaam, Zanzibar, Mtwara au Tanga kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kuondoka katika Bahari Kuu ya Tanzania.

“Kwa kitendo hiki cha kukiuka masharti haya ya leseni zao maana yake wameshiriki uvuvi haramu, wamechafua mazingira kwa kiasi kikubwa, wamefanya uvuvi holela na makosa mengine ya baharini, vitendo hivi vimekuwa vikikosesha Taifa mapato kwa kiasi kikubwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli, haitakubali tena kuchezewa na kugeuzwa Tanzania kuwa shamba la bibi kwa kila mmoja kuja na kuvua anavyotaka katika bahari yetu,” alisema Mpina.

Mpina aliongeza kuwa Serikali haiko tayari tena kufanya kazi na watu wanaovunja sheria za nchi na kwamba operesheni ya kuzisaka meli hizo itaendelea na zitaendelea kukamatwa kila siku kwani uhuru waliokuwa nao wakuiba rasilimali hizo za taifa haupo tena katika awamu hii ya tano.

Alisema eneo la bahari lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000 limekuwa likinufaisha mataifa mengine na kwamba msimamo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha rasilimali hizo zilizomo ndani ya eneo hilo zinachangia katika ukuaji wa pato la Taifa.

Katibu Mkuu wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa nguvu zote kulinda rasilimali za uvuvi na kudhibiti uvuvi haramu hivyo meli hizo zinazopewa leseni na kushindwa kufuata masharti zitaendelea kuchukuliwa hatua na kwamba maagizo yote ya Waziri Mpina atayasimamia ili yaweze kutekelezwa kwa wakati.

“Serikali haina mchezo katika jambo hili, itaendelea kuchukua hatua kali kwa lengo la kulinda rasilimali hizi ili ziweze kunufaisha Watanzania na Taifa kwa ujumla,” alisema.

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Divisheni ya Mashtaka Makao Makuu Dar es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Dawati la Makosa ya Mazingira na Malisiali, Wankyo Simon, alisema wamiliki wa meli hizo wasipolipa fedha hizo ndani ya muda uliotolewa na Serikali, taratibu za kuwafikisha mahakamani zitafanyika.

Aidha, Wankyo, aliongeza kuwa mbali na hatua hizo za Mahakama pia Serikali itawasiliana na nchi zilizotoa bendera kwa meli hizo ili kuzifutia usajili na kutoruhusiwa tena kufanya shughuli za uvuvi katika sehemu yoyote duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles