26.1 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

MECHI ZA NYUMBANI ZIWE FUNZO KWA SIMBA NA YANGA

TIMU za Simba na Yanga zilizokuwa zikishiriki kwenye mashindano ya kimataifa, zimeshindwa kufanya vizuri na hivyo kutolewa.

Yanga wao walikuwa wakishiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika, juzi ilitolewa baada ya kulazimishwa suluhu na timu ya Township Rollers ya Botswana, hivyo kusukumwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1 waliyofungwa katika mchezo wa kwanza katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutokana na matokeo hayo, Yanga wameangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo watamenyana na moja ya timu zilizofuzu hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Kwa upande wa Simba, wao walitupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, licha ya kulazimisha suluhu dhidi ya Al Misri juzi nchini Misri, hivyo kutolewa kutokana na sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo kongwe nchini zimeonyesha kuwa zinaweza kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya kimataifa kama zitaongeza nguvu hasa kwa kushinda idadi ya mabao mengi katika uwanja wa nyumbani.

Simba na Yanga zimecheza vizuri ugenini na hazikuruhusu nyavu zake kutikiswa, hii inaonyesha kuwa kama wangekuwa wamejipanga vema katika mechi za nyumbani kwa kupata ushindi, leo hii tungekuwa tunazungumza kwa kuzisifu na kuzipongeza.

Lazima timu hizi na hata nyingine za Tanzania zijifunze kuhusu hili, ukianzia nyumbani lazima uwe na mtaji wa mabao ya kutosha ya kufunga ili ugenini iwe rahisi kuzuia na hata ikitokea kufungwa iwe kwa uchache.

Lazima kuwe na mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa mechi za nyumbani ni mtaji na ugenini ni kusaka suluhu, sare au ushindi wa kushtukiza kama hali itakuwa ngumu kwa wapinzani.

Kwa kuzifuatilia Simba na Yanga katika mechi zake za nyumbani walizocheza, zimeonyesha udhaifu mkubwa wa kukubali nyavu zao kutikiswa na timu pinzani.

Hali ya kuruhusu kufungwa na wapinzani wako katika mechi unayocheza nyumbani, inawapa faida ya wakiwa nyumbani kwao, ndio maana timu nyingi zinapocheza ugenini hutafuta sare ili kazi iwe nyepesi kwao.

Sisi MTANZANIA tumeona hili liwe funzo kwa Simba na Yanga katika mechi zake za nyumbani na zihakikishe kuwa zinapata ushindi mnono ambao utawaweka vizuri katika mechi za marudiano wanapokuwa kwenye michuano ya kimataifa.

Ni lazima makocha wawe na mbinu za kuhakikisha kuwa ushindi wa mapema nyumbani ni bora, kwa kuwa unawapa mwelekeo katika mechi ya marudiano.

Kwa kuwa Yanga bado wanaendelea na michuano ya kimataifa, wachukue somo hilo na walifanyie kazi ili waliepuke kwenye Kombe la Shirikisho ambapo wameangukia.

Na kwa upande wa Simba, wajitazame upya na kujipanga mwakani kama wakibahatika kushiriki kwenye michuano ya kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles