23.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

MECHI YA WATANI… Sven awatoa hofu Simba, Yanga waapa

Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amewatoa hofu wapenzi wa timu hiyo kuelekea pambano la kukata na shoka dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga litalochezwa kesho kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Wakati ikiwa hivyo kwa upande wa Simba, Yanga wao wameapa kuwaliza wakongwe wenzao hao wa soka hapa nchini, zaidi wakitambia safu yao imara ya ulinzi.

Mtanange huo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka hapa nchini na kwingineko, unatarajiwa kuwa wa aina yake kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili.

Simba inaingia uwanjani kesho ikiwa imetoka kushinda mechi mbili mfululizo, zilizoirudisha mchezoni baada ya kupoteza michezo miwili na kuharibu hali ya hewa Msimbazi.

Wanamsimbazi hao wamepata mzuka zaidi baada ya juzi kuichapa Kagera Sugar mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini humo.

Baada ya mchezo huo, Sven, alisema anatambua mechi ijayo anakutana na Yanga, lakini hana wasiwasi na hawezi kuzungumzia sana, hadi watakapokutana makocha wote katika mkutano leo.

Alisema anachofurahia ni kiwango cha wachezaji wake kinavyozidi kuimarika na hadi sasa ana imani timu yake kupambana kupata ushindi.

Alisema katika timu hiyo, kila mchezaji anapambana na kujituma, wakiwamo wale aliowapa nafasi hivi karibuni.

Sven alieleza kuwa wapo majeruhi katika kikosi chake, ila anaamini nafasi zao zinaweza kuzibwa na wengine kutokana na mfumo aliotengeneza.

“Nafurahia kiwango kizuri cha wachezaji wangu walichoonesha kwa Kagera Sugar, mechi ya Yanga siwezi kuizungumzia, ina sehemu yake, ni TFF, tukikutana makocha kuzungumza Ijumaa (leo),” alisema Sven. 

Alifafanua kuwa kulingana na nyota alikuwa nao, mchezaji yeyote anaweza kuvaa kitambaa cha unahodha na kusimamia vizuri wenzake bila shida.

“Kitambaa cha unahodha wapo wachezaji zaidi ya saba wanaweza kukivaa, umeona siku nyingine Jonas Mkude, Tshabalala (Mohammed Hussein), Ndemla na wengine,” alisema Sven.

Simba inakutana na Yanga ambayo haijafungwa mchezo hata mmoja kati ya tisa ya Ligi Kuu Bara, huku Wanamsimbazi hao wakipoteza mechi mbili.

Kwa upande wa Yanga, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Cedric Kaze, amesema vijana wake wapo tayari kuiliza Simba kesho, akiahidi kutumia mbinu kabambe ili kuibuka na pointi zote tatu.

“Nashukuru wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wanasubiri kwa hamu mchezo na Simba na walichonihakikishia ni ushindi tu, hivyo mashabiki wa Yanga waje kwa wingi uwanjani, hatutawaangsuha,” alisema Kaze.

Kikosi cha Yanga kilichotoka kupata suluhu dhidi ya Gwambina, jijini Mwanza juzi, kimejichimbia huko Kimbiji kujiwinda na mchezo huo wa kesho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,293FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles