NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Dylan Kerr, amesema kipigo walichopigwa na mahasimu wao Yanga kimewaathiri wachezaji wake na kuwafanya wacheze chini ya kiwango dhidi ya Stand United juzi kwa kukosa umakini uwanjani.
Wekundu hao wa Msimbazi walishuka dimbani kuikabili Stand United juzi na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Joseph Kimwaga, wakitoka kufungwa mabao 2-0 dhidi hasimu wake Yanga.
Ushindi huo umeifanya Simba kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 12 sawa na Mtibwa Sugar zikitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Imeelezwa kuwa kikosi hicho kimeanza kurudi kwenye kasi na ubora wake licha ya juzi kupata ushindi wa kubahatisha dhidi ya Stand United katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kerr alisema pamoja na wachezaji kupoteza umakini kwa kufungwa na Yanga, kasi ya viwango vyao imeanza kuimarika huku akiendelea kuyafanyia kazi makosa hayo kabla ya mchezo unaofuata.
“Katika mchezo wa leo (juzi) wachezaji walionekana kuchoka mapema tofauti na ilivyo kawaida yao lakini waliporudi uwanjani kipindi cha pili walijitahidi kuongeza umakini na kutumia nguvu na akili na kubahatika kupata bao,” alisema.
Kocha huyo raia wa Uingereza alisema washambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Hamis Kiiza ‘Diego’ ambao hawakucheza kutokana na kuwa majeruhi wanaweza kucheza mchezo unaofuata kama afya zao zitaimarika.
Alisema anawaamini wachezaji wake kwa kuwa wanauwezo mkubwa wa kuipatia timu hiyo ushindi katika mechi zinazofuata Ligi Kuu.