22.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mdee apelekwa gerezani

Halima Mdee
Halima Mdee

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na wenzake nane jana wamekwenda gereza la Segerea baada ya kunyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Mdee na wenzake walifikishwa mahakamani hapo wakituhumiwa kufanya mkusanyiko kinyume na sheria kwa nia ya kutaka kuandamana kwenda Ikulu.

Watuhumiwa hao walipelekwa gereza la Segerea saa 10 jioni kwa kutumia gari la polisi lenye namba za usajili PT 1848.

Mbali ya gari, kulikuwa na magari mengine matano ya polisilikiwamo la maji ya kuwasha yakisindikiza msafara huo.

Wakati akiondoka mahakamani hapo, mbunge huyo alisikika akitumia kaulimbiu ya chama chake ya Peoples power.

Kabla ya Mdee kupelekwa gerezani, mawakili wa Chadema, Mabere Marando na Peter Kibatala walikuwa wakihaha kutaka kuonana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Isaya Arufani, ili atoe dhamana kwa watuhumiwa hao.

Jitihada za mawakili hao ziligonga mwamba baada ya Hakimu Arufani kukataa maombi ya mawakili hao.

KABLA YA KWENDA SEGEREA

Washtakiwa hao walisota mahabusu ya Mahakama ya

Hakimu Mkazi Kisutu kutwa nzima wakisubiri kupata dhamana baada ya kusomewa mashtaka.

Wafuasi wa Chadema na baadhi ya wabunge walioshinda mahakamani hapo, walianza kupoteza matumaini na kuhaha kuomba msaada kwa hakimu mwingine saa saba mchana baada ya Hakimu Mfawidhi Janeth Kaluyenda anayesikiliza kesi hiyo kwenda nyumbani kwa ajili ya kunyonyesha.

Walimfuata Hakimu Mkazi Hellen Riwa kuomba awasilikilize, lakini alisema hawezi kufanya hivyo kwa sababu Wakili wa Serikali aliyekwenda kuhakiki barua za dhamana hajarudi.

Awali washtakiwa hao walipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Kaluyenda na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa Serikali Mkuu, Kongola.

Kabla ya kusoma mashtaka, Kongola aliwataja washtakiwa kuwa ni Mbunge wa Kawe, Mdee, Rose Moshi, Penina Peter, Anna Linjewile, Mwanne Kassim, Sophia Fanuel, Edward Julius, Martha Mtiko na Beatus Mmari.

Alidai katika shtaka la kwanza kwamba washtakiwa wote wanadaiwa Oktoba 4 mwaka huu, Mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, walikaidi amri ya Ofisa wa Polisi SP Emmanuel Tillf iliyowataka watawanyike.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wote wanadaiwa Oktoba 4, mwaka huu, maeneo ya Mtaa wa Ufipa jijini Dar es Salaam wakiwa na lengo moja walikusanyika kinyume na sheria wakitaka kwenda ofisi ya rais.

Washtakiwa walipotakiwa kujibu mashtaka, walikana kutenda makosa hayo.

Kongola alidai upelelezi umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali, na Hakimu Kaluyenda alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21, mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Alisema mashtaka yanayowakabili yanadhaminika, na kuwataka kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, wawe na barua na vitambulisho.

Washtakiwa wote walipata wadhamini, lakini hata hivyo Kongola aliomba apewe muda wa kuhakiki barua za wadhamini na Hakimu Kaluyenda alikubali na kuongeza kwamba zikirudi na majibu mazuri watapewa dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kumfuta kazi mwanasheria mkuu wa Zanzibar mh.Shein amefanya uamuzi wa haraka sana. hii inaonyesha wazi kwamba wapo wengi hawakupenda baadhi ya vifungu ndani ya katiba pendekezwa lakini kwa unafiki wameshindwa kuonyesha hisia zao.
    binafsi namsifu sana mwanasheria huyo kwa kuonyesha hisia zake kama mwanasheria na mtanzania aliyepata bahati ya kuwa mmoja wapo wa watu watakao kumbukwa kwa kuwa na msimamo kwa manufaa ya watu wengi yaani Taifa/nchi yake/lake la/ya Zanzibar.
    Ikumbukwe kwamba katiba hii itaishi kipindi kirefu kijacho kama baadhi ya mambo muhimu na ambayo yamekuwa kero muda mrefu na hata kutishia amani ya nchi yasipo wekwa vizuri kisheria ni muda mfupi tu itakuwa na viraka mpaka itakuwa aibu kwa mashujaa wote walioshiriki kuitengeneza.
    Mwisho;-Ukweli unauma na Ukweli unagharimu kwa Dr. Shein ninaamini sio muumini wa visasi maamuzi aliyoyatoa anajua mwenyewe chanzo chake ni nini.
    Kwa mhe. mwanasheria uliyefutwa kazi ukweli umekugharimu lakini mimi ninaamini wewe ni hazina kwa taifa kwa viongozi wengine wajao wakitumia hekima zako muungano wa Tanganyika na Zanzibar utadumu na Tanzania itakuwa kisiwa cha amani milele

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles