22.7 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Mdahalo uchaguzi wa urais Marekani, Trump afufua matumaini, Clinton aendeleza ushindi

rs_1024x759-150709052426-1024-donald-trump-hillary-clinton-jr-70915_copy

Na JOSEPH HIZA,

UNAKUMBUKA lile pambano la ngumi lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa duniani mwaka jana baina ya Floyd ‘Money’ Mayweather wa Marekani na Manny Pacquiao wa Philippines?.

Bila shaka jibu litakuwa ndiyo kutokana na promo kubwa iliyotumika kulitangaza huku likitajwa kama pambano la karne.

Kingine kinachochangia kutosahaulika miongoni mwa wapenzi wa masumbwi ni kutokana na awali mabondia hao wakati wakihesabiwa kuwa ndio bora kuliko wote duniani kukwepana kuzichapa kwa miaka kadhaa.

Hatimaye walikutana Mei 2, mwaka jana kwenye ukumbi wa kihistoria wa MGM Grand Garden mjini Las Vegas, Nevada, Marekani ambapo Floyd Mayweather alimshinda Pacquiao kwa pointi.

Ushindi huo ulimfanya Mayweather kuendeleza rekodi yake ya kutoshindwa pambano hata moja tangu aingie katika ngumi za kulipwa.

Hata hivyo, licha ya kushindwa ni Pacquiao aliyekuwa kivutio kutokana na kushambulia kama nyuki kwa ngumi kali kali huku mpinzani wake akitumia muda mwingi kujihamu, akiachia ngumi kwa staili ya kudonoa, zilizompatia ushindi.

Staili hiyo ya ngumi baina ya mabondia hao, yaani ya kushambulia iliyotumiwa na Mfilipino na kujihami na kudonoa Mmarekani ndiyo iliyoshuhudiwa wakati wa mdahalo wa pili wa urais baina ya Hillary Clinton na Donald Trump nchini Marekani.

Mchuano huo wa Jumapili usiku huko St. Louis ulitajwa kuwa fursa nzuri ya mwisho kwa Trump mgombea kutoka Chama cha Republican kubaki katika kinyang’anyiro hicho baada ya kukabiliwa na miito ya kumtaka ajiengue kutokana na kauli zake za kidhalilishi dhidi ya wanawake.

Tangu mwanzo wa mdahalo, bilionea huyo wa New York, aliyeshindwa katika mdahalo wa kwanza, ambao alikuwa akiitikia zaidi huku mpinzani wake akishambulia, alihakikisha safari hii hampi nafasi mpinzani wake kutoka chama cha Democratic.

Hakika kama ule usiku wa Mei 2, 2015 unavyobakia katika kumbukumbu za wapenzi wa masumbwi, ndivyo basi usiku Oktoba 9, 2016 wa mdahalo wa pili utabakia kujadiliwa kwa vizazi vingi vijavyo katika madarasa ya Sayansi ya Siasa na semina za tafiti za wanawake.

Kwa kufanya hivyo, Trump alifanikiwa si tu kuzuia kushambuliwa bali pia kupoteza malengo ya shutuma mbalimbali zinazomkabili ikiwamo ukwepaji kodi na hili la kudhalilisha wanawake kimapenzi ambazo zinatishia safari yake ya kuelekea Ikulu.

Lakini mdahalo huo ulionesha tofauti baina ya mkakati wa Clinton na mbinu za Trump.

Clinton aliingia katika mdahalo huo, akiangazia mahitaji ya kisiasa ya siku 10 zijazo lakini mpinzani wake Donald Trump akilenga kunusuru maisha yake ya kisiasa.

Licha ya kupata fursa za kumshambulia mpinzani wake, Clinton alimhakikishia Trump kubaki katika kinyang’anyiro hicho, lakini akihakikisha anashinda japo kwa pointi mdahalo huo kwa staili ile ya kudonoa.

Wito kutoka chama cha Republican kutaka Trump ang’oke na kumpisha mgombea wake mwenza Mike Pence awanie kiti hicho, ulichoma mno masikio.

Pence, ambaye ameondokea kuwa kipenzi cha wana Republican wengi tangu amshinde Tim Kaine wa Democratic katika mdahalo pekee wa wagombea wenza, pia anashinikizwa amsuse Trump.

Uhai wa Trump katika kinyang’anyiro hicho ni kitu ambacho timu ya kampeni ya Clinton ilikitaka. Kambi hiyo inaamini uwepo wa Trump utawasafishia njia ya kuelekea Ikulu kirahisi kuliko kukabiliana na mgombea mwingine wa kaliba ya akina Pence.

Wanachotegemea kambi ya Clinton ni siku 30 zilizobaki za kampeni, ambazo Trump anaweza kufanya madudu zaidi ya kumnufaisha si tu katika urais bali pia useneta na ubunge kwa chama chao cha Democratic.

Wazo la mkakati halikuwepo katika nyoyo za kambi ya Trump, ambayo kampeni yake imejeruhiwa vibaya na inachofanya ni kutumia kila silaha iliyo nayo dhidi ya Clinton.

Inatumaini kwa mbinu hizo za kurusha mashambulizi makali si tu kutafufua imani ya kumbakisha miongoni mwa wana Republican bali pia fursa ya kuikamata White House.

Mashambulizi yake ya nguvu yalilenga moja kwa moja kubakiza wapiga kura wake watarajiwa weupe, wanaume, daraja la wafanyakazi.

Mbinu hizo zilitosha pia kuwakumbusha maadui zake ndani ya Republican wanaotaka ajiengue namna alivyopata ushindi uliompatia tiketi ya kukiwakilisha chama hicho licha ya kupigwa vita.

Kwa suala la Clinton kutumia barua pepe binafsi kwa masuala nyeti, Trump alitumia fursa hiyo kurusha mashambulia.

Lakini hakumwangusha moja kwa moja, badala yake Clinton aliyastahimili na kumpatia faida ya kimkakati.

Alimruhusu abwabwaje atakavyo; tishio lake la kumfunga jela Clinton iwapo ataingia madarakani; linahesabiwa kama matumizi mabaya ya madaraka pia kinyume kabisa na historia ya siasa na utamaduni unaoenziwa Marekani.

Kwa sababu hiyo, Democrats wamepata silaha ya kuitumia kuwa kitisho hicho cha Trump, ambacho tayari kimelaaniwa vikali ni ushahidi tosha hafai kupewa mamlaka ya kuwaongoza Wamarekani.

Na kitendo chake cha kuueleza wazi kuwa hakubaliani kabisa na msimamo wa mgombea wake mwenza, Mike Pence kuhusu mgogoro wa Syria kina faida kubwa kwa Democratic.

Mbaya zaidi Trump bila kupima athari ya matamshi yake, alisema hajazungumza na mgombea wake huyo mwenza kwa siku nyingi.

Hata hivyo, Pence ambaye siku moja kabla ya mdahalo huo alilaani kauli za kudhalilisha wanawake za Trump zilizosikika katika video ya mwaka 2005, alionesha ukomavu akisema hatajitoa kuwa mgombea mwenza wa Trump na anampongeza kwa kazi nzuri aliyooneshha katika mdahalo huo.

Kuwa tayari kushirikiana na Urusi kulishinda kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) kunazidisha wasiwasi miongoni mwa wapiga kura wa Marekani kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin anaingilia uchaguzi huo.

Wanamshutumu kwa kudukua taarifa za Chama cha Democratic na Clinton ili kumzuia Hillary kuwa Rais wa 45 wa Marekani na mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wenye mkubwa kuliko wote duniani.

Kuanzia sasa hadi siku moja kabla ya kupiga kura kuchagua rais hapo Novemba 8, kambi ya Clinton itatumia maneno ya Trump kunasa wapiga kura wa Republican na wale huru katika majimbo muhimu (swing states).

Huku kura za maoni zilizoendeshwa kisayansi na Shirika la Habari Marekani (CNN) zikimtangaza Clinton kushinda mdahalo huo wa pili kwa tofauti ya asilimia 13, Hillary amepata kile alichotaka licha ya kwamba alishambuliwa sana, yeye akienda kwa kudonoa donoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles