MCHUNGE MTOTO NA MICHEZO YA HATARI

0
624

NA AZIZA MASOUD,

MTOTO ana hatua mbalimbali katika makuzi yake.

Anapoanza kutambaa  ama  kutembea anahitaji kukaa katika sehemu ama nyumba  yenye eneo kubwa,  ili aweze  kuwa na nafasi ya kufanya vitendo hivyo vya ukuaji.

Mbali na kuishi katika eneo kubwa, pia mtoto anahitaji uangalizi wa karibu sana, hasa anapokuwa katika mazingira  yaliyozungukwa na vitu vingi.

Mtoto anapokuwa katika hatua ya kutambaa mpaka kutembea mara nyingi anakuwa katika kipindi cha hatari ya kupata ajali mbalimbali, ambazo nyingine humuwekea alama hadi ukubwani.

Katika kipindi hiki mzazi anapaswa kuwa makini, kwakuwa mtoto anakuwa katika hatua pekee ambayo wanaumia viungo, ikiwamo mikono, miguu, pia wapo wanaoungua moto ama maji ya moto au chai, hii yote inatokana na hali ya mtoto kutamani kushika kila kitu kilicho mbele yake.

Zipo ajali zinazomtokea motto, ambazo  ni ngumu kuzuilika, pia zipo zile ambazo zinatokana na uzembe wa mzazi au mlezi.

Ni vema mzazi kumjengea mtoto mazingira salama na eneo la kucheza, ikiwa ni pamoja na kumwondolea vitu hatari mbele ya macho yake.

Katika mazingira ambayo yamezungukwa na vitu vingi, hasa vinavyoweza kusababisha athari kwa motto, kama vyenye ncha kali, vitu vya kuvunjika mzazi unapaswa kuwa makini na mtoto anapoanza kutambaa.

Wakati anaanza kutambaa au kutembea, hakikisha unaondoa samani za kuvunjika na vitu vya umeme sebuleni na katika maeneo ya wazi ambayo unahisi atafika katika matembezi yake.

Mzazi unapaswa kuhakikisha vitu kama kisu, pasi, soketi za umeme pamoja na vitu vyenye asili ya udongo pamoja na majiko vinakuwa mbali na eneo ambalo mtoto anakuwa anafanya mizunguko yake ya kila siku.

Hata kama mzazi si mtu wa kushinda nyumbani, ni vema kutoa maelekezo kwa watu waliobaki ili kuhakikisha wanakuwa waangalifu na kumwangalia mtoto kwa ukaribu ili asipatwe na tatizo kwa wakati ambao wanakuwapo.

Mtoto anapocheza katika sehemu salama unamsaidia kumwepusha na majanga, ikiwamo kupata majeraha pamoja na ulemavu.

Ni vizuri kuchukua tahadhari ili kupunguza ajali ndogondogo zitokanazo na watoto.

Endapo utaona mtoto wako ni mtundu sana, hivyo hawezi kucheza eneo ambalo lina vitu kama sebuleni, ni vema ukamtengenezea eneo maalumu la kucheza.

Eneo hilo liwe lina uwazi ambalo litakuwa na vitu vidogo vidogo vya kuchezea ambavyo vitamsaidia kutopata akili ya kuzungukazunguka na kufikia sehemu ambapo huhitaji aende.

Ni vema kuwalea watoto katika mazingira salama ambayo yanakuwa chachu ya kumfanya awe mtulivu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here