25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mchungaji: Tusichague viongozi kwa itikadi za siasa

NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

KANISA la Babtist Tanzania limesema katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu Watanzania wanatakiwa kuchagua kiongozi  mwenye uwezo wa kuwatumikia wananchi bila kuangalia itikadi, kabila wala dini yake.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwangalizi Mkuu wa Makanisa ya Babtist Tanzania, Mchungaji Anord Manase, wakati alipofungua  kongamano la wanawake wa Kibabtisti nchini lililofanyika Chuo Kikuu cha Mount Meru wilayani Arumeru mkoani hapa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mchungaji Manase aliwakumbusha wanawake kuliombea kikamilifu Taifa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Ni vyema mkatambua kwamba tunahitaji viongozi waadilifu na wenye uwezo wa kuisaidia jamii ya Watanzania bila kuangalia itikadi zao za kisiasa, kabila wala dini.

“Ni wakati mwafaka wa kuangalia maneno, matendo na namna wanavyofanya uamuzi kwa manufaa ya Watanzania ili wananchi mwisho wa siku waweze kupata maji safi, huduma za afya, elimu na mambo mengine,” alisema Mchungaji Manase.

Alisema kanisa linao wajibu mkubwa wa kushiriki kwa kufuatilia kwa makini mambo yote yanayoendelea katika siasa ili itakapofika wakati wa kuchagua viongozi wananchi wawe na uwezo mkubwa wa kuwapima wagombea.

Kuhusu huduma ya akina mama ndani ya kanisa hilo, mchungaji huyo aliwataka kuhakikisha uanzishwaji na ukuaji wa umoja wao ndani ya makanisa ya Kibabtist.

Alisema hatua hiyo itawezesha umoja huo kuwa na nguvu kuanzia ngazi ya chini hadi juu ikiwamo suala zima la uwajibikaji wa viongozi wa makundi yote.

“Hatuwezi kuwa na matokeo tunayoyatarajia kama tuna watu wasiowajibika na wasio wazalendo katika huduma zetu ndani ya kanisa,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa akina mama wa Makanisa ya Wababtist, Dk. Lugano Mtafya, aliwashukuru wanawake hao kwa kuhudhuria kongamano hilo kwani litatoa mwamko mpya katika shughuli zao za ndani na nje ya kanisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles