Gustaphu Haule -Pwani
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste lililopo Kongowe, Kibaha Mjini mkoani Pwani, Japhes Manwa (40), akituhumiwa kutenda ukatili wa kumchoma moto mtoto wake mikononi na mgongoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Kibaha kuwa tukio hilo lilitokea Januari 21, mwaka huu saa saba mchana Kata ya Kongowe.
Kamanda Nyigesa alisema kuwa mtoto huyo wa kiume mwenye miaka saba, mlemavu wa utindio wa ubongo ambaye anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kalabaka ni wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto wanne wa mchungaji huyo.
Alisema kuwa inadaiwa mchungaji huyo hampendi mtoto huyo kwakuwa ni mlemavu na siku ya tukio alimchoma moto katika mikono yake miwili na mgongoni na kumsababishia maumivu makali.
“Kitendo alichofanya mchungaji huyu ni cha ukatili, kwani amediriki kumchoma moto mwanae wa kuzaa mikono yote miwili na hata mgongoni, kwahiyo tutaendelea kumshikilia mpaka hatua nyingine za kisheria zitakapochukuliwa,” alisema Kamanda Nyigesa.
Aliongeza kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi na baba yake katika Kata ya Soga, Kijiji cha Vikuge wilayani Kibaha baada ya kutengana na mkewe.
“Mtoto huyo wa kiume ni wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto wanne wa mtuhumiwa na alizaa na mzazi mwenzake Edina Ismail ambaye kwa sasa hawaishi pamoja, ndiyo maana alipata nafasi ya kumdhuru jambo ambalo ni ukatili mkubwa usiofaa katika jamii,” alisema Kamanda Nyigesa. Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuacha kutoa adhabu kali kwa watoto kwakuwa nyingine madhara yake ni makubwa na kama wanataka kuwakanya watoto wao ni vyema wakatoa adhabu zinazoendana na umri wao.