31.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Mchungaji Lwakatare achambua upepo wa kisulisuli

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MCHUNGAJI wa Kanisa la Mikocheni Assemblies of God, maarufu Mlima wa Moto, Getrude Lwakatare, ametoa ufafanuzi wa neno upepo wa kisulisuli huku akifurahi watu kutafsiri tofauti.

Amesema anafurahi jambo hilo la upepo wa kisulisuli limeweza kugusa jamii, wanaume na wanawake.

Maneno hayo upepo wa kisulisuli yamepata umaarufu baada ya Mchungaji Lwakatare ambaye wakati wa ibada kanisani kwake huwaita wasichana ambao hawajaolewa watoke mbele ili awaombee wapate waume wa kuwaoa.

“Wanaume kutoka Kaskazini, Magharibi, Mashariki waletwe na upepo wa kisulisuli, waletwe Mlima wa Moto waangalie wasichana wetu wawaoe,” anasema Mchungaji Lwakatare na kuwaita wasichana hao kutoka mbele mbio huku kila mmoja akiinua mikono kuomba kupata mume amtakaye.

UFAFANUZI

Akitoa maana ya maneno hayo wakati akihojiwa na moja ya televisheni ya kwenye mtandao, Mchungaji Lwakatare alisema upepo wa kisulisuli maana yake ni nguvu za Mungu.

Alisema mtu asiyeelewa anashika upepo wa kisulisuli kwa tafsiri yake, kitu ambacho si kibaya.

“Ukisoma katika kitabu cha Hesabu 11:4, Mussa alivyokuwa Jangwani na Wana Israel wakiwa wamechoka kula mana, wakalalamika wakisema Bwana tumechoka kula mana sasa tunataka kula nyama, kwanini umetuleta hapa tunakula tu mikate kila siku.

“Ndipo Mungu akasikia, akamwambia Mussa waambie Wana wa Israel kama hicho ndiyo kinawafanya wakonde, kinachowaumiza mioyo yao ni nyama basi tutaleta kware kwa upepo wa kisulisuli.

“Fikiria kware Jangwani, nyama ya kuwalisha watu wote itatoka wapi, sasa Mungu akaleta nguvu zake kwa njia ya upepo, kwa njia ya roho Mtakatifu, hiyo ndiyo imekuwa upepo wa kisulisuli,” alisema.

Akifafanua zaidi Mchungaji Lwakatare alisema ule upepo wa kisulisuli ndio uliweza kuleta kware ambao ni kuku wa kienyeji wa porini walio watamu zaidi kuliko kuku wa kienyeji.

Alisema kuwa Mungu alitaka kuwaridhisha kusudi ile hamu yao iishe, kwa hiyo kware waliswagwa kwa upepo wa kisulisuli kokote waliko hadi karibu na Wana wa Israel.

“Alisema tena haitakuwa zaidi ya mita moja, tena watakuwa hawana nguvu ya kuruka tena, kuna mtu yeyote angeweza kuwakamata wale kware, ilikuwa ni muujiza.

“Sasa watu wanafikiria upepo wa kisulisuli kwa sababu nilikuwa naombea wasichana waolewe, wanafikiri ni kwa ajili ya wasichana tu kwamba waletewe wanaume, lakini maana yake ni kwamba upepo wa Kisulisuli ulete kitu ambacho wewe unakihitaji zaidi kuliko vyote.

“Kwa mfano wewe hitaji lako ni gari, kwa upepo wa Kisulisuli Mungu akuletee gari kutoka Japan, kwa upepo wa kisulisuli Mungu akuletee mume, zile nguvu za Mungu akuletee cheo,” alisema.

Mchungaji Lwakatare alisema ilikuwa si rahisi kware wale maana wao kazi yao kukimbia kimbia kuruka, lakini pale walikaa, hata mtoto mdogo angeweza kuwashika, ule ulikuwa ni muujiza.

Alisema yeye kama mchungaji anaombea watu wote si wanawake tu, anaombea watu wasiozaa, wenye utasa au kama mtu mimba imekawia kuingia.

“Mimi nawaombea upepo wa kisulisuli wa Mungu maana yake ni roho Mtakatifu, lete mtoto kwa mama huyu ambaye ana haja ya mtoto, nachukulia ile kama silaha yangu ya kiroho.

“Sasa kama tatizo la wasichana wengi ni kuolewa, kwa mfano kanisani inajulikana kwa kawaida robo tatu ya waumini wanakuwa ni wanawake na robo ndiyo inakuwa wanaume au pengine theluthi tatu kwa moja, sasa kama theluthi mbili ni wanawake si lazima uombe.

“Sasa mimi nikiona mabinti wazuri, nikiona wasichana wangu wamekaa muda mrefu wakaniambia mchungaji mimi nataka mume, naomba niombee sitaki kutenda dhambi, sitaki kumuudhi Mungu, wenzangu wanaenda kwa mafundi, rafiki zangu wanaenda kwa waganga, sasa mimi lazima niombe kwa sababu mtoto ameamini Mungu, anampenda Mungu.

“Na mimi nasema sasa kwa nguvu na uwezo na silaha alizonipa Mungu katika jina la Yesu, basi naomba ulete wanaume Mashariki, Kaskazini, Magharibi waje waoe wasichana hawa.

“Wakati mwingine huwa nabadilisha kibao, nawaita wanaume, haya njooni vijana kwanini hujaoa unaponea wapi, lazima kama kweli umeokoka uoe mke wako mwenyewe,” alisema Mchungaji Lwakatare.

KUHUSU KUOA/KUOLEWA

Akizungumzia kuhusu kuoa au kuolewa jambo lililozua mjadala kwenye mitandao ya kijamii na watu mbalimbali, kuwapo idadi kubwa ya wasichana ambao hawajaolewa huenda ndiyo sababu ya yeye kuwaombea waumini wake, alisema mpango wa Mungu ni kila mtu kuoa na kuolewa.

“Kwa kweli mpango wa Mungu kwamba kila mtu awe na mume wake, ndiyo maana baada ya kumuumba Adam, Mungu akaangalia akasema si vyema mtu huyu akae peke yake nitamfanyia msaidizi.

“Kwa hiyo mpango wa Mungu tangu siku ya kwanza ni ndoa. Kwa sababu unaona kwamba Mungu kabla hajaanzisha taasisi yoyote duniani sijui mahakama au shule, alianzisha ndoa, akasema ndoa na iheshimiwe na watu wote.

“Nayo maradhi yawe safi maana wazinzi na waasherati Mungu atawahukumia adhabu, ndiyo maana unasikia kuna Ukimwi, magonjwa ya zinaa, ile ni adhabu.

“Mungu anataka kuwe na jamii na ndiyo maana akasema mtu na mume wake wajuane wakazae waijaze nchi ndiyo mpango wa Mungu. Kwa hiyo ukamilifu wa mwanadamu ni mtu kuwa na mume wake au mke wake,” alisema.

NDOA KUVUNJIKA

Kuhusu ndoa kuvunjika Mchungaji Lwakatare alisema mmomonyoko wa maadili unachangia kwani watu hawafundishwi maana ya ndoa.

“Ndoa inatakiwa iwe paradiso ndogo duniani ndiyo mpango wa Mungu, kwa hiyo kwa kukosa maadili watu hawakalishwi chini wakafundishwa kwamba ndoa ni nini, wengine wanafikiria ndoa ni fasheni kwa sababu rafiki zangu wote wameolewa na mimi nataka kuolewa, no (hapana).

“Eti kwa sababu mimi nisipokaa na mwanamume watanicheka, hapana lazima umjue yule ambaye unamuoa au unayeolewa naye, chukua muda wako, haraka haraka haina baraka, ukishamjua mtu anakuwa rafiki yako, hata mkioana ndoa inadumu.

“Mimi nilikuwa nasema kwa sababu ndoa ni taasisi takatifu, kama ulimpenda mwenzako umpende kama alivyo mtadumu, kuna wakati mwenye pesa atakuwa hana, akiwa mweupe akipata mimba atakuwa mweusi.

“Mpende mwenzako kama alivyo, muwe kama wazungu, wanamkubali kama alivyo tena anampa majina mazuri, akiwa mwembamba anasema; ‘the nearer the bones the sweeter the meat’ (ukaribu wa mifupa ndiyo utamu wa nyama).

“Ukubali ukatae mwanamume ni bidhaa adimu, huwezi kuipata super market, huwezi kumpata mwanamume, nenda China utarudi na masanduku, huwezi kurudi na mwanamume, nenda Marekani huwezi, ni Mungu ndiyo anakupangia huu ndiyo ubavu wako,” alisema Mchungaji Lwakatare.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles