31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mchungaji awaonya maaskofu kumuheshimu mkewe

NAIROBI, KENYA

MCHUNGAJI maarufu nchini hapa wa Kanisa la Neno Evangelist Ministry, James Ng’ang’a amegonga vichwa vya habari kwa mara nyingine tena baada ya kutishia kufunga matawi ya kanisa lake akidai kwamba maaskofu hawamuheshimu mke wake.

Picha ya video iliyosambaa katika vyombo vya habari, inamwonesha mchungaji huyo akiwakaripia maaskofu kwamba atawafurusha wote iwapo hawataheshimu onyo lake akidai kuwa matawi hayo yamekuwa vibanda.

“Wakati huu nitawaonyesha uwezo wangu… mwanamke yeyote ambaye hatamuheshimu mke wangu…. mulinipata hapa na wake zenu, mumejitajirisha kupitia juhudi zangu .

“Wajinga nyie… wajeuri… nilikuwa nikihubiri katika mkokoteni, naapa mbele ya Mungu nitawaonyesha Ng’ang’a ni nani…,” alisikika katika video hiyo akisema.

Mchungaji huyo anaonekana akiwaambia kwamba ni kinyume kwa wao kujigamba kuhusu utajiri waliojipatia kutoka katika kanisa lake na bado hawamuheshimu.

“Nataka kuwaambia nyinyi maaskofu, iwapo hamutamuheshimu mke wangu nitawafurusha katika kanisa langu. Sitaki kujua wewe ni nani,” alisema mchungaji huyo.

Alisema kuwa amefikisha umri ambao anahitaji kuheshimika na maaskofu wote. 

“Ninapokohoa lazima mutii,” alisema.

Mchungaji huyo alisema kuwa anakabiliwa na changamoto kwa sababu shetani anataka kuliangusha kanisa lake.

“Shetani anakabiliana nami kwa sababu anataka kuniangusha, hakuna kitu munachoweza kuniambia… Mimi ni Neno na ndio maana ninapigwa… Sitawaruhusu nyinyi na wake zenu kunipatia msongo wa mawazo zaidi.

“Iwapo munataka kujiita maaskofu, munahitaji kufikiria kule mulikotoka, ni vipi munajigamba mbele yangu na mulikuja kwangu na umaskini… nitawafukuza nyie nyote… takataka,” alisema.

Alisema kuwa atayafunga matawi yote na kusalia na makao makuu pekee.

Ng’ang’a aliwataja maaskofu wake kuwa watu wasio na maana, wajinga na wasiomuheshimu kama mtu aliyewasaidia.

“Ni lazima waniheshimu la sivyo nitaelekea kuvifunga mimi mwenyewe vibanda vyote nibakie na kanisa kubwa lililopo jijini Nairobi. Mimi ndio mwanzilishi wa Neno,” alisema huku akipongezwa na wafuasi wake.

Ng’ang’a alisema kuwa maaskofu katika matawi ya kanisa lake hawana heshima, lakini akawataka kujua kwamba yeye ndio kamanda mkuu.

Mchungaji huyo amegonga vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni kwa sababu ambazo sio nzuri.

Mwezi uliopita alikamatwa na maofisa wa polisi na kushtakiwa mahakamani kwa madai ya kumwibia mfanyabiashara mmoja pauni 36,000 kwa njia ya udanganyifu.

“Alikuwa amekubali kulipa, lakini akachelewa kuheshimu makubaliano hayo. Hivyo basi tuliamua kumchukulia hatua mahakamani,” alisema kamanda wa kituo cha polisi cha Central, Stanley Atavachi.

Katika kesi nyengine, alishtakiwa kwa kutishia kumuua mwandishi wa runinga ya Citizen nchini hapa, Linus Kaikai.

Pia anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ghasia na ukiukaji wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles