24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Mchumba wa Khashoggi akataa mwaliko wa Rais Trump

ISTANBUL, UTURUKI


MCHUMBA wa mwanahabari wa Saudia aliyeuawa, Jamal Khashoggi, Hatice Cengiz, anasema amesusia mwaliko wa Rais wa Marekani, Donald Trump, katika Ikulu ya White House kwa madai kiongozi huyo hajaonesha nia ya kutaka kujua ukweli kuhusu mauaji hayo ya kikatili.

Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni juzi nchini Uturuki, Hatice Cengiz amesema kwamba, mwaliko huo unalenga kubadili maoni ya Wamarekani. Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul wiki tatu zilizopita.

Utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia umekanusha madai ya kuhusishwa kwa familia hiyo katika mauaji hayo na badala yake umelaumu watu iliyowataja kuwa mawakala wa ukatili.

Katika mahojiano ya kusikitisha katika televisheni, Cengiz alielezea jinsi mchumba wake alivyotoweka baada ya kuingia ubalozi wa Saudia mjini Istanbul.

“’Kama ningelijua mawakala wa idara ya usalama wa Saudia walikuwa na njama ya kumuangamiza nisingelimruhusu kuingia humo,” alisema Cengiz.

Awali Saudia ilidai kuwa mwanahabari huyo ambaye alikuwa akiishi Marekani, alitoka ndani ya ubalozi wake.

Baada ya shinikizo wakasema kuwa aliuawa alipojaribu kupambana na baadaye wakakiri kuwa aliuawa katika operesheni isiyo rasmi na ambayo haikubarikiwa na Mfame wa nchi hiyo, Mohamed Bin Salman.

Huku hayo yakijiri, mtoto wa kiume wa Jamal Khashoggi, Salah Khashoggi pamoja na familia yake wamewasili Marekani siku chache baada ya kukutana na Mwanamfalme Mohammed Bin Salman.

Hadi sasa mwili wa mwanahabari huyo haujapatikana, huku Mwendesha Mashtaka wa Saudi Arabia akisema mauaji ya Khashoggi yalikuwa yamepangwa.

Mapema wiki hii Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alisema kuwa mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi yalipangwa siku kadhaa kabla ya kutekelezwa.

Erdogan alisema hayo alipokuwa akiwahutubia wabunge wa chama tawala nchini Uturuki. Alisema Uturuki ina ushahidi mkubwa wa kuthibitisha kuwa mauaji ya Khashoggi yalikuwa yamepangwa na kutekelezwa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Oktoba 2, mwaka huu.

Erdogan sasa anataka washukiwa wa mauaji hayo wafunguliwe mashtaka mjini Istanbul, Uturuki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,207FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles