29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mchujo wa pili CCM waanza

Na MWANDISHI WETU

BAADA ya  kukamilika kwa mchakato wa kwanza ndani ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa  kuwachuja wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia kura za maoni zilizofanyika kote nchini, mchakato wa pili unaoshabihiana na huo umeanza.

Mchakato huo ambao baadhi wanaona umebeba sura ya  ‘mchujo wa pili’ unahusu maamuzi yatakayofanywa na ngazi ya wilaya.

Kwa mujibu wa wa taratibu za CCM, ngazi hiyo ya wilaya  ikifuatiwa na ile ya mkoa imepewa jukumu la kuitisha vikao  kwa ajili ya kujadili, kuweka maksi, na kutoa mapendekezo  ya zoezi zima la kuwapata wagombea na wagombea waliopatikana baada ya kupigwa kwa kura za maoni na wajumbe wa chama hicho.

Ratiba ambazo gazeti hili limeona tayari baadhi ya wilaya zilianza mchakato huo jana na nyingine zinatarajiwa kuanza leo na kukamilisha kesho Jumatatu na kisha kuelekea ngazi ya mkoa kabla ya ile ya vikao vya juu kabisa vya CCM.

Kwa mujibu wa ratiba hizo, mchakato ndani ya wilaya nyingi umeonekana kuanza kwa wagombea ubunge kwa siku moja na kisha udiwani siku ya pili.

Ratiba hizo zimewaelekeza wagombea wote katika siku waliyopangiwa kufika bila kukosa mbele ya Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya kwa ajili mahojiano.

Kuitwa kwa wagombea wote ni agizo la juu la chama hicho na hivi karibuni tu, Katibu Mkuu wa CCM , Dk. Bashiru Ally alisisitiza majina ya wagombea wote yajadiliwe kama ilivyokuwa katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.

Itakumbukwa wagombea wote watano waliopendekezwa kwenye vikao vya awali vya Zanzibar na kupelekwa Kamati Kuu ya CCM, waliitwa Dodoma ingawa matokeo hayakubadilika. 

Tangazo la ratiba hizo zimewataka wagombea kufika na kadi zao zote kama CCM, Wazazi, UWT na UVCCM pamoja na kitambulisho cha mpiga kura.

Wagombea pia wametakiwa  kufika na uthibitisho mwingine walionao kama elimu, kazi, biashara na nakadhalika.

Wakati vikao hivyo vikiwa vimeanza na vingine vikijiandaa kuketi leo na kesho zipo dalili za kuibuka kwa hoja ya rushwa ambayo imetuhumiwa waziwazi na baadhi ya wagombea katika baadhi ya maeneo.

Baadhi wanaolalamika wanaona taarifa za kuwako kwa rushwa imetoa matokeo yasiyo ya haki kwa baadhi ya wagombea.

Kama hilo likitokea wafuatiliaji wa siasa ndani ya chama hicho wanasema mapendekezo au maksi zitakazotolewa katika vikao vya wilaya au mkoa huenda pia yakabadili matokeo ya awali yaliyowapa ushindi baadhi ya wagombea.

SI WAJUMBE HATMA SASA W/VITI

Wakati ngazi ya kura ya maoni walioonekana kushika hatma ya wagombea wakiwa ni wajumbe, katika ngazi ya wilaya na mkoa wanaoonekana kushikilia nafasi hiyo sasa ni  Wenyeviti na Makatibu  Wakuu  wa Wilaya wa CCM na baadae mkoa.

Zipo taarifa zinazoeleza kuwa baadhi ya wagombea walioshinda na walioshindwa  wameanza kutafuta mbinu na wengine kujaribu kurekebisha tofauti zao na viongozi hao, ili vikao hivyo vitakapoketi wawakumbuke kuwapatia maksi nzuri.

Aidha Wenyeviti wa CCM wa ngazi ya wilaya na mkoa waliogombea nafasi hizo za ubunge au udiwani kwa mujibu wa Dk.Bashiru hawataruhusiwa  kushiriki katika vikao hivyo vya maamuzi kwa sababu wana maslahi.

POLEPOLE/VIKAO YA JUU

Wakati vikao hivyo vya ngazi ya wilaya vikiwa vimekwishaanza, vikao vya juu vya chama hicho bado haijajulikana vitaanza lini.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema ratiba ya vikao vya juu ya chama hicho kwa ajili ya kuwajadili wagombea ubunge na udiwani pamoja na Ilani ya chama hicho bado haijapangwa na kwa sasa wapo kwenye mchakato huo.

Alisema ratiba itakapopangwa itafahamika na mchakato utaendelea. 

Vikao hivyo vya ngazi ya wilaya na ile ya mkoa navyo vina kibarua chake kama ilivyokuwa wakati wa kura za maoni kutokana na idadi kubwa ya watia nia waliojitokeza kugombea nafasi hizo.

Mchakato wa kura za maoni ulianza kufanyika Julai 20,2020. 

Wagombea wa nafasi zote walipewa nafasi ya kujinadi kwa wapiga kura ambao ni wajumbe walioamua hatma yao.

‘Wajumbe’ sasa limekuwa kama neno la utani katika mazungumzo na mitandao ya kijamii kutokana na shughuli ya kukata wagombea ilivyofanyika.

Wengi wamewanyooshea mkono  baadhi yao na  hata kuibua malalamiko makubwa ya tuhuma za rushwa.

Baadhi ya wachambuzi walisema tangu mwanzo kwamba kura hizo za maoni huenda zikawa moja ya mtihani mkubwa kwa chama hicho na jambo hilo tayari limedhihirika kutokana na si tu wingi wa wagombea bali malalamiko hayo ya rushwa yaliyoibuliwa waziwazi na baadhi ya wagombea na wanaCCM. 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli jumla ya wagombea wa ubunge waliochukua fomu walifikia 10,367 na waliorejesha walikuwa 10,321 na 46 hawakurejesha.

WALIOANGUKA MATUMAINI YAPO?

Mchakato huo wa mwanzo wa kura za maoni pia  umeshuhudia wabunge waliomaliza muda wao zaidi ya 70 wakianguka kwenye kinyang’anyiro hicho wakiwamo wateule wa rais kama vile wakuu wa mikoa,wilaya na makatibu wakuu ambao nao walijitosa kwenye kwenye mbio hizo.

Wabunge na wateule hao wa rais ambao uteuzi wao ulikwishatenguliwa ambao baadhi wameshindwa pia  kwenye kura za maoni sasa na hawajui hatma yao ya kisiasa nao pia wameelekeza imani yao kwenye vikao hivyo vya juu. 

Huko nyuma watendaji wakuu wa CCM walipata kuwaonya wateule hao wakiwataka watosheke na nafasi walizonazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles