MCHICHA DAR SI SALAMA

0
1328

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


LICHA ya watu wengi kupenda kutumia mboga za majani ikiwamo mchicha katika Jiji la Dar es Salaam, ni wazi sasa mboga hiyo inayolimwa katika bonde la Mto Msimbazi si salama tena kwa afya ya binadamu.

Hatua hiyo inatokana na wakulima wengi wanaolima katika bustani za mboga katika eneo hilo, kutumia maji yanayotiririka katika Mto Msimbazi na Kibangu yaliyo na kemikali zinazotoka viwandani ambazo ni hatari kwa afya za wakazi wa jiji hilo.

Jopo la wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) na Taasisi ya Mto Wami, wametoa matokeo ya awali kuhusu vipimo vya maji ya Mto Msimbazi.

Maji hayo yenye kemilikali za sumu yamekuwa yakimwagiliwa kwenye bustani hizo za mchicha ambao hutumiwa kama mboga na sehemu kubwa ya wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Timu hiyo ya wataalamu ilikuwa imeambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina ambao walilazimika kuchukua sampuli ya vipimo na kupima maji hayo na ilibaini kuwa na viuatilifu ambavyo ni hatari kwa wananchi wanaotumia mbogamboga na mimea inayomwagiliwa na maji hayo.

Mbali na hilo, pia wananchi wanaotumia mchicha huo wa bonde la Mto Msimbazi wapo hatarini kupata maradhi ya saratani na kuathiri mfumo wa akili.

Kutokana na matokeo hayo ya awali, Naibu Waziri Mpina alitoa siku 14 kwa jopo hilo la wataalamu kuwasilisha matokeo mengine ya mabonde matano yaliyopo Mkoa wa Dar es Salaam ili kuweza kutoa maelekezo ya kitaalamu.

Mpina alisema ni muhimu kujua ubora wa maji ya mto huo na Mto Mlalakuwa, Kibangu, Ng’ombe na Kijitonyama ili kama kuna watu viwanda au makampuni yanayotiririsha maji yenye kemikali zenye sumu, waweze kuacha mara moja sambamba na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema uchafu wa mazingira ni mkubwa viwandani, hususani kwa viwanda visivyo na mfumo  wa majitaka.

Kutokana na hali hiyo, aliwaonya wote wanaohusika katika kutiririsha maji hayo yenye kemikali kuwa sheria ya mazingira haitawaacha.

Alisema matokeo hayo ya uchunguzi yatasaidia kujua athari zitokanazo na maji hayo na jitihada madhubuti za kuchukua ili kutunza na kuhifadhi vyanzo vya mito.

Kwa upande wake, Mkemia Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Emanuel Gwae, alisema vipimo vya awali vinaonyesha maji hayo yana hewa ya oksijeni miligram 3.3 ambayo viumbe hai hawawezi kuishi na kwamba yalitakiwa kuwa na miligram 6.

Alisema watachunguza madini tembo katika maji hayo ambayo ni kemikali zinazoweza kuwa na  madhara kwa jamii ikiwamo viuatilifu vyenye kusababisha satarani kwa watumiaji wa mazao ya mbogamboga katika eneo hilo.

Naye Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto, alisema wananchi watafaidika kiafya kutokana na malalamiko yao ya muda mrefu.

Hatua ya kupimwa kwa maji hayo yenye kemikali zenye sumu kutoka viwandani, inatokana na ziara iliyofanywa na Naibu Waziri Mpina, juzi katika bonde la Msimbazi na kupokea malalamiko ya wakulima wa bustani kwenye eneo hilo kuhusu maji hayo ambayo yamewachubua ngozi pindi wanapoyatumia kwa shughuli za umwagiliaji.

Hata hivyo, eneo kubwa la wakazi wa Dar es Salaam, hasa waliokuwa jirani na mabonde yenye mito wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo cha bustani za mbogamboga na kuonekana kama eneo mbadala la kujiari na kujipatia kipato kwa kuendesha maisha yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here