30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

MCHEZO WA SOKA UNAVYOJIVUA GAMBA  

 

ADAM MKWEPU NA MITANDAO


UNAWEZA ukawa wakati mgumu katika historia ya mchezo wa soka duniani, kutokana na mabadiliko au mapinduzi ya baadhi ya kanuni, sheria na taratibu zinazotumika kuendesha mchezo huo,  yanayotarajiwa kufanyika chini ya uongozi wa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) Gianni Infantino.

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la hilo, Marco van Basten, ni mmoja kati ya wanaoandaa mapinduzi makubwa katika soka yanayolenga kufanya maboresho katika maeneo yenye ukakasi.

Van Basten ni miongoni wa kongwe katika soka ambao wana mafanikio makubwa katika mchezo  huo lakini anaonekana kufikiria kufanya mapendekezo kadhaa ambayo anaamini yatakuwa na tija.

“Tunatakiwa kuangalia soka, kila siku lazima kuhakikisha tunaendelea katika mchezo huo ili kuufanya mchezo wenyewe kuaminika na kuwavutia wengine.

“Ninatamani sana kuona namna gani mchezo wa soka unachezeshwa bila kuwa na ‘offside’, nina hofu kwamba watu wengi watapinga jambo hilo, binafsi napenda litokee kwa sababu itafanya mchezo kuvutia zaidi,”alisema Van Basten alipozungumza na Sky sport.

Kiongozi huyo anaongeza kuwa yapo mapendekezo ya kuondoa kadi ya njano na adhabu ya muda wa dakika tano au kumi kabla ya dakika 90 za mchezo kumalizika.

Akizungumzia kuhusu penalti, anasema mpigaji anaweza kuchezea mpira ndani ya dakika nane akiambaa golini kwa kipa umbali wa mita 25.

“Jambo jingine tunataka kubadili idadi ya michezo kwa mwaka, tunafanya  kila kitu ili kuhakikisha mchezo wa soka unakuwa bora kwa kuwa tunapata fedha nyingi kupitia soka, kwenye soka hakuna tatizo la pesa tunachotakiwa kufanya ni kuangalia ubora wa mchezo wenyewe.

“Tunatakiwa kupunguza michezo kwa mwaka kutoka 80 hadi 50 ili kuweza kuwasaidia wakina Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Zlatan Ibrahimovic ambao mashabiki wao wanataka kuwaona kila siku,” anasema Van Basten.

Van Basten pia amezungumzia kupunguza idadi ya mpira wa adhabu kutokana kuwa mingi hivyo  zinaitajika kupunguzwa.

“Nina wazo kwamba beki anayecheza mchezo wa kikapu anaweza kufanya jumla ya faulo tano katika mchezo na kutolewa nje kwa nini jambo hilo lisitokee katika soka.

Aidha mapendekezo mengine ya mabadiliko kuonekana katika michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kufanyika nchini Urusi mwaka 2018.

Moja ya mabadiliko hayo ni kuwapo  mpango wa kupunguza muda wa kipindi cha kwanza na kile cha pili cha mchezo ili kuwa dakika 30 badala ya 45.

Bodi ya kimataifa ya soka duniani inajiandaa kujadili pendekezo hilo linalolenga kuondoa muda unaopotezwa kwa makusudi ndani ya uwanja.

Waliopendekeza mpango huo wanasema kuwa mechi huchezwa kwa dakika 60 pekee kati ya 90 na muda uliobakia hutumiwa kupoteza wakati.

Wanapendekeza dakika 30 kila kipindi huku wakisimamisha muda kila mpira unapotoka nje ya uwanja kusaidia kukabiliana na muda unaopotezwa lengo likiwa kuufanya mchezo kuvutia zaidi.

Hata hivyo wakosaoji wanasema kuwa mabadiliko kama hayo hayatakuwa na umuhimu wowote iwapo sheria ya kupoteza muda itaimarishwa.

Pendekezo jingine ni lile la wachezaji kutoruhusiwa kupiga mpira mara ya pili baada ya kipa kuupangua wakati wa penalti.

Na iwapo penalti hiyo haikupigwa ilivyotarajiwa, mchezo utasitishwa na mpira wa adhabu kutolewa kuelekea kwa timu ambayo mchezaji wake amefanya makosa hayo.

Mapendekezo mengine yanashirikisha kuweka saa katika uwanja ambayo italingana na ile ya refa mbali na sheria mpya itakayoruhusu mchezaji kujipigia mpira ama hata kuambaa na mpira wakati anapopiga mpira wa adhabu.

Tayari aliyekuwa mkufunzi wa timu ya Chelsea, Gianfranco Zola anapendelea pendekezo hilo la kupunguza muda wa mechi hadi dakika 60.

Moja ya majaribio ya mapendekezo hayo yalifanyika nchini Japan katika mashindano ya FIFA ya Kombe la Dunia kwa Klabu   yaliyofanyika Juni mwaka huu na waamuzi wa mechi hizo walipata msaada wa maamuzi yao kwa kutumia video kutoka kwenye mfumo wa majaribio uitwao VARs.

Mfumo huo wa Video huwasaidia waamuzi kutoa uamuzi wawapo uwanjani, umefanyiwa majaribio rasmi ya FIFA kwa mara ya kwanza katika mechi ya kimataifa  Septemba  mwaka huu wakati Italia ilipocheza na Ufaransa  nchini Bari.

Kwenye  mfumo huo wa Video, mwamuzi msaidizi anakuwapo pembeni mwa uwanja na ana kuwa na mawasiliano na mwamuzi  wa mechi wakati wote wa mechi hiyo akipitia video bila kusitisha mechi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles