Mchegerwa  atoa onyo watumishi wanaobania walimu

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),  Mohamed Mchengerwa,  amesema yuko tayari kutofautiana na watumishi   wanaokwamisha utatuzi wa changamoto za walimu ambao wanalitumikia Taifa  kwa moyo.

Chengerwa metoa kauli hiyo jana  Novemba 27, 2023,  jijini Dar es Salaam wakati wa  hafla ya  kukabidhi gari, pikipiki  62 na kompyuta mpakato 159 kwa Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu iliyofanyika kwenye shule ya sekondari Tambaza.

“Nikiwa Ofisi ya Rais – Utumishi chini ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita tuliwapandisha madaraja walimu 227,363 na kuwabadilishia walimu 11,642 lakini katika kufanikisha hili kuna wakuu wa idara ya utumishi tuliwaondoa kwenye nafasi zao kwa sababu walikuwa wanakwamisha haki hizi za walimu.

“Sasa nielekeze tena katika kipindi changu kusikia changamoto za walimu kila mmoja kwenye nafasi yake anayehusika kwa namna moja au kutatua changamoto za walimu awajibike ipasavyo vinginevyo  nitamchukulia hatua stahiki,”amesema Mchengerwa.

Amesema kipindi hiki kitakuwa kigumu kwa wale watumishi  wazembe katika kutekeleza majumuku yao lakini kitakua kizuri kwa wale wanaochapa kazi kwa maslahi ya watanzania.

“Nataka changamoto zote za walimu za kupandishwa madaraja na malimbikizo ya mishahara zikafanyiwe kazi ipasavyo,”amesema.

Kuhusu wakurugenzi wanaosubiria bajeti amesema yeyote atakayefanya hivyo, atalazimika kusubiri bajeti hiyo akiwa nje ya mfumo wa Serikali, huku akiwasisitiza kutumia makusanyo ya ndani ya halmashauri kutekeleza hilo.

Amesema serikali haitakubali kumuona Mkurugenzi wa Halmashauri yoyote atakayesingizia bajeti ya Serikali kuu kuchonga madawati kwa ajili ya shule za eneo lake.

Ameongeza kuwa ili kutekeleza hilo, alitaka mipango ya maendeleo, kila halmashauri iweke kipaumbele mahitaji yanayowasaidia wananchi kwanza.

“Wakurugenzi wa halmashauri, mpango wa maendeleo uendane na mahitaji ya wananchi katika eneo husika, kwamba mahitaji ya kwanza yawe yale yanayokwenda kusaidia watanzania katika maeneo husika,” amesema.

Aidha amesema zipo halmashauri zinazojiwekea mpango wa matumizi makubwa ambayo si ya msingi kwa wananchi wa eneo husika.

Ametolea mfano kuwa yapo maeneo ambayo wananchi wanahitaji madawati 50, mkurugenzi anasema anasubiri bajeti ya serikali kuu kupeleka madawati 50 au 100.

“Taifa litapiga hatua iwapo kila mmoja atajitoa kwa ajili hio, haiwezekani tujiwekee mpango wa matumizi makubwa ya fedha ambayo hayana faida kwa wananchi na mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa yupo,” amesema.

Amesema wapo wanaopewa nafasi lakini hawawafikirii watanzania bali kujitanguliza wao na kwamba yuko tayari kumlinda anayewajali wananchi kwanza.

 Mchengerwa ameitaka TSC ifanye tathmini ya muongozo wa walimu, kisha iishauri Serikali namna nzuri ya kuhakikisha  wanapata stahiki zao.

“Mkajipange kuhakikisha mnafanya tathmini ili kuishauri serikali juu ya walimu wanaokwenda kusoma mishahara yao iendane na ngazi za elimu yao na kuishauri serikali namna bora ya kulinda maslahi ya walimu na kuongeza kuwa  Serikali imejenga zaidi shule na miundombinu ya elimu, amesema kwa sasa inatarajia kukuelekeza katika ujenzi wa nyumba za walimu,”ameeleza. 

Pia amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha shule zinazojengwa katika maeneo yao zinakamilika ndani ya muda zikiwemo zile za Novemba 30 na Desemba 30, mwaka huu.

Naye  Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Paulina Mkwama amesema vifaa hivyo vinavyokabidhiwa leo vitasaidia kuboresha utendaji kazi kwa watendaji wa tume na kuboresha utoaji wa huduma.