27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MCHANGO WA MAHAKAMA KURAHISISHA UFANYAJI BIASHARA WAHITAJIKA NCHINI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


KILA mwaka mahakama huadhimisha Siku ya Sheria nchini, maadhimisho hayo huambatana na kaulimbiu ambapo mwaka huu ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa Wakati Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi’.

Kaulimbiu hiyo ina lengo la kuifanya mahakama kuwa sehemu ya kuongeza pato kwa Taifa.

Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria, aliweka wazi mkakati wa kukuza uchumi na kuelezea mahakama jinsi inavyoweza kuwa sehemu ya kukuza uchumi.

Anasema utoaji haki una mchango mkubwa katika uchumi na katika urahisi wa kufanya biashara.

Pamoja na jukumu kuu la kutoa haki, mahakama imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi inajenga na kuweka mazingira bora ya biashara shindani ili kuvutia uwekezaji, kama ilivyojieleza kwenye maudhui ya Siku ya Sheria.

Jaji Juma anasema ili kuvutia uwekezaji nchini Tanzania, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano, uliweka lengo la kuwa Tanzania iwe miongoni mwa nchi bora 100 duniani katika vigezo au viwango vya mazingira ya

biashara.

Anasema kwa mwaka 2016, taarifa ya Benki ya Dunia ilionyesha Tanzania kushika nafasi ya 139 ( imedorora kwa ripoti iliyofuata ya  2017 na kuwa  nchi ya 144) kati ya nchi 189 duniani.

“Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kigezo cha kusimamia mikataba tu ndicho kilifikia mafanikio ya lengo ya kuwa ndani ya 100 bora kwa kupata nafasi ya 64 ( na iliboreka kuwa nafasi ya 60 kwa ripoti ya mwaka 2017) duniani, fanikio hili ni juhudi za mahakama katika kutekeleza majukumu yake,” anasema.

Anasema taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2017, inaonesha kwamba kiujumla Tanzania imekuwa nchi ya 132 kati ya nchi 190 duniani, ikiwa ni fanikio

la kupanda nafasi 12, kwa kigezo cha kusimamia mikataba imeshika nafasi ya 59.

Taarifa hiyo pia inaonesha kuwa, katika kundi la nchi 27 duniani za kipato cha chini, Tanzania imeshika nafasi ya 4kiujumla na kwa kigezo cha kusimamia mikataba imeshika nafasi ya kwanza.

Kiongozi huyo wa mahakama anasema eneo la kusimamia mikataba limekuwa na ufanisi mkubwa kwani Tanzania imeweza kushika nafasi ya tatu kati ya nchi 47 za Kusini mwa Jangwa la Sahara

Anasema hayo ni mafanikio makubwa na ya kujivunia kwa nchi yetu katika kuboresha mazingira ya kibiashara ili kuvutia uwekezaji na kuongeza ukuaji wa uchumi.

Jaji Juma anasema mahakama imeendelea kuboresha maeneo yanayopimwa katika viwango vya mazingira ya biashara kwa kufanya

maboresho katika utoaji wa huduma za kimahakama kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 – 2019/20).

 

Mafanikio hayo yameanza kujidhihirisha katika kuboresha mazingira ya biashara kwa mfano; mahakama kwa mwaka huu, ilijiwekea lengo la wastani wa siku 480 kumaliza shauri la kibiashara.

Takwimu zinaonyesha ni wastani wa siku 390 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, kiwango hicho ni sawa na lengo lililotegemewa mwaka 2020/21 ambalo ni siku 380 kadiri ya viashiria vya malengo hayo.

“Tunaomba sana kupitia kwako wadau wengine kwenye vigezo muhimu saba vya urahisi wa kufanya biashara, watimize wajibu wao kama ilivyo kwenye usimamizi wa mikataba eneo la upatikanaji wa umeme ambayo kwa sasa Tanzania inafanya vizuri,” anasema.

 

Rais Magufuli anena

Akizungumzia suala la kukuza uchumi, Rais Dk. John Magufuli anasema kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, Serikali ilishinda kesi za kodi ambazo thamani yake ni Sh trilioni 7.5 lakini fedha hizo hazijakusanywa mpaka sasa.

Anasema ni kwa namna gani utoaji haki unaendana na kukuza uchumi wakati kiasi hicho cha fedha hakijakusanywa.

“Nikiwa kama Rais suala la utoaji haki kwangu ni upatikanaji wa fedha za kuwatumikia Watanzania,” anasema.

Anasema wakwepa kodi ndio wanaoheshimika katika nchi na kueleza kusikitishwa kwake na namna mahakama inavyoshughulikia kesi zinazohusiana na ukwepaji wa kodi na anatoa wito kwa mahakama na wadau wake kujipanga kukabiliana na dosari hiyo inayorudisha nyuma juhudi za maendeleo ya nchi.

Dk. Magufuli ameipongeza mahakama na wadau wake kwa kazi kubwa inayofanywa kuleta mabadiliko na uboreshaji wa huduma na miundombinu na ametaka kaulimbiu ya mwaka huu itekelezwe vizuri kwa kutanguliza masilahi ya Taifa, ikiwamo kuhakikisha wanaopatikana na hatia ya kukwepa kodi wanalipa.


“Haiwezekani mwekezaji anachimba madini yetu, kodi halipi, anashtakiwa mahakamani anashindwa, halafu pesa haitolewi.

“Sasa tujiulize, kama utoaji haki unaakisi ujenzi wa uchumi wa nchi, ni kwa kiasi gani kesi zenye thamani ya Sh trilioni 7.5 zimeathiri uchumi?” anahoji Rais Magufuli.

Amezitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na mahakama wajipange kwa pamoja ili kushughulikia ipasavyo mashauri mbalimbali na kuondokana na migongano ambayo imekuwa ikidhohofisha ufanisi wa shughuli za kimahakama.

Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama, mwaka 2016 jumla ya mashauri 279,331 yamesikilizwa sawa na asilimia 101 ya matarajio ya kusikiliza mashauri 276,147.

Mahakama imefanikiwa kumaliza kesi 248 kati ya kesi 249 za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilizohusisha Ubunge na Udiwani na pia Mahakama Kuu imefanikiwa kuanzisha Divisheni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi (Mahakama ya Mafisadi). Kwa mwenendo huu unatia moyo kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles