25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MCHANGA WA MADINI WAMSOMBA MNYIKA

Na MAREGESI PAUL–DODOMA

MJADALA wa Wizara ya Nishati na Madini jana uliingia doa, baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuagiza askari wa Bunge wamtoe bungeni kwa nguvu Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.

Tukio hilo lilitokea saa 5:20 asubuhi, wakati Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alipokuwa akichangia bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018. Bajeti hiyo iliwasilishwa juzi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Kabla Mnyika hajatolewa nje, awali Lusinde alianza kumpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hatua aliyochukua hivi karibuni ya kuzuia makontena ya mchanga wa dhahabu yasisafirishwe nje ya nchi.

Pia aliwashangaa wabunge wa upinzani, huku akisema wana haki ya kuwaunga mkono wezi wa madini, lakini wabunge wa CCM wana haki ya kumuunga mkono Rais Dk. Magufuli.

“Wabunge wa upinzani mna haki ya kuwatetea wezi, lakini sisi tuna haki ya kuungana na Rais katika jambo hili kwa maslahi ya Taifa.

“Kuna mbunge mmoja hapa amesema kwanini Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, hajachukuliwa hatua wakati waziri wake amechukuliwa hatua. Hivi mimi nawauliza, Kafulila (David) alipofukuzwa Chadema, Mbowe (Freeman) naye alifukuzwa?

“Hivi Zitto alivyofukuzwa Chadema, Dk. Slaa naye alifukuzwa, au marehemu Chacha Wangwe alivyofukuzwa, Mbowe naye alifukuzwa?

“Acheni hizo, hiyo biashara ya kuuza ng’ombe ili tununue bakora hapa haipo, huwezi kujenga zahanati ya shilingi milioni 10 halafu unaiba shilingi milioni 200, baadaye unataka tunyamaze.

“Lakini kumbukeni katika wizara zenye maslahi makubwa kitaifa kama hii, wakubwa wana kawaida ya kuwagawa wabunge na hilo limeonekana hapa,” alisema Lusinde, ambaye ni maarufu kwa jina la Kibajaji.

Wakati akiendelea kuchangia, Mnyika aliomba kuhusu utaratibu na aliporuhusiwa na Ndugai, alisema pamoja na Serikali kuzuia mchanga wa dhahabu usisafirishwe nje, bado nchi inaendelea kuibiwa kupitia dhahabu halisi inayoendelea kusafirishwa kwenda nje.

Kwa mujibu wa Mnyika, mikataba yote inayolalamikiwa katika sekta ya madini, iliingiwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, baada ya kusema hayo na kutakiwa kukaa, mbunge mmoja wa CCM alisikika akisema, Mnyika ni mwizi.

Kauli hiyo ilimkera Mnyika, akalazimika kusimama na kumtaka aliyemwita mwizi, athibitishe, lakini Ndugai alikataa na kumtaka akae ili Lusinde aendelee kuchangia.

Baada ya mabishano hayo, Ndugai aliagiza askari wa Bunge wamtoe Mnyika kwa kile alichosema ameshindwa kuheshimu kiti cha spika.

“Sajenti arti arm, njooni mumtoe Mnyika haraka sana mumpeleke nje na sitaki kumuona hapa kwa wiki nzima ijayo,” aliagiza Spika.

Baada ya agizo hilo, askari wanne walimfuata Mnyika, lakini walipomfikia, walishindwa kumtoa haraka kama walivyoagizwa na kumfanya Ndugai aanze kuwafokea.

“Nyie askari wa wapi nyie, naagiza mumtoe halafu mnachelewa, au nyie ni raia, mtoeni haraka anatupotezea muda huyo, tena mpelekeni nje kabisa ya Bunge,” aliagiza Ndugai na kuwafanya askari hao wamshike Mnyika kwa nguvu na kutoka naye nje.

Wakati Mnyika akitolewa nje, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alionekana akimvuta koti mmoja wa askari hao.

Akizungumzia tukio hilo, Ndugai alisema Bunge bado liko imara na kwamba kitendo kilichotokea ni changamoto za kawaida.

 

“Wabunge, Bunge bado liko imara, tutakwenda hadi mwisho na bajeti kuu itapatikana. Hadi sasa hatujatoka kwenye reli, yaliyotokea ni changamoto za kawaida. Nimesikia anasema atakata rufaa, mwacheni akate rufaa, tutamsikiliza.

“Wakati Mnyika akitolewa nje, Esther Bulaya (Mbunge wa Bunda), alikuwa akiwahamasisha wabunge wengine watoke nje, hiyo ni aibu kwa wananchi wa Bunda na kwa wanawake wote nchini kwa sababu wanawake wetu hawako hivyo.

“Katika haya, tayari nimeiagiza Kamati ya Maadili imuite leo leo (jana) na samansi yake apewe leo leo (jana) ili asije akatoroka na Jumatatu tutaanza nao hapa hapa. Lakini pia, wakati Mnyika anatolewa nje, Mdee alikuwa akimvuta koti askari wa Bunge, jambo ambalo si la kawaida. Huyo ningeweza kumchukulia hatua hapa hapa, lakini nasubiri Kamati ya Maadili inishauri. Wote hao, Jumatatu tutaanza nao,” alisema Ndugai.

Ndugai awataka mawaziri wasaidie wabunge wanaowaunga mkono

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amewaagiza mawaziri wanaohusika na Wizara ya Nishati na Madini wawe wanayasaidia majimbo ya wabunge wanaowaunga mkono wakati wa kupitisha bajeti ya wizara hiyo.

Ndugai alitoa kauli hiyo bungeni jana mchana, alipokuwa akijiandaa kuahirisha Bunge hadi jioni.

“Hatua ambazo Rais amechukua kuhusu makinikia, sisi wabunge tupo naye na baada ya kuona uzito wa jambo hili kama mnavyofahamu kwamba spika hajawahi kutoka kwenda kwenye jambo lolote la mradi ama kukagua, niliamua kwenda mwenyewe hadi kule bandarini pamoja na baadhi ya wabunge kukagua makinikia hayo.

“Kwa uzito wa jambo hili, hatuwezi kuwa tunaibiwa halafu tubaki kucheka na kulifanya kama jambo dogo. Haiwezekani, ingawa tunajua katika nchi hii na kwa baadhi ya wabunge, wanasimama na kupinga uamuzi huo wa Serikali.

“Mtu hawezi kusimama na kuwashabikia watu wanaoitia hasara nchi yetu kwa kiasi hicho wakati yeye ni mbunge anatoka kwenye jimbo ambalo madarasa hayatoshi, vyoo vya shule havitoshi, madawati hayatoshi, idadi ya walimu haitoshi, zahanati na dawa ni pungufu, barabara ndiyo hizo na huduma za maji hakuna.

“Lakini wameshimiwa wabunge, ukishaona mbunge anafanya hayo, ujue kuna mshindo nyuma, hapo kuna kitu fulani, ndiyo maana sasa mmeyaona haya yaliyotokea hapa.

“Lakini Wizara ya Nishati na Madini, muwe mnajua wanaosimamia bajeti yenu hadi inapita ni akina nani. Nyie tatizo lenu nini, sihitaji kusema hapa kwa sababu kama ni mpira si unajua pasi unapiga upande gani?

“Pigeni pasi inavyotakiwa na mtaona mwakani watu wamekaa hapa, hii huruma huruma yenu ndiyo inatuletea haya matatizo.

“Yaani nyie, aliyekupitishia bajeti ni mwingine, halafu unashughulika na mwingine, angalieni vizuri kwa sababu hata wananchi wake wakikuuliza, jibu unalo, waambie mbunge wenu alikataa bajeti yangu,” alisema Ndugai.

MAIGE

Wakati huo huo, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alimshutumu Mkurugenzi wa Kampuni ya Acacia kwa kusema ni fedhuli, mwizi na muuaji.

“Huyo Mkurugenzi wa Acacia ni fedhuli kwa sababu baada ya Tume ya Bomani kutoa taarifa yake na mapendekezo fulani, alikataa kukaa meza moja na Serikali, ikiwa ni pamoja na kubadilisha mrahaba aliokuwa akitoa wakati wamiliki wa migodi mingine walikubali.

“Nasema huyo ni muuaji kwa sababu hadi sasa watu 49 wameshapoteza maisha katika mgodi huo na wengine wamepata madhara mbalimbali ya kiafya kwa sababu wanavuta hewa chafu na hawatibiwi.

“Vile vile, nasema ni mwizi kwa sababu familia 4,600 zilizoondolewa kupisha Mgodi wa Bulyankulu eneo la Kakola, hawajalipwa fidia zao.

“Kwa maelezo hayo, nasema kilichofanywa na Rais Dk. John Magufuli ni sawa na Watanzania wote tunatakiwa kumuunga mkono kwa sababu uamuzi huo utalinufaisha Taifa,” alisema Maige.

 

KUBENEA

Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), amelieleza Bunge jinsi Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), alivyohusika katika moja ya mikataba ya sekta ya nishati.

Kubenea aliyasema hayo bungeni jana, alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

“Hakuna mtu anayepinga juhudi za Rais Dk. John Magufuli kuokoa rasilimali za nchi, ila hoja yangu ni kwanini hatuzungumzii kitendo cha ndege kubeba dhahabu bali tunajadili mchanga.

“Rais amemtumbua Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amemtumbua Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, lakini Naibu Waziri hajawajibika.

“Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Dk Medald Kalemani), amefanya kazi pale wizarani tangu mwaka 1999 alipomaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akiwa mwanasheria na amekuwapo hapo hadi alipopata PhD.

 “Kama tunataka kumtoa Muhongo kafara ni lazima Naibu Waziri awajibike na ni lazima tujenge msingi katika Taifa, ni lazima Waziri wa Fedha awajibike, tusiwe na double standard.

“Katika nchi hii, tuna shida serikalini, yaani kuna mawaziri au baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali wanakuwa na maslahi katika mikataba na wanakaa kwenye Baraza la Mawaziri wakati nje wana kampuni yao au ya marafiki zao.

“Bunge la tisa lilipitisha uamuzi mwaka 2008 juu ya Richmond, lakini maazimio yale hayajatekelezwa. Kuna mtu anaitwa Bashiru Mrindoko ambaye alikuwa Kamishna wa Madini pale Wizara ya Nishati na Madini na alitajwa kuwa ni miongoni mwa watu wanaopaswa kuwajibishwa na Rais mwaka 2008.

“Lakini, mwaka 2010 Mrindoko alitoa kibali kwa Kampuni ya Singida Wind Power Project Limited iendeshe umeme wa upepo Singida, wakati baadhi ya wamiliki wa kampuni hiyo, wako humu bungeni.

“Mwambalaswa ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo na alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini na pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco na ndiye rafiki mkubwa aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe. Sasa, katika mazingira hayo, Taifa litawezaje kupata mikataba mizuri?

“Kwa kuwa Serikali ya CCM iko madarakni muda mrefu na sasa mnataka tuwe wazalendo kwa kuungana na ninyi wakati Taifa linaangamia, hatupo tayari kwa sababu Rais amekosea kuzuia makontena yasisafirishe mchanga wa dhahabu nje,” alisema Kubenea.

NGELEJA

Wakati huo huo, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), alisema hakuna haja ya kuvutana juu ya uamuzi wa Rais Magufuli, bali kinachotakiwa ni kushirikiana ili mikataba inayolalamikiwa ipitiwe upya.

“Mimi nimekaa pale wizarani kwa miaka mitano na nusu na ninajua sera mpya ya madini ilipatikana mwaka 2009 na mwaka 2010 tukapata sheria mpya ya madini. Wanaosema ripoti ya Bomani haikufanyiwa kazi wanakosea, kwa sababu baada ya kuiona na kuanza kuifanyia kazi, ikaonekana gharama ya kujenga kiwanda cha kuchenjulia madini ni kama shilingi bilioni 600 hadi 800.

“Kwa hiyo, mimi kama waziri wa wizara hiyo ninayetarajia kufikisha miaka mitano Juni 4, mwaka huu tangu nilipojiuzulu, naomba tupitie mikataba yote ya madini kwa sababu kuna vipengele vinaruhusu kuipitia kila baada ya miaka mitano,” alisema Ngeleja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles