31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MCHAKAMCHAKA UREJESHWE SHULENI – SAMIA

samia-suluhu

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, imeagizwa kurudisha mchakamchaka shuleni kama zamani.

Agizo hilo lilitolewa jana Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakati wa ufunguzi wa kampeni ya kufanya mazoezi kitaifa ambayo imelenga kuhamasisha jamii kufanya mazoezi kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.

“Zamani wakati sisi tunasoma, tulikuwa tunakimbia mchakamchaka na uliwekwa makusudi kwani tulipata fursa ya kufanya mazoezi.

“Leo hii shuleni hakuna mchakamchaka, Waziri wa Elimu aurudishe kama awali, wanaweza kusema kwamba umbali wanaotembea watoto tayari ni mazoezi, hapana, mchakamchaka una nafasi yake na ni wa muhimu, wapange jinsi itakavyokuwa,” alisema.

Pia aliziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinarudisha viwanja vya michezo vilivyouzwa ili wananchi wavitumie kwa kufanya mazoezi.

“Kila halmashauri ihakikishe viwanja vya michezo vilivyouzwa vinarudi kwa wananchi, wakishindwa watafute vingine na Jeshi la Polisi lisimamie bodaboda na bajaji zisipite kule katika njia za watembea kwa miguu, maana watu wanafanya mazoezi ya kukimbia,” alisema.

Akizungumzia kampeni hiyo, Samia ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema imezinduliwa kutokana na kuongezeka kwa watu wanaougua magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.

“Tunaendekeza usasa, usharobaro, hatutaki mazoezi, lakini tunajiumiza, nawaagiza wakuu wa mikoa na wilaya watenge kila Jumamosi ya pili ya mwezi watu wafanye mazoezi.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza yanachangia asilimia 27 ya vifo vyote duniani.

“Utafiti wa mwaka 2012 hapa nchini uliohusisha wilaya 53, ulionyesha viashiria hatarishi vya magonjwa haya. Asilimia 26 walionekana kuwa ni wanene kupita kiasi, asilimia 26 walikutwa na lehemu nyingi mwilini, asilimia 33 wana mafuta mengi, asilimia 9.1 wana ugonjwa wa kisukari, huku asilimia 25.9 wakiwa na shinikizo kubwa la damu,” alisema Ummy.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema anatamani kila mwananchi katika mkoa wake atakayebainika kuugua kwa uzembe magonjwa yasiyoambukizwa, atozwe gharama ya matibabu mara mbili.

“Wengi wanaougua kwa kutokufanya mazoezi, gharama inakuwa kubwa kwa Serikali, leo (jana) imeitishwa kampeni, lakini wengine wamelala, natamani kupendekeza atakayeugua kizembe, atozwe mara mbili, kama ni Sh 300,000 basi atozwe 600,000 ili tubadilike,” alisema Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles