28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Mcameroon atozwa faini ya Sh milioni 100

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

RAIA wa Cameroon, Kohnson Tebo (32), ametiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 100 na Dola za Marekani 84,300 alizokutwa nazo zimetaifishwa.

Mshtakiwa huyo angeshindwa kulipa faini hiyo, alitakiwa kwenda jela miaka mitatu kwa kosa la kushindwa kutoa maelezo ya fedha alizokutwa nazo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA).

Hukumu hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashidi Chaungu baada ya mshtakiwa kukiri makosa yake.

Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro aliomba mahakama pamoja na adhabu ya kulipa faini, fedha zitaifishwe kuwa mali ya Serikali.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai Februari 27 mwaka huu katika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, uwanja namba tatu, mshtakiwa alikuwa akiondoka nchini akiwa na Dola za Marekani 84,300 bila kuzielezea kwenye Mamlaka ya Forodha ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa alikiri makosa na kusomewa maelezo ya awali dhidi ya mashtaka yanayomkabili.

Inadaiwa mshtakiwa, mkazi wa Linde, Cameroon ambaye ni mfanyabiashara, aliingia nchini Februari 26, mwaka huu na kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo Mamlaka ya Forodha, hakueleza kama anaingia na fedha zozote.

Wakili Wankyo alidai Februari 27 alikuwa akiondoka nchini kupitia ndege ya Rwanda na alikuwa na tiketi ya kielektroniki pamoja na hati ya kusafiria.

Aliieleza mahakama kuwa ndege hiyo ilikuwa ikiondoka saa 11.40 jioni kuelekea Kigali na baadae Duoala, Cameron.

Wakili Wankyo alidai mshtakiwa huyo alikuwa ameshikilia begi mkononi na akiwa uwanjani alianza utaratibu wa kuingia na akapita kwenye mashine ya kwanza ya ukaguzi, alipoenda kwenye mashine ya pili ili aingie kwenye chumba cha kusubiria abiria, kitu kisicho cha kawaida kiligundulika katika begi lake.

Inadaiwa alielekezwa aache mkoba wake kwenye mashine kwa mara ya pili ambapo kitu kisicho cha kawaida kilibainika.

“Aliamuliwa kutoa kila kitu kilichokuwa kwenye begi, fedha hazikuwa miongoni mwa vitu vilivyotolewa.

“Wakati begi tupu lilipowekwa kwenye mashine ilibainika kuwa ndani ya begi kwa chini zilifichwa fedha. Sehemu hiyo ilipopekuliwa ilibainika Dola 84,300 za Marekani zilifichwa,” alidai Wankyo.

Alidai fedha zilizokamatwa ziliwekwa kwenye akaunti katika Benki ya NMB na namba zake zilinakiliwa. 

Inadaiwa kumbukumbu za Uhamiaji zinaonyesha kuwa mshtakiwa aliingia nchini Februari 26, 2020 kama mtalii na kupewa viza ya utalii, hakutembelea kituo chochote cha utalii na alipoingia nchini hakueleza kama alikuwa na fedha za Marekani. 

Ushahidi ulikuwa unaonyesha wazi kuwa mshtakiwa alikuwa anaondoka nchini bila kueleza Mamlaka ya Forodha fedha alizokuwa nazo. 

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles