24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mbwa wanavyokwaa nyadhifa za kisiasa Marekani

HASSAN DAUDI Na MITANDAO

WAKATI ikionekana kuwa ni jambo geni na la kushangaza pia, nchini Marekani ni kawaida kwa wanyama aina ya mbwa kushika nyadhifa za kisiasa.

Unaweza kuliona hilo katika maeneo ya California, Minnesota, Colorado, Kentucky na San Francisco.

Katika maeneo hayo, wapo mbwa waliochaguliwa na wengine wako mbioni kuwa mameya wa manispaa wanazoishi.

Mfano; kuanzia mwaka 1981 hadi 1994, Manispaa ya Sunol, California, ilikuwa ikiongozwa na mbwa aliyepewa jina la Bosco.

Wakati wa kampeni, ilionekana kuwa Bosco angeshindwa kwa kuwa alikuwa mnyama, lakini aliwashangaza wengi kwa ushindi wake mbele ya wanasiasa wawili.

Akiwa na wananchi takribani 1,000, mbwa huyo aliiongoza Sunol kwa miaka 13 na hata kung’oka kwake madarakani ni baada ya kufariki mwaka 1994.

Ukiachana na Bosco, yupo mbwa mwingine aliyepewa jina la Lucy Lou, ambaye aliweka rekodi ya kuwa ‘mwanamke’ wa kwanza kuwa meya wa Rabbit Hash, akiongoza kuanzia mwaka 2008 hadi 2016.

Lucy Lou aliingia madarakani baada ya mbwa mwingine aliyekuwa akiitwa Goofy kuachia madaraka hayo. Goofy aliingia kwenye uongozi kupitia uchaguzi wa mwaka 1998.

Hata alipoondoka madarakani kipindi hicho si kwamba alibwagwa kwa kura, bali ni kwa kuwa aligombea kiti cha urais, ambacho hata hivyo kura zake hazikutosha. Mbwa huyo alifariki mwaka jana.

Mbali ya huyo, mwingine ni Brynneth Pawltro, ambaye ndiye aliyekalia kiti cha Lucy Lou, katika Manispaa ya Rabbit Hash. Alishinda nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2016 baada ya kuwagaragaza paka na punda.

Katika orodha hii, Manispaa ya Idyllwild, California, nayo inaingia ikiwa na historia ya kuongozwa na mbwa aitwaye Max baada ya uchaguzi wa mwaka 2013. Max II alikalia kiti kilichokuwa kimeachwa wazi na mbwa mwenye jina hilo pia.

Wakazi wengi wa eneo hilo, walimtambua Max II kuwa ni kiongozi aliyependa kutumia mapumziko yake ya mwishoni mwa wiki kuzunguka bararani na kuyafikia maeneo mbalimbali ya wapiga kura wake, akiwa amevaa tai na hata kofia wakati mwingine.

Kwa upande mwingine, yupo pia Duke, mbwa aliyekuwa meya wa Manispaa ya Cormorant Village, Minnesota. Duke aliingia madarakani baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2014 na kuanzia hapo alishinda awamu mbili mfululizo.

Wengi walishangazwa na ushawishi wake katika uchaguzi wa mwaka 2016, ambapo alijikusanyia kura zote isipokuwa moja iliyokwenda kwa mpenzi wake, Lassie. Bahati mbaya kwa wananchi wa Cormorant Village ni kwamba Duke aliiaga dunia mwanzoni mwa mwaka huu.

Pia katika orodha hiyo anapatikana Pa Kettle, mbwa aliyechaguliwa kuwa Meya wa Divide, Colorado, mwaka 2014. Wakati anawania kuingia madarakani, alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa punda, mbweha, paka na mbwa wengine.

Kuthibitisha ni kwa kiasi gani alikuwa kwenye hatari ya kupoteza, hata ushindi wake haukuwa wa kishindo kwani alimzidi kwa kura 55 pekee aliyeshika nafasi ya pili, mbweha anayeitwa Kenyi, ambaye aliukwaa wadhifa wa naibu meya.

Gus Hall ni mbwa mwingine aliyekuwa meya wa Coronado, California, akiibuka kidedea kwa ushindi mnono wa kura zaidi ya 20,000. Kivutio chake kikubwa wakati wa kampeni ni jina lake, likiwakosha wengi kwa kuwa lilifanana na mmoja kati ya waliokuwa waumini wa sera ya ujamaa nchini Marekani.

Huko Edgewater, eneo linalopatikana Kaskazini mwa Chicago, safari hii nako kuna upinzani mkali wa mbwa watatu wanaowania nafasi ya kuwawakilisha wananchi katika kiti cha meya, ambapo wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa paka na mbuzi.

Ukija kwa wanyama wengine, inakumbushwa kwamba paka aitwaye Stubbs alikuwa meya wa Talkeetna, Alaska, kwa kipindi cha miaka 20. Si tu paka huyo alisifiwa kwa tabia yake ya kupatikana ofisini mara nyingi, pia utawala wake ulipongezwa kwa kutopandisha kodi.

Inaelezwa kuwa Stubbs alianza kutoonekana machoni mwa wananchi wake mwaka 2015, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni umri mkubwa na alifariki mwaka juzi.

Aidha, Lincoln ni jina la mbuzi na ndiye meya wa Fair Haven, Vermont, akiweka rekodi ya kuwa wa kwanza kushika nafasi hiyo alipoteuliwa mwaka huu.

Ni kama ilivyokuwa kwa Clay Henry IV, ambaye pia ni mbuzi na meya wa Lajitas, Texas. Wanaomjua vizuri Clay watakwambia sifa yake kubwa ni kupenda kunywa pombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles