29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNIFU NEMBO YA TAIFA ANAUGUA UTAPIAMLO

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM


RIPOTI ya awali ya uchunguzi wa kiafya aliofanyiwa mbunifu wa Nembo ya Taifa (bibi na bwana), Francis Ngosha (86) katika Kitengo cha Magonjwa ya Dharura Hospitali ya Mkoa ya Amana, inaonyesha kuwa anakabiliwa na tatizo la lishe duni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura Muhimbili ambako mgonjwa huyo kahamishiwa, Dk. Juma Mfinanga, alisema hata hivyo watamfanyia uchunguzi wa kina zaidi kujua iwapo anakabiliwa na matatizo mengine.

“Kwa mujibu wa madaktari wenzetu hapa Amana, walimpokea Ngosha akiwa katika hali ya kuchoka na mwenyewe amewaambia kwamba hana ndugu yeyote hapa Dar es Salaam, anaishi kwa kusaidiwa na wasamaria wema,” alisema.

Alisema wamepokea ripoti hiyo ya wenzao na kwamba wataendelea kumfanyia uchunguzi ili kujua hasa nini kinachomsumbua.

“Wamedokeza kwamba huenda amechoka kutokana na lishe duni, lakini umri wake pia ni mkubwa, inawezekana hali hiyo ni kutokana na uzee, tutakapomaliza uchunguzi wetu tutatoa 'comprehesive' ripoti,” alisema Dk. Juma.

Akizungumza, Ngosha alisema kwa muda mrefu amekuwa akiishi peke yake baada ya mkewe kufariki kwa ajali ya gari.

 

“Nilikuwa naishi na mke wangu tangu mwaka 1977, tulipanga huko Buguruni, lakini yeye amefariki kwa ajali ya gari, hatukujaliwa kupata watoto, wale walionipangisha wananifadhili, hivi sasa silipi kodi ya chumba,” alisema.

Alisema yeye ni mwenyeji wa Misungwi, Kijiji cha Bulima ambako alisoma katika Shule ya Msingi Misungwi darasa la kwanza hadi la nne na kisha kuhamia katika Shule ya Msingi Bwiru ambako alimalizia elimu yake ya msingi.

“Nina dada zangu ambao wamejaliwa watoto wako huko Sengerema, lakini bahati mbaya simu yangu iliharibika, hivyo sina mawasiliano nao kwa muda mrefu na hawajui kama ninaugua hivi sasa,” alisema.

Alisema dereva mmoja wa daladala za Buguruni ndiye aliyepeleka taarifa zake kwenye vyombo vya habari, kwamba anaugua na hana msaada wowote, ndipo wakaenda nyumbani kwake na kumuhoji.

“Bado siwezi kusimama na kutembea peke yangu, ili nisimame na kutembea nahitaji kusaidiwa kwa kushikiliwa na mtu,” alisema.

Akielezea kuhusu nembo hiyo, Ngosha alisema aliichora pamoja na mwenzake Ali Panga mwenyeji wa Tanga ambaye hata hivyo kwa sasa ni marehemu.

“Tulichora nembo hiyo mwaka 1957 baada ya kupewa tenda, tuliambiwa kwamba itatumika pindi Mwenyezi Mungu atakapotujalia kupata uhuru na kweli tulipata,” alisema.

Pamoja na hayo, Ngosha alisema ana mpango wa kumpatia Rais Dk. John Magufuli zawadi ya picha tatu ambazo amezichora.

“Ninazo picha tatu, ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere,  Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na ya kwake mwenyewe (Rais Magufuli ambazo nimepanga kumpatia zawadi,” alisema.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangwalla, alisema kuanzia sasa Serikali itampatia matibabu na huduma za kijamii mzee huyo kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa taifa.

“Mchango wake tunautambua, kwanza tutampatia matibabu, lakini pia tunakusudia kumpeleka kwenye makazi ya wazee ili tumtunze baada ya matibabu kukamilika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles