25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Mbunge wa Nyamagana atwishwa zigo la wahitimu kidato cha sita

Na BENJAMIN MASESE

WAHITIMU wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Twihulumile   Mwanza, wamemuomba Mbunge wa   Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM) kukaa na  wabunge wa chama hicho   kuishauri Serikali kukubali Bodi ya Mikopo  ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HSELB)   itoe mikopo kwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi.

Ombi hilo lilitolewa juzi na Asha Omari  kwa niaba ya wahitimu wenzake  wakati wa mahafali yao   katika risala yao kwa mgeni rasmi, Mabula ambaye aliwakilishwa na Diwani wa Kata ya  Nyegezi, Edith Mudogo (CCM).

Walimtaka mbunge huyo  kukaa  na  wabunge wenzake  kuishauri Serikali kupitia wizara ya elimu na bodi ya mikopo kuangalia upya mfumo wa utoaji mikopo  kuwawezesha wanafunzi waliosoma kwenye shule binafsi kupata fursa hivyo sawa na wahitimu waliosoma shule za umma.

Omari alisema hawafurahishwi  kuona  namna Serikali inavyowabagua wanafunzi waliosoma kwenye shule binafsi na kuwapa unafuu waliosoma kwenye  shule za umma wakati wote ni watanzania.

“Kusoma kwenye shule binafsi  hakumaanishi wazazi wao wana uwezo mkubwa wa  uchumi bali hujikamua na kujinyima  kuwawezesha kupata haki ya elimu baada ya kukosa fursa kwenye shule za serikali.

“Hivyo tunaomba utusaidie kufikisha kilio chetu bungeni kwa waziri wa elimu aone utaratibu unaofaa wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wanaojiunga na vyuo vikuu bila kujali shule walizosomea.

“Kama mbunge unayetokana na CCM tunaomba ukae na wabunge wenzako  muishauri Serikali na bodi ya mikopo ili na sisi tupate fursa hiyo,” alisema Omari.

 Hata hivyo  walimpongeza Rais  Dk. John Magufuli  kwa kuboresha  huduma za jamii  zikiwamo elimu bure, afya, maji,umeme na barabara  huku  utulivu kwa wafanyabiashara wadogo (machinga)  ukiiamarika  baada ya kuwatetea na kuwatengenezea vitambulisho.

 Akijibu risala hiyo,  Mudogo  alisema maombi yao ya mikopo atayafikisha kwa mhusika kama   na kuwataka wahitimu hao  kuendeleza nidhamu waliyokuwa nayo shuleni baada ya kuingia uraiani ambako kuna changamoto na tabia mbalimbali.

Aliwashauri kujiepusha kufanya vitendo vya ngono   kuepuka kuambukizwa Ukimwi ambao umeendelea kuteketeza nguvukazi ya taifa. 

“Elimu ndio kila kitu katika karne hii ambayo itaondoa changamoto  mbalimbali na ni ufunguo wa maisha.

“Niwapongeze walimu na wazazi kuona umuhimu wa elimu kwa sababu  ni urithi pekee wanaostahili kupewa watoto, utampa vyote mtoto vitakwisha lakini elimu akishaipata haiwezi kutoka kichwani,”alisema.

  Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Buhongwa, Paul Mbinayamaswa alisema serikali ya awamu ya tano ni sikivu, inasikiliza maombi ya wahitimu hao kuhusu utaratibu wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanaochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu.

Awali, Mkuu wa shule hiyo,  Michael Boniface alisema  licha ya kuwapo na  changamoto   shule  imepata mafanikio makubwa ya  taaluma tangu kuanzishwa kwake.  Hata hivyo alisema imani yake kwa wahitimu hao 44 ni  kupata ufaulu  wa daraja la kwanza, pili na tatu  kwani wana uwezo mkubwa wa  taaluma

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,430FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles