24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE MWINGINE CHADEMA YAMKUTA

Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema)

 

Na KULWA MZEE -DODOMA

BUNGE limemsimamisha Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema) kuhudhuria vikao vitatu, huku likimsamehe Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), baada ya kukiri kosa la kudharau mamlaka ya Spika.

Uamuzi huo ulifikiwa bungeni jana baada ya Bunge kuridhishwa juu mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili wabunge hao.

Kwa upande wa Rwamlaza, adhabu hiyo ilitolewa baada ya mbunge huyo kuthibitika alisema uongo, kwamba Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), alitumia madaraka yake vibaya kujimilikisha zaidi ya ekari 4,000, wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kabla ya uamuzi huo wa Bunge, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, iliwaita wabunge hao na kuwahoji kisha kuwatia hatiani na kupendekeza adhabu hizo.

Wakati Rwamlaza akiadhibiwa kwa kosa hilo,   Nassari alikuwa anatuhumiwa kudharau mamlaka ya kiti cha Spika na kufanya fujo bungeni kwa kutupatupa vitabu na kusababisha usumbufu wakati Bunge likiendelea, Mei mwaka jana.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, George Mkuchika, alisema kutokana na maneno yaliyotolewa dhidi ya Profesa Tibaijuka, mbunge huyo alimwandikia Spika akimlalamikia Rwamlaza na kudai kuwa hayakuwa na ukweli wowote.

Wakati wa kujadili malalamiko hayo, Mkuchika alisema Rwamlaza alitakiwa kufika mbele ya kamati na kujibu ni kwa nini asichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka kanuni ya 63 (1) na 64 (1)(a) ya kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januari 2016.

“Baada ya mbunge huyo kujieleza mbele ya kamati, alisema hana uhakika kama Profesa Tibaijuka anamiliki ekari zaidi ya 4,000 isivyo halali, bali aliambiwa na wanakijiji wa Kyamyorwa.

“Kwa upande wake, Profesa Tibaijuka alisema shamba hilo alianza kulimiliki mwaka 1991 baada ya mumewe kufariki na mwaka 1,997 lilipimwa akapewa hati.

“Pia, alisema kwamba wakati anamilikishwa hilo shamba, hakuwa waziri kwani uwaziri aliupata mwaka 2010.

“Kutokana na hali hiyo, kamati iliona Profesa Tibaijuka anamiliki kihalali shamba hilo lenye ekari 1,098 kisha inapendekeza Conchesta apewe adhabu ya kutohudhuria vikao vitatu.

“Nassari alipotakiwa kujieleza mbele ya kamati,

alikiri kuwa alifanya fujo bungeni jambo ambalo kamati iliona asamehewe kwa sababu alikiri kosa na ni mara yake ya kwanza kufanya kosa,” alisema Mkuchika.

Kuchukuliwa hatua kwa wabunge hao kumekuja baada ya wabunge wengine wa Chadema, Halima Mdee (Kawe), Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Bunda Mjini) na John Mnyika (Kibamba) kuadhibiwa hivi karibuni baada ya kupatikana na hatia bungeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles