27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Mbunge: Mtaona matokeo ya kuzaa mwaka 2021

BENJAMIN MASESE -RORYA

MBUNGE wa Rorya, Lameck Airo (CCM), amesema matokeo zaidi ya elimu bure yataanza kuonekana kuanzia mwaka 2021 kutokana na Watanzania kuruhusiwa kuzaa bila kikomo.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi   kuendelea zaidi kujenga vyumba vya madarasa shule za msingi na sekondari kwa kuwa idadi ya watoto watakaojiunga na shule hizo watakuwa wengi zaidi.

Kauli hiyo aliitoa kwa nyakati tofauti hivi karibuni akiwa katika mikutano na wananchi wa jimbo hilo.

Airo alisema vyumba vya madarasa vilivyopo katika shule za msingi na sekondari havitatosheleza mahitaji kuanzia mwaka 2021 na kuendelea kwa kuwa watoto watakuwa wengi.

 “Tusijidanganye kwamba vyumba vya madarasa vilivyopo vinatosheleza kwa watoto wetu, kumbukeni baada ya Serikali kutangaza elimu bure mmeshuhudia idadi kubwa ya watoto ikiongezeka shuleni, hasa shule za msingi.

“Fikirieni elimu bure imeanza mwaka gani na watoto hao watakwenda sekondari mwaka gani, mtagundua nini kinakuja kujitokeza.

“Pia kumbukeni hivi sasa Rais Dk. John Magufuli amesema tuzae tu na mimi naunga mkono kwani  wingi wa watu ni mtaji katika taifa, lazima tujiandae kupokea matokeo yake hapo mbeleni.

“Kuanzia mwaka 2021 tutaanza kupokea matokeo kwa shule za sekondari kwani watoto watakaojiunga na kidato cha kwanza watakuwa wengi zaidi.

“Pendekezo langu katika jimbo hili tuendelee kujenga vyumba vya madarasa na kila shule tuwe na wastani wa vyumba 20 vya ziada ambavyo vitaweza kupokea watoto wetu ifikapo 2021 na kuendelea, ardhi tunayo tusihofie kuzaa.

“Hii Shule ya Sekondari Nyamtinga nitatoa malori ya kusomba mchanga na mawe ili viwe hapa kwa ajili ya ujenzi wa baadaye, pia vyumba ambavyo vimejengwa kwa nguvu ya wananchi nitatoa mabati ya kuezeka,” alisema.

Mbali na Sekondari ya Nyamtinga, Airo pia alitembelea Shule ya Msingi Rwang’enyi na kutoa msaada wa tanki la maji lita 5,000, mabati 200, saruji mifuko 100 na kuwataka madiwani na viongozi wengine wa vijiji kusimamia shughuli za maendeleo.

Akiwa Komuge, Omuga, Nyasoko, Kowak na Nyathorogo, aliwataka wananchi kujenga nyumba za kudumu ili waweze kupata umeme kutoka Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) awamu ya tatu kwa kuwa Serikali imekusudia kusambaza nishati hiyo vijiji vyote nchini.

Katibu wa CCM Wilaya ya Rorya, Aveline Ngwaba, alishangazwa na vitongoji vya Kururya na Mbatamo kujenga shule za sekondari mbili wakati maeneo mengine yana vitongoji tisa, lakini wameshindwa kukamilisha majengo ya shule yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles